Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mungu kwa kutupa afya, nawashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kutoa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Naibu Waziri na timu nzima, kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kwa hiyo nafahamu kwa kina nini kinaendelea. Anafanya kazi nzuri ingawa ni wazi lazima tupate maeneo ya kusema ili kufanya kazi iwe nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na pongezi. Pongezi ya kwanza ni kuhusiana na ujenzi wa nyumba za walimu. Biharamulo kwenye shule zenye mazingira magumu nimepata shule mbili, Shule ya Sekondari Katahoka ujenzi unaendelea, Shule ya Sekondari Nemba tumepata mgao lakini naona kuna kuchelewa kidogo, naomba tufuatilie ili tuende kwa kasi. Lakini naomba tuzitazame shule nyingine mbili moja ni Nyakahura Sekondari mpakani kabisa kule na Ngara na Karenge Sekondari hali yake ni mbaya sana. Tunashukuru kwa tulichopata, lakini tunaomba tuzitazame hizo mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, napenda kupongeza suala moja ambalo ni la Kitaifa, hili la Bodi ya Mikopo. Ukiangalia takwimu zinaonesha kabisa mwaka 2015/2016 mwaka ambao Serikali ya sasa iliukuta tayari umeanza, urejeshaji wa mikopo ulikuwa shilingi bilioni 32, lakini 2016/2017 tukaenda shilingi bilioni 116; 2017/2018 tumekwenda shilingi bilioni 130. Ni kazi nzuri kwa kweli, inaonesha kabisa namna gani tunafanya kazi nzuri kwa upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba naomba tutafute namna ya kimkakati zaidi ya kuweza kuboresha zaidi kwenye eneo hili kwa sababu tumeshaonesha tunaweza. Nadhani inawezekana kabisa tukaondoka kwenye Bodi ya Mikopo tukaibadilisha ikawa Higher Education Loan Fund ili ubunifu ukae vizuri zaidi na mianya ya kutapakaa na kuwa na mambo mengine ya kufanya zaidi kuweza kusimama yenyewe iweze kuwa mingi zaidi na wawe na ile autonomy ya kutosha zaidi watafanya kazi vizuri. Hili ni eneo ambalo kwa kweli napongeza lakini tutafute namna ya kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie habari ya ubora wa elimu nikihusianisha na hii habari ya shule za Serikali na shule za binafsi. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbatia, ameisema vizuri sana leo muda mfupi uliopita, kwamba jamani hizi shule zote ni za kwetu na zote zina mchango wa kutosha kwenye kutoa elimu ya nchi hii kwa watoto wetu. Kwa hiyo, tuna wajibu wa kuwasikiliza na kuwasaidia lakini pia tuna wajibu wa kuwasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na upande wa kuwasikiliza. Ilitokea mjadala mwaka jana nakumbuka na wote mnaukumbuka wa habari ya shule za private hizi, wanatoa mitihani mtoto anapotaka kutoka kidato kimoja kwenda kingine, mitihani ndani ya shule na wanaitumia kama kigezo cha kumwambia asiendelee ama arudie. Ni wazi nakubaliana na msimamo wa Serikali, kwamba tukilifanya jambo hili kiholela itakuwa ni hatari, kwamba haujui, huwezi kupima kwamba shule “X” imetumia kipimo gani na shule “Y” imetumia kipimo gani, ni vizuri tukawa na kipimo kimoja ili tuweze kujua nani anafanya nini na kwa manufaa yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili, naiomba Wizara pia kuacha bila kupima nayo ni hatari, tutafute namna ambayo kila mtu asipime kiholela, lakini tuwe na namna ambayo tunawapima hawa watoto wajue kwamba nisipofanya bidii nitashindwa kutoka kidato cha kwanza kwenda cha pili na ule umri mnafahamu ni umri ambao bado wako kwenye hali ambayo wengine hawajielewi, kama hatuna namna ya kupima tunawaacha kiholela, matokeo yake ndiyo tunapata matokeo mabovu sana huko mbele, kwa hiyo naomba hilo Serikali tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili ni upande wa kuwasimamia. Mimi nina mawili, mtanisamehe wenzangu ambao kwa bahati nzuri ama mbaya ni wamiliki wa shule, nalisema hili kwa nia njema tu. Kuna hili suala la shule inachagua watoto kwenda kidato cha kwanza kutoka darasa la saba “A” zote ili matokeo ya kidato cha nne yakitoka ionekane yeye alifaulu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijawahi kuona hospitali ambayo Mheshimiwa Waziri naona hanisikilizi, sijawahi kuona hospitali ambayo mtu akienda daktari anaangalia anasema wewe ninavyokuona unachechemea naomba hapa usije kabisa unaweza ukafia hapa! Ni kazi ya hospitali kwenda kuchukua mtu hata aliye hoi kwa sababu ni kazi yako kutibu.

Sasa kazi ya shule ni kufundisha watu, naomba tuwe na utaratibu ambapo katika watoto mia unaotaka kuchukua wewe shule ya private, chukua 30 cream, chukua 30 wa kati, chukua 40 siyo waliofeli kabisa lakini ile ngazi inayofuata, waliofeli kabisa tuwaache, lakini tuwe na namna tuchanganye ili hata ukija kusema umefaulu tunajua ulifanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tunakupa wenye “A” zote halafu unakuja unasema mimi nimekuwa wa kwanza, tutafute utaratibu, tuchanganye ili tupime kwa usawa na kila mmoja apate fursa ya kufundishwa. Vinginevyo na hospitali nazo ukienda unachechemea zaidi unaambiwa wewe usiingie bwana utatufia hapa ni kazi yao kukutibu, wakishindwa watakupeleka mahali ambapo kuna ujuzi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kusimamia kwenye hizi shule za private ni habari ya likizo. Mtoto humuoni mwaka mzima wanasema mwezi wa sita hawaji, mwezi wa 12 hawaji, haiwezekani, hata kuja kusalimia wazazi ni sehemu ya shule. Hebu angalia shule za Seminari za Katoliki, wale ukikutwa unasoma saa ya michezo unafukuzwa kwa sababu unafundishwa kutumia muda wako wa kusoma vizuri ili muda wa kula uutumie vizuri, muda wa kucheza uutumie vizuri, lakini ndiyo wanaongoza kufaulu kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna shule yaani mtoto haonekani mwaka mzima wanasema wana masomo maalum! kuja nyumbani kuzungumza na wazazi ni sehemu ya shule, tunaomba usimamie Mheshimiwa Waziri, hizi shule zote ni za kwetu, tusimamie wasome, saa ya kucheza wacheze, saa ya kula wale, saa ya kusoma wasome, likizo waje nyumbani, ni sehemu ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea pia ukurasa wa 112, ameongelea Chuo cha Mkwawa, kuna shilingi bilioni mbili pale inapelekwa kwa ajili ya maabara ya kompyuta na vitu kama hivyo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kama nilivyosema, nimeshuhudia mwaka huu tumekwenda Mkwawa pale. Serikali imepeleka pesa pale ya kujenga ukumbi wa mikutano lakini mambo yanayoendelea ni maajabu ni ubadhirifu mtupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tubadilishe namna ya kusimamia pesa hizi. Tutakuwa tunafurahi hapa kwamba imekwenda bilioni mbili lakini kama usimamizi haukai vizuri mwisho wa stori ni kutumbua watu kutafuta nani ameiba ambayo haitusaidii, tutafute namna ya kusimamia kabla hazijaibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.