Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia kilimo huwezi kukosa kuzungumzia ukosefu wa ardhi ya kilimo kwa baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wafugaji na hifadhi za Serikali, wakulima na hifadhi. Mfano mzuri upo mgogoro kati ya wakulima na Hifadhi ya Akiba ya Uwanda katika Jimbo langu la Kwela. Mwingine ni mgogoro wa wananchi na mwekezaji wa shamba la Malonje. Serikali imalize haraka migogoro hii bila kufanya hivyo inaweza kusababisha mapigano na kuleta maafa makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kwenye pembejeo. Pembejeo nyingi hazifiki kwa wakati, hazitoshelezi, wanaofaidika ni wachache na bei kuwa kubwa isiyolingana na bei ya mazao. Naomba Serikali iangalie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchi yetu haiwezi kuwa na uchumi imara. Tunayo mito mingi inayotiririsha maji msimu wote, lakini bado hatujaitumia vizuri. Nichukulie mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, miaka minne mfululizo tuliomba miradi ya umwagiliaji lakini hatujapata fedha za kujenga miradi hiyo. Miradi hiyo ni wa Msia, Uzia, Maleza, Nkwilo, Nankanga na Mbulu. Naomba Serikali itupatie fedha kwa ajili ya miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunalo tatizo kubwa la wakulima wetu kukosa soko la mazao na kuwafanya kukata tamaa na vijana wengi kukimbilia mijini baada ya kuona kilimo hakiwalipi. Hivyo, Serikali itafute masoko ya bei nzuri ya mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa maghala. Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi lakini hakuna maghala ya kutosheleza kuhifadhi mazao. Matokeo yake ikifika wakati wa mvua mazao hunyeshewa na kuoza. Naomba Serikali itueleze ni lini Mkoa wa Rukwa utajengewa maghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetelekeza Ziwa Rukwa pamoja na ziwa hilo kutoa ajira kubwa kwa wananchi na hasa vijana. Serikali haijawahi kutoa mikopo ya vikundi vya wavuvi, kwa nini mmelitelekeza Ziwa Rukwa?