Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kipekee nianze kwa kumshukuru Mungu, muweza wa yote aliniwezesha kusimama na kutoa mchango katika hoja hii muhimu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kuandaa taarifa nzuri na kuiwasilisha vizuri. Kipekee, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri na timu yake yote; IGP Kamanda Sirro, Kamanda wa Magereza, Kamanda wa Uhamiaji na Kamanda wa Zimamoto kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha nchi ya Tanzania tunaendelea kuishi kwa amani na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashuhudia kwamba Mamlaka hii ya Mambo ya Ndani wameweza kudhibiti mauaji ya Albino. Ni ukweli usiopingika, wamedhibiti wezi wakiwemo na wezi wa magari; ni ukweli usiofichika, wamedhibiti mpaka na wezi wa mabenki; ni ukweli usiofichika, wamedhibiti mauaji ya raia wasiokuwa na hatia; Albino, vikongwe, Askari wetu waliokuwa mstari wa mbele na hata wananchi wa Kibiti ambao walikuwa wanauawa kama kuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni, haki yake apewe. Hongera sana Kamanda Sirro, hongera sana Makamanda wote. Nataka niwaambie, akutukanaye hakuchagulii tusi; na ukiