Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hamadi Salim Maalim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala, kwa kunijalia uwezo huu wa kusimama hapa kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Baada ya shukrani hiyo, pia nikushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze moja kwa moja kwenye vyuo vikuu. Kwenye nchi yetu kuna vyuo vikuu mbalimbali na kwenye vyuo vikuu hivi kuna wanafunzi ambao wanalipiwa na Bodi ya Mikopo, lakini pia kuna wanafunzi ambao hawakupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo wanagharamiwa na familia zao, familia za kimaskini na kinyonge. Leo kuna baadhi ya vyuo vikuu baada ya kumalizika mwaka wanabadilisha malipo yaani malipo yanaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelewa kwa ambavyo nilisoma mimi katika vyuo vikuu, mkataba ule unapobadilika kwa yule ambaye anaendelea mwaka mwingine unakuwa haumuathiri lakini kilichotokezea kwa baadhi ya vyuo vikuu ni kwamba wanapobadilisha mkataba mwanafunzi aliyepo mwaka wa pili na wa tatu pia mkataba ule unamuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, juzi nilikutana na wanafunzi wa Zanzibar University, kuna wanafunzi wanafanya degree ya nursing na walikuwa wanalipia kwa mwaka shilingi 2,197,000 kwa wale walioanza mwaka jana lakini mabadiliko yalipotokea mwaka huu uliopita wamepandishiwa kutoka shilingi 2,197,000 mpaka shilingi 2,486,000. Tumuangalie mwanafunzi huyu ambaye analipiwa na familia ya kinyonge, ataelekea wapi mzazi keshajipangia kwamba hana uwezo wa kuongeza shilingi 400,000 kwa mwaka za kumsaidia mtoto wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi wa diploma ambaye alikuwa analipa shilingi 1,500,000 sasa anatakiwa alipe shilingi 1,900,000, athari hii ilitakiwa imuangalie yule ambaye anaanza sasa. Naomba Waziri atakapokuja kujumuisha atupe maelezo, vyuo kama hivi ambavyo vinapandisha tuition fee katika hali ambayo si ya kiutaratibu wanavichukulia hatua gani? Kwa sababu wanafunzi hawa tayari walishaanza na mkopo ambao unakubalika lakini wanapandishiwa mkopo ule katikati ya masomo, hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala zima la upungufu wa walimu. Tunasema kwamba hakuna elimu bila ya walimu, kama hatuna walimu na elimu inakuwa haipo. Upungufu wa elimu uliopo katika nchi yetu ni mkubwa sana. Tukichukua data ya mwaka 2016/2017 na suala hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililisema katika bajeti ya mwaka 2016 na ya 2017 na mara hii tunalizungumza tena kwamba upungufu wa walimu ni mkubwa sana. Kwa mfano, katika bajeti ya 2016/2017 kwa shule za msingi kulikuwa na upungufu kutoka walimu 191,772 mpaka kufikia walimu 179,291 ambapo hii ni sawa na asilimia 6.5. Ushukaji huu mkubwa wa idadi ya walimu umesababisha uwiano wa mwalimu mmoja kuweza kufundisha wanafunzi zaidi ya 50 mpaka kufikia 70. Tuangalie, hapa tutapata elimu bora au tutapata bora elimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waziri atakapokuja atueleze ni mkakati gani wameuandaa kwa sababu toka 2016 mpaka leo hakuna ajira ya walimu iliyofanywa. Hali kadhalika kuna walimu ambao wanastaafu katika kipindi chote hicho, kwa hiyo, ina maana kwamba bado idadi hii niliyoisema hapa inawezekana ikawa ni kubwa zaidi kufikia leo kwa sababu hii ni idadi ambayo ilikuwa imeoneshwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika shule za awali hali kadhalika upungufu nao ni mkubwa. Katika shule za awali alitakiwa ratio iwe ni 1:25 lakini ratio hiyo inakuwa ni 1:150. Hebu tuangalie, wanafunzi hawa wanaoanza sasa tunawasomeshaje wanafunzi 150 kwa mwalimu mmoja, matokeo yake yatakuwa ni yapi? Mtoto anatoka shule ya awali anarudi nyumbani, ukimuuliza umefundishwa nini anakwambia kwamba nimefundishwa kukata (kuvuka) barabara. Hivi kweli ufanisi utakuwepo jamani? Mkakati unahitajika, Waziri atueleze ni mkakati gani pia wameuandaa katika kutatua suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la maslahi ya walimu, madeni pamoja na kupandishwa madaraja. Jamani ni kitu cha aibu, tulisema kwamba tunafanya uhakiki ukikamilika tutapandisha walimu madaraja na tutalipa madeni. Kuna walimu tokea siku waliyopewa barua za kulipwa madeni yao ni mwaka mzima sasa hivi Halmashauri zimeshindwa kuwalipa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)