Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, nianze kwa kuunga mkono hoja iliyopo mezani, sambamba na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri ya kuendeleza sekta ya elimu nchini na hili linathibitishwa na masuala yafuatayo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni masuala ya elimu bure kwa watoto kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga karibu shilingi bilioni 263.6 kwa ajili ya kuhudumia elimu ya watoto wa Kitanzania, ni budi kuipongeza Serikali kwa hatua hii kwani ni Serikali chache duniani zinatoa au kupatia wananchi wake elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ni kubwa ambalo Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kwenye sekta hii ya elimu ni pamoja na mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini. Kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga karibia 483 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, hili ni jambo la kuungwa mkono maana karibia wanafunzi laki moja wamekuwa wakinufaika na mikopo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya pongezi hizo, pia nijikite kwenye changamoto zinazoikabili sekta hii ya elimu nchini nazo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utitiri wa nyaraka zinazokinzana katika kusimamia elimu ya msingi, sambamba na Sheria ya Elimu kutokukidhi mahitaji ya wakati uliopo. Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 (Na. 25) imepitwa na wakati, haiendani na mahitaji ya sasa na hili lilijitokeza baada ya mabadiliko ya Sera ya Elimu mwaka 2014. Aidha, kumekuwa na utitiri wa nyaraka unaotumika kusimamia utoaji wa elimu nchini ambazo kimsingi kwa sehemu kubwa zinakinzana. Ninapenda kuishauri Serikali ione umuhimu wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, ifanyiwe marekebisho ya haraka ili iweze kuendana na Sera mpya ya Elimu ili iweze kuendana na wakati uliopo au mahitaji ya sasa. Pia Serikali iangalie namna ya kuifanyia marekebisho kupitia upya nyaraka na miongozo inayokinzana na kufanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya wakati uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili ni mfumo wa ufundishaji wetu hasa kwa masomo ya kiingereza na kiswahili kwa shule zetu za awali hadi msingi hususani darasa la pili. Tafiti za kisayansi zinaonesha ufundishwaji wa lugha kwa binadamu huweza kujifunza vizuri na kwa urahisi lugha yoyote akiwa katika umri mdogo. Hivyo ni vema misingi ya ufundishaji wa lugha ikajengwa kimfumo ili kuwawezesha watoto kumudu lugha hizo kuanzia madarasa ya awali. Wakati sera inatambua kiswahili na kiingereza kuwa ni lugha rasmi zinazotumika katika ngazi mbalimbali za elimu nchini, bado ufundishaji wake haujajengwa kimkakati kuanzia elimu ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilivyo sasa kwenye mfumo wa ufundishaji wanafunzi wanaosoma shule zinazotumia kiswahili kama lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya awali, hawasomi somo la kiingereza hadi wafike darasa la tatu na kwa wale wanaosoma shule zinazotumia kiingereza kama lugha ya kufundishia, hawatakiwi kusoma kiswahili hadi wafike darasa la tatu ingawaje wote wanatarajiwa kufanya mitihani inayofanana kwa masomo hayo wafikapo darasa la nne.

Mheshimiwa Mwneyekiti, jambo hili kama litaachwa liendelee litakuwa na madhara makubwa kwa vijana wetu maana makundi yote wanakosa umahiri wa lugha nyingine kwa kukosa misingi yake kuanzia hatua za awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika changamoto hii ya mfumo wa ufundishaji katika lugha, ninapenda kuishauri Serikali iangalie upya juu ya suala hili hususani masomo ya lugha ya kiingereza na kiswahili, yafundishwe sambamba kuanzia elimu ya awali ili kuwajengea msingi unaofanana na mzuri vijana wetu na hivyo waweze kumudu vema masomo yao katika ngazi ya sekondari na elimu ya juu. Ni vema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iongeze uwekezaji hasa katika ufundishaji fasaha wa somo la kiingereza ambalo ndilo linalotumika kuanzia elimu ya sekondari kwa shule zote hadi elimu ya juu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mihula na siku za masomo kwa shule za awali, msingi na sekondari nchini inayochochewa na changamoto kubwa ya usafiri nchini hasa kwa watoto wadogo wa shule za awali na msingi huhitaji kusoma kwa muda mfupi na kupumzika. Hivyo, nashauri Serikali iruhusu utaratibu wa kuwa na mihula mitatu kwa shule za msingi, awali na sekondari nchini kama inavyofanywa na nchi nyingi za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.