Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kwa siku ya leo. Alhamdulillah.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwashukuru Mawaziri wote wa Wizara hii Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako na Naibu wake Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi nzuri wanazofanya kuhakikisha elimu yetu inasonga mbele. Naomba nichangie Wizara hii kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Mitihani; nitoe pongezi nyingi kwa kazi nzuri zinazofanywa na Baraza hili hususani ya kuandaa mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya walimu. Pamoja na kazi nzuri lakini napenda nitoe ushauri hasa kwenye utungaji wa mitihani wa kumaliza elimu ya msingi (standard vii). Kwa muda mrefu mtihani huu umekuwa ukitungwa kwa kutumia aina moja ya maswali (multiple choice questions) kutoa swali la kwanza hadi 50 pasipo kutunga aina nyingine ya maswali hasa yale yenye kupima stadi nyingine kama kuandika. Hivyo nashauri Baraza litunge mtihani kwa kuchanganya aina nyingine ya maswali ili tuwapime wanafunzi wetu hasa kwenye kuandika na kushirikisha ubongo wao. Pia nashauri mtihani wa hisabati usitungwe kwa multiple choice ili kuwafanya wanafunzi wakokotoe wenyewe pasipokupewa msaada wa majibu ya kuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu lugha ya kufundishia, wanafunzi wetu wengi wanafeli mitihani kwa kushindwa kujua lugha ya kufundishia hususani kiingereza pale wanapokwenda sekondari, hivyo naiomba Serikali kusisitiza lugha ya kiingereza ianze kufundishwa vizuri na walimu mahiri tangu elimu ya awali kwani ndiyo lugha atakayoitumia sekondari hadi chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bodi ya Taaluma ya Ualimu, ni ukweli usiopingika kuwa walimu wetu wengi waliingia kwenye kazi ya ualimu kama kazi mbadala baada ya kazi za career zao kukwama hivyo kufundisha pasipo weledi na kwa ubora unaotakiwa hali inayopelekea kuzalisha wanafunzi wabovu. Hivyo naiomba Serikali kuanzisha Bodi ya Taaluma ya Walimu ili kuweza kuhakikisha elimu yetu inatolewa kwa ubora unaotakiwa na pia inatolewa na walimu bora na siyo bora walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), niipongeze Wizara kupitia Bodi ya Mikopo kwa kuwawezesha wanafunzi maskini kupata mikopo ya kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kusoma elimu ya chuo kikuu. Lakini bodi hii imekuwa ni mwiba kwa wale wanufaika pale wanapoanza kurejesha mikopo hiyo kwani baada ya mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2016 ambapo makato yalibadilika toka asilimia nane hadi asilimia 15 pasipokumuangalia mwalimu anakabiliwa na makato mengi kama kodi, NHIF, PSPF na CWT hali inayopelekea mshahara kuwa chini ya 1/3. Niishauri Serikali kuwapunguzia mzigo wa makato walimu hawa kwa kuacha asilimia nane kwa wale walionufaika kabla ya mwaka 2016 na wale wanufaika baada ya sheria ya mwaka 2016 ndiyo waendelee na asilimia 15 kwani sheria siyo maandika ya Biblia au Qurani hivyo inaweza kuletwa Bungeni na kujadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule binafsi, hawa ni wadau muhimu sana katika kuisaidia Serikali kutoa elimu kwa wananchi. Lakini shule hizi zinapambana na changamoto nyingi sana katika uendeshaji hasa changamoto ya kodi na tozo mbalimbali, lakini pia gharama za ukaguzi za kudhibiti ubora. Hivyo, naomba Serikali yetu Tukufu izipunguzie kodi hizo ili zijiendeshe vema. Pia ningeomba Serikali iwe na utaratibu wa kuongea na wamiliki wa shule hizi juu ya changamoto mbalimbali na namna pia ya kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukaririsha wanafunzi. Napenda niishauri Wizara kwenye suala la kukaririsha wanafunzi hasa pale inapobainika wamefeli mitihani au hawajui kusoma wala kuandika warudie tu. Pia kwenye shule binafsi ambazo imeonekana suala la kukaririsha ni mwiba kwao wapewe masharti kuwa kama wanafunzi ameshindwa kufikisha alama zinazotakiwa basi aruhusiwe kukariri ila kwa sharti la kutolipa ada upya kama kweli wanataka ku-improve quality na siyo academic business.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuwasilisha.