Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri anayofanya hasa katika sekta hii ya elimu. Pia niwapongeze sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako na mtani wangu Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi njema ambayo mnaifanya katika sekta hii. Mimi naamini mnaandika historia na historia itawakumbuka, mnafanya kazi njema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ya jambo ambalo linabezwa humu ndani la elimu bila malipo au elimu bure. Hili ni jambo kubwa kabisa ambalo alianza nalo Mheshimiwa Rais wetu na tukaanza kwa kupeleka shilingi bilioni 18.77 tulipoanza Serikali ya Awamu ya Tano. Tumeongeza tukaenda shilingi bilioni 20.24 leo tunapoongea kwa kila mwezi tunapeleka zaidi ya shilingi bilioni 23.876. Hii ni dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba inataka kuwaondoa watoto wa maskini, wale ambao walikuwa hawaendi shule sasa waende shule wasome bila tatizo. Si vizuri sana tukabeza kila jambo kwa sababu tu mimi ni mpinzani, mimi ni vile lakini hapana, tutende haki katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ningependa kulisemea katika dakika hizi chache ni mchango wa sekta binafsi kwenye sekta hii ya elimu. Kama Serikali tunathamini sana mchango wa sekta binafsi katika sekta ya elimu na ndiyo maana mwaka jana katika mapendekezo waliyotuletea sekta binafsi tuliondoa tozo nne kwa sekta binafsi katika elimu. Hii ni dhamira ya dhati ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tumekumbwa na tatizo moja kwamba huwa tunaweza kuongelea zaidi matumizi bila kujiuliza mapato yanapatikana wapi. Hili tukiweza kulielewa vizuri kwamba tuondokane sasa na matumizi tuanze kufikiria mapato, mapato yetu yanatoka wapi. Tunaposema tuondoe hiki na kile na sheria na kanuni zetu zimeweka wazi unapopendekeza ondoa kodi hii lete mbadala basi tulete kodi ipi ili iweze kufidia yale mapato ambayo yameondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikari ya Awamu ya Tano ni njema kabisa, tulianza na tunaendelea kutekeleza. Tayari task force ipo kazini, juzi tulikuwa think tank meeting kwa ajili ya kupitia maombi mbalimbali yaliyoletwa na wadau wetu mbalimbali ya kikodi na ushuru mbalimbali, tunaendelea kuyafanyia kazi. Nakiri tumepata maombi pia kutoka kwa ndugu zetu hawa wa sekta binafsi kwenye elimu na sisi tunaendelea kufanyia kazi lazima tushirikiane kwa pamoja kuona maendeleo ya Taifa letu yanapelekwa vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kulisemea kwa uchache kwa siku ya leo ni hili pia ambalo linabezwa ndani ya Bunge lako tukufu kwamba Serikali haiwathamini na haiwajali walimu, siyo sahihi na nasema hili kwa sababu moja tu. Baada ya kuingia madarakani tulikuwa na tatizo kubwa la watumishi hewa, tumefanya kazi vizuri wameweza kuondoka watumishi hewa. Tumefanya uhakiki wa madai ambayo watumishi wote walikuwa wanadai tumemaliza na sisi sote Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi mwezi wa pili Serikali yetu imelipa madai ya shilingi 43,005,747,874 na tumelipa deni hili kwa watumishi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tusikilizane tuelewe nini Serikali inafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shilingi bilioni 43 tulizolipa zilikuwa ni kwa ajili ya watumishi 27,118. Kati ya watumishi hao walimu walikuwa 15,593. Kwa hiyo, tuiangalie hii ratio kabla ya kutafuta cheap popularity kwamba Serikali haiwajali walimu si sahihi hata kidogo. Lazima twende kwa takwimu tuieleze vizuri tuweze kujua nini Serikali ya Awamu ya Tano inafanya. Niwaambie walimu tuko pamoja na ndiyo maana Serikali imeongeza kufikia shilingi bilioni 23 kwa sababu tunakwenda kuwalipa walimu pesa yao ya madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana walimu wetu waendelee kuchapa kazi Serikali ya Magufuli ya viwanda, tunatambua mchango wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.