Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rukia Ahmed Kassim

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza Profesa Ndalichako kwa kufanya juhudi ya kuwafanya watoto wetu waweze kuwa na ufaulu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kusema kwamba watoto wetu wengi wanakwenda masafa marefu kufuata shule. Shule nyingi ziko mbali sana na makazi ya watoto, hivyo basi, naishauri Serikali iweke sehemu ambazo wazee watalipia ili watoto waweze kukaa pamoja na kuweza kubadilishana mawazo na kusoma kwa pamoja kwa wale ambao watakuwa na uwezo wa kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwa wale wanafunzi ambao wanaonekana wana uwezo mzuri wawekwe pamoja kuanzia shule za msingi. Ikiwa wataanza kuwekwa pamoja kukawa na madarasa maalum na baadae wawe na madarasa maalum sekondari basi tutapata wanafunzi wazuri wa sayansi na masomo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia tatizo sugu la maslahi ya walimu. Walimu wanaishi katika mazingira magumu sana nashauri waboreshewe maslahi yao. Bila ya mwalimu kupata utulivu basi hawezi kuwa na moyo wa kufundisha vizuri, anakuwa na mawazo mengi sana hajui atalala wapi, atakula nini na huku ana familia inamtegemea. Naiomba Serikali ijitahidi sana kuboresha maslahi haya ya walimu ili watoto wetu waweze kufundishwa kwa utulivu na waweze kupata ufaulu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu vyoo katika shule zetu. Watoto wa kike wanapata shida sana wanapokuwa kwenye hedhi wanashindwa kuhudhuria masomo. Hivyo basi, naishauri Serikali ihakikishe katika shule zetu kuna matundu ya vyoo pamoja na maji.