Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba Mheshimiwa Waziri amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuzungunguka kwenye Mikoa yetu kufuatilia shida ya maji na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hilo tu mnalifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa kwamba kama Wabunge tunakubaliana mimi ningetoa hoja ama mtu yeyote atoe hoja kwamba Wizara hii tusiipitishe mpaka Waziri wa Fedha aje kutoa commitment ndani ya Bunge kwamba kwa nini fedha za miradi ya maeneleo hazipelekwi kwenye Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya chama kinachoongoza, Chama cha Mapinduzi, hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati anazindua Bunge aliongea kwa msisitizo kwamba anakusudia kuhakikisha kwamba anamtua mama wa Kitanzania ndoo kichwani na Watanzania walimfuatilia na wakamshangilia tukadhani kwamba yale yanayoongelewa tutakuja kuyaona sasa kwenye utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nipate majibu yafuatayo na wa kutujibu upande wa Serikali ambao ninyi ndiyo mmepewa dhamana na wananchi, upande wa Chama cha Mapinduzi, mtueleze sekta ya maji mmeipa kipaumbele cha ngapi kwenye vipaumbele vyenu. Haiwezekani kwamba Watanzania waliopo vijijini mpaka leo wanaopata maji ni asilimia 56 pekee, haiwezekani, hizi asilimia 44 wanaishije? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi ilianzishwa na World Bank na World Bank wakati wanaanzisha mradi walitoa fedha dola za Kimarekani bilioni 1.4, miaka saba ya utekelezaji wake shida ya maji iko palepale. Hili linatokana na kwamba kulikuwa na usimamizi mbovu wa miradi mingi ya maji iliyokuwa inatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukawa tunapambana na individuals, kuamini kwamba labda Waziri hafanyi kazi, Naibu Waziri hafanyi kazi ama Katibu Mkuu hafanyi kazi, tatizo ambalo linapelekea Watanzania kukosa maji ni mfumo na inawezekana hakuna political will waliyonayo Chama Tawala ya kutatua matatizo ya maji, inawezekana hakuna political will. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa nane na wa tisa inaelezea upatikanaji wa maji vijijini na mijini. Takwimu hizi ambazo Mheshimiwa Waziri amezisoma zina-contradict sana na uhalisia. Lakini pia hata hizi takwimu zenyewe zinajikanganyakanganya ukizisoma na ukazipitia ukafanya calculation kidogo zina tofauti. Kwa mfano, upatikanaji wa vyanzo vya maji kwa Jiji la Dar es Salaam unaonesha kwamba kwa sasa umeshuka kutoka asilimia 85 mpaka asilimia 76, lakini upatikanaji wa vyanzo vya maji siyo upatikanaji wa maji kwa wananchi kwa sababu haya maji yanahitaji usambazaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukienda ukaangalia namna mtandao wa maji ulivyosambazwa na vyanzo vya maji vilivyopo ni tofauti, na ndiyo maana leo ukifanya mahesabu wakazi wa Dar es Salaam anaopata huduma ya maji, waliounganishiwa kwa huduma ya bomba hawafiki hata robo ya wakazi wa Dar es Salaam. Hili ndilo tatizo, unaweza ukaona kwamba kwenye takwimu tunasema kwamba watu wengi wa Dar es Salaam wanapata huduma kumbe wanaopata huduma ni wachache, walio wengi tunaishi Dar es Salaam, tunatumia maji ambayo mengine siyo salama ni yale maji ya kuchimba wenyewe. Ukifanya research Dar es Salaam watu wengi wamechimba maji chini, yale maji ambayo siyo salama sana lakini mtandao wa maji wa Ruvu Chini, Ruvu Juu na vyanzo vyote vya Dar es Salaam, bado havijawafikia wakazi wengi wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda maeneo ya Temeke, Mbagala huko Chamazi, Kigamboni na maeneo mengi, ukienda ukiangalia mtandao wa maji Dar es Salaam unaona kabisa kwamba maji hayawajafikia, sisi tunaishi Dar es Salaam karibu wote hapa tuna makazi yetu Dar es Salaam tunajua. Kwa hiyo, hizi takiwmu zenyewe ambazo Mheshimiwa Waziri amezisema kidogo zina mashaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nirudi upande wa Wizara ya Fedha na labda Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, hivi Serikali ina diplomatic complication na wahisani tunajiuliza? Ukisoma hotuba ya bajeti ya mwaka 2017 na ya mwaka huu, fedha ambazo wahisani walihaidi kuzitoa hazijatolewa mpaka sasa. Sasa wakati mwingine unajieleza inawezekana Bunge linapaswa kufahamishwa kama kuna matatizo ya kiplomasia baina ya Tanzania na wahizani wetu tuelezwe ili tujue kwamba kinachoendelea kumbe hatupati fedha za wahisani kwa sababu tumenasanasa hapa ili Bunge lichukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wakati tunajadili