Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia hoja hii ya maji ambayo ni muhimu sana. Tatizo hili sijui kama ni sugu au ni donda ndugu au ni nini, lakini ni tatizo kubwa sana hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo mengi sana katika kipindi cha miaka miwili na nusu. Tumeshuhudia mambo mengi kwenye sekta mbalimbali za afya, miundombinu, lakini sekta ya maji bado Awamu ya Tano haijashughulikiwa ipasavyo. Nashauri sasa hivi mwelekeo uende kwenye maji. Suala hili sasa hivi ni tatizo siyo katika Jimbo la Muheza tu, Jimbo la Muheza naweza kusema sijui ni sugu au ni donda ndugu, lakini ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu juhudi ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wanashughulika sana kutatua tatizo la maji, lakini hawana hela. Mipango ambayo ipo kwenye kitabu hiki kama ingetekelezwa ninaamini kabisa tungeweza kupunguza sana tatizo la maji. Kama mambo ambayo yametajwa kwenye kitabu hiki fedha zingeenda kutolewa, basi tatizo hili tungeweza kulipunguza kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona aibu sana kwa sababu Tanga sasa hivi kuna miradi mikubwa ambayo inakuja na unapopita kwenda Tanga huachi kupita kwenye Jimbo la Muheza, ni lazima upite Muheza. Ninyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge, unapopita Muheza unapopita
Lusanga unakwenda Mkanyageni, Ngomeni, Kilapula unakaribishwa na madumu ya maji barabarani. Madumu ya maji watu wanasubiri kwenda kuchukua maji Tanga. Sasa hii kitu inanisononesha sana na ninaona aibu sana. Kwa kweli suala hili ni gumu na ninaomba sana Wizara iweze kuliangalia kwa sababu ndiyo miradi ipo mingi, lakini inachelewa kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Wizara kwa kuanzisha mradi wa Pongwe. Pongwe mpaka Muheza tumechukua maji na huo mradi umeanza kufanya kazi. Nawashukuru sana tena sana kwa sababu mradi huu tuliutegemea tuufungue mwezi huu, lakini naona itashindikana labda baada ya miezi miwili au mitatu ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nashukuru kwa sababu Mheshimiwa Waziri wenyewe na Maofisa wake wote kwa kweli wanashughulika sana ili kuhakikisha kwamba haya maji yanafika Muheza Mjini kama ilivyopangwa ili wananchi wa Muheza waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru Wizara kwa kuweza kuangalia vyanzo, vijiji vingi vya Mashewa kule Amani ambavyo vinazungumza Mto Zigi vimeweza kupata maji, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi bado nina miradi ya vijijini, najua nimepangiwa hela hapa karibu shilingi bilioni
1.169 na ninaamini kabisa kwamba kuna miradi ambayo tuliipanga kwenye mwaka uliopita haikutekelezwa. Mradi wa kutoa maji kutoka Mto Pangani wa Kirongo, Mradi wa Umba – Ngomeni, Mradi wa Mkwakwa – Mafleta na mradi wa Tongwe. Hii miradi ipo kwenye hatua za kuwekewa sign. Sasa tunaamini kabisa kwamba haitasita na tutaendelea ili iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kimoja ambacho nimesikitika sana ni hii miradi 17. Miradi 17 ya mkopo wa India dola milioni 500 imekuwa kama ni kichekesho sijui ni sindimba au ni nini. Miaka miwili iliyopita tumeambiwa hapa, Waziri Mkuu wa India amekuja ameweka saini Ikulu pale, miradi 17 Muheza ikiwemo, sasa hivi hapa Mheshimiwa Waziri kwenye taarifa yake anasema majadiliano yanaendelea. Mwenyekiti wa Kamati anasema issue ipo kwenye vetting kwa Attorney General. Sasa sijui tuamini ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-windup atuhakikishie kwamba kweli hiyo financial agreement imeshasainiwa? Maana yake tatizo lilikuwa ni financial agreement, kila siku financial agreement, sasa imeshasainiwa ili tuweze kujua kama ni nini? Kama ipo kwa Attorney General, hiyo issue ya vetting, Attorney General imefikia wapi? Hiki kitu miaka miwili na nusu inazungumzwa hapa! Ninaamini miradi hii ingeanza, ingeweza kupunguza sana tatizo la maji kwa sababu ni miradi ambayo ime-cover karibu nchi nzima mpaka Zanzibar, sasa kwa nini haitekelezwi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni suala la tozo ya mafuta. Hili suala ni la muhimu sana kwa sababu takwimu zinaonesha kwamba hizi tozo hata Hazina hawaziingilii, zinakwenda moja kwa moja na Wizara ya Maji wanazishughulikia hizi. Ukishapeleka hati mara moja tu unapewa hela zako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiria kwamba Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono wazo lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamati, lazima tozo hii ya shilingi 50 iongezwe iwe shilingi 100. Kwa kweli bila kufanya hivyo Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Fedha wakati wa kupitisha Financial Act hapa itakuwa ni matatizo. Hatutakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naona muda haupo kwangu, nakushukuru sana na ninashukuru kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja.