Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na nimpongeze kwa hotuba yake nzuri ambayo imeitoa leo, nilikuwa na karatasi karibia nane za kuchangia, lakini nimejikuta kila akitoa hotuba nachana moja baada ya nyingine na sasa nimebakiwa na kipande nusu ambayo nitaitoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa programu yake ya elimu bure, katika hili Mheshimiwa Rais ametusaidia hasa ambao tunatoka majimbo ya vijijini ambayo asilimia kubwa wazazi ni wakulima. Kuna changamoto chache fedha hii imekuwa ni kidogo sasa hivi utakuta katika shule zetu za kule vijijini walimu yale mazoezi ya kila Jumamosi wanaandika ubaoni. Kwa hiyo, naomba waongeze pesa ili walimu waweze kwenda kisasa na kuwapunguzia mzigo wa kuandika ubaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine sasa hivi Serikali ambacho inatakiwa tu kuifanya ni kuwafanya walimu waifurahie ile kazi kama kazi zingine wasiichukulie kama tunavyowachukulia, wawajengee nyumba, wawapandishe madaraja kwa muda, maana yake kumekuwa na changamoto kuna walimu wanafundisha hadi miaka 12 hawajapanda daraja hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hili linahusu upande wa TAMISEMI kidogo, lakini naomba mshirikiane na Wizara. Hawa Walimu ambao wametolewa sekondari kupelekwa shule za msingi kuna sintofahamu, kuna walimu ambao wana diploma wameachwa sekondari, wamechukua walimu wenye degree wamewapeleka shule za msingi hili ni tatizo kwa sababu mliwaachia Walimu Wakuu na Maafisa Elimu walisimamie wenyewe matokeo yake wamefanya ndivyo sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ukaguzi ameliongelea Mheshimiwa Maghembe; Wakaguzi wengi hawa hata vyombo vya usafiri. Sasa kwa ambao tunatoka majimbo ya vijijini inawawia vigumu kwenda kukagua hizo shule matokeo yake wamekuwa wakikagua makaratasi na ndiyo maana ufaulu unashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea suala la vitabu wiki iliyopita kwa kweli hili ni tatizo, tuna shule zaidi ya 170,000 vitabu vya darasa la nne ambao wanatakiwa wafanye mtihani mwezi wa Novemba mpaka leo hii havijatoka. Hebu niambie, kuvisambaza hivi vitabu Serikali yetu ninavyoifahamu na ukosefu wa magari katika Wilaya zetu huko kwenye sekta ya elimu vinaweza vikachukua zaidi ya mwaka mmoja. Kwa hiyo, wananfunzi wa darasa la nne mwaka huu ninauhakika watafanya mitihani wakiwa hawajapata vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kukariri madarasa, hii iko kwenye secondary schools. Wizara tulitoa maoni, Kamati wametoa maoni na Wabunge tunaomba kusisitizia, endapo tutaruhusu wanafunzi waende ili mradi waende baada ya miaka mitano tutazalisha kizazi cha wanafunzi ambao hamna kitu. Kwa sababu huwezi ukampeleka mwanafunzi kidato cha pili kama hakuelewa kidato cha kwanza na hawezi akafanya chochote kidato cha pili kama hajafanya kidato cha kwanza.

Kwa hiyo, mngeliachia kwa shule za private wao wana utaratibu mzuri wafanye kwa ajili kuzalisha matokeo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nichangie kwenye upande wa Loans Board. Niipongeze Serikali kwa kuongeza fedha za loans board, lakini limetokea tatizo sasa hivi hakuna kigezo maalum cha kusababisha wanafunzi wapate mikopo. Kwa mfano, mwenyewe nina ushahidi, kuna Taasisi moja ya Solida Made ambayo ilikuwa inasomesha wanafunzi, inawasaidia kutoka shule za sekondari mpaka Chuko Kikuu. Mwaka huu walikuwa na wanafunzi zaidi ya 400, walikubali kuwalipia ada za Chuo Kikuu wale wanafunzi ambao hawana uwezo, ambao waliwasaidia tangu shule za msingi, lakini walivyofika Chuo Kikuu Serikali ikagoma kuwapa mkopo ikasema hawana utaratibu huo. Zile taasisi walichotaka ni Serikali iwagharamikie fedha za chakula, lakini ada watawalipia wenyewe, Serikali ikakataa. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu anaweza akanitolea ushahidi nilifika ofisini kwake, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo nilifika ofisini kwake, lakini wamekataa kuwapa wanafunzi hawa mikopo. Taasisi imetusaidia kuwalipia ada, lakini ninyi mmekataa kutoa fedha za chakula, kwa hiyo hili ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niliongea wiki iliyopita Waziri alisema hakunielewa vizuri na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi. Kumekuwa na tatizo ya Vyuo Vikuu, wanafunzi wetu wa kike wanapata shida mno. Katika vyuo vyetu vikuu kuna walimu ambao wanajulikana kabisa kuwa hawa Walimu ni madume ya mbegu, wanafelisha wanafunzi wa kike, wanataka wawape rushwa za mapenzi ndiyo wawafaulishe. Mheshimiwa Waziri nitashirikiana na wewe kama utanipa ushirikiano, nitakuletea majina ya walimu wa Vyuo Vikuu vyote Tanzania ambao ni madume ya mbegu kazi yao ni kufelisha wanafunzi na kutaka rushwa za ngono. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara chini kitengo chake cha P4R kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule za sekondari. Kwanza niwapongeze katika kujenga shule mpya na nyumba za Walimu. Mimi mwenyewe binafsi nimepata shilingi milioni zaidi ya 500 kwa ajili ya kukarabati shule yangu moja ila ninachoomba hii fedha ya P4R iende moja kwa moja kwenye Halmashauri lakini wasitumie Wakandarasi, kwa sababu tumeshuhudia wakitumia Wakandarasi fedha inakwenda nyingi lakini inafanya kazi kidogo lakini mkitumia Force Account ile fedha kidogo inafanyakazi kubwa. Naomba mtoe maelekezo hii fedha mtumie force account

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kushuka kwa ufaulu. Muda wangu bado.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia zaidi ya asilimia 60 wanapata division four na division zero, naomba mtumie nguvu kubwa katika kuwekeza katika vyuo vya ufundi hii miaka minne ambayo mwanafunzi anasoma kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne tungewekeza kwenye ufundi angeweza ku-achieve kitu kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka niiase Serikali yangu. Serikali yangu tumeichukulia shule za private kama adui, yaani tunavyoichukulia CHADEMA na CCM na ndiyo Serikali na shule za private. Imekuwa kumiliki shule ya private ni sawa na kupita na mihadarati katika kituo cha Polisi.

Naomba niwatoe hofu Serikali, mitaala mnatunga ninyi, mitihani mnatunga ninyi, tarehe ya kufanya mitihani mnaweka ninyi, kusimamia mnasimamia ninyi, mitihani mnasahihisha ninyi, matokeo mnatangaza ninyi, hofu yenu ni nini na shule za private? Fanyeni vizuri hizi shule za private zitakufa zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulinda muda, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie maoni ya Kamati, hotuba yake ni nzuri sana, tangu nimfahamu Waziri hotuba hii ni ya kwanza, good! Endelea hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.