bajeti hapa ilielezwa kulikuwepo na dola milioni 503 na wako Wabunge waliishabikia kwamba fedha hamuioni kuna dola milioni 503 ipo, mpaka leo mbona haionekani kwenye utekelezaji wala kwenye kitabu humu hakuna. Hiyo dola milioni 503 iliyokuwa imesemwa mwaka jana na tukaambiwa kwamba Waziri wa India alishakuja na ametia sahihi sasa kilichokwama ni wapi, tumenasa wapi ili dola milioni 503 ili iweze kwenda kukamilisha miradi yetu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukiangalia Wabunge tunaweza tukasemaa sana hapa, lakini jambo la maji kwa sasa, kwa upatikanaji wa fedha za maendeleo wa asilimia 22 nilidhani Wabunge leo tungesimama pamoja tukasema tunahitaji commitment ya Serikali ama taarifa ya Serikali very intense watuleleze ndani ya Bunge kwamba kwa nini Wizara ya Maji haipewi fedha za maendeleo, haingii akilini kuona Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inapewa asilimia 0.85. Sasa hii mishahara ambayo inalipwa wafanyakazi, wanalipwa ili wafanye kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaweza kuona kwamba tatizo watu wengi wanaweza kusema kwamba kuna tatizo labda kwenye utendaji tunaweza tuka-deal na personalities, tunaweza tukaona kwamba Katibu Mkuu labda tatizo, ama Waziri tatizo ama Naibu Waziri, kumbe tatizo ni mfumo kwamba fedha hazitolewi labda Waziri wa Fedha anakipaumbele chake yeye tofauti na kipaumbele ambacho vimetajwa kwenye ilani ya chama chenu ama kile kipaumbele ambacho Mheshimiwa Rais alikitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji maelekezo ya kina mje kutueleza namuona Naibu Waziri wa Fedha yupo, jambo la maji ni jambo tete, huko vijijini tunakotoka Watanzania wana shida kubwa ya maji na hili tatizo linapelekea kuwa na tatizo lingine la magonjwa ya mlipuko, kwa sababu maji wanayopata Watanzania ni maji ambayo siyo maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukaongea sana hapa tukajenga hoja tunavyoweza kujenga. Lakini suala linabaki palepale kama Waziri amepewa asilimia 22 ya fedha za maendeleo afanye nini, hiyo asilimia 22 tunaigombania hapa na unajua likitokea swali hapa la Wizara ya Maji, Wabunge wote tunasisima humu kila mtu ana shida ya maji, lakini asilimia 22 ikafanye nini! Wewe mwenyewe leo umeelezea suala la maji Ilala na maeneo mengine, lakini pia kuna haja kubwa ya kuipitia mikataba ya karandasi za maji ambazo zilitolewa pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kubwa upo mradi wa maji uko pale Longido, nilikuwa kwenye Kamati ya maji tuliutembelea mwaka huu una shida kubwa Mkandarasi yupo amepewa fedha zaidi ya asilimia 80 amelaza mabomba tu hakuna kinachofanyika. Kwa bahati mbaya watendaji wa Wizara yako ambao ndiyo waliingia mkataba wanautoa sasa wanataka kujivua baada ya kuona wanaenda kukwama wanawapelekea watu wa Arusha Water Supply ili wakausimamie. Kwa hiyo, mwisho wa siku mtakuja kuona kwamba kumbe usimamizi mbovu umepatikana Arusha Water Supply Agency kumbe tatizo ni Wizara yako. Hivyo, kuna tatizo kubwa pia la kuingia mikataba

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa nini taasisi za Serikali hazilipi ankara za maji, huu ni mtihani mwingine. Nikiwa Kamati ya Maji tulitembelea katika Mamlaka ya Maji pale Moshi tulikuta Chuo cha Polisi cha Moshi kinadaiwa shilingi milioni 900, RPC wa Moshi anadaiwa shilingi milioni 300 anaambiwa kwamba sasa tukufungie mita za prepaid anakataa anagoma. Sasa unaweza kuona kwamba kumbe tatizo linalokwamisha maji wakati mwingine maeneo ya mijini ni taasisi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa Arusha yule Mtendaji Mkuu wa Idara ya Maji Arusha aliieleza Kamati kuwa kama Serikali inaweza ikalipa madeni yake yote, yeye hahitaji ruzuku kutoka Wizarani kwako, inakuwaje sasa Idara za Serikali zinatengewa bajeti tunaidhinisha humu kwenye Bunge, bajeti inakwenda wanatumia huduma za maji hawataki kulipa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo siyo tu kwamba mfumo wenyewe haupeleki fedha kwenye Wizara ya Maji, pia hata mfumo hautaki kuzisimamia Taasisi na Idara za Serikali zikaweza kulipa bill zake ili wananchi wakaweza kupata huduma za maji. Hii nayo ni changamoto nyingine Mheshimiwa Waziri unakutana nayo.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye kitabu chako hapa kuna uchimbaji wa visima vya DDCA nami nimekuomba, Mheshimiwa Waziri naomba vile visima uviweze kuvikamilisha ili wananchi wa Jimbo la Mchinga wapate huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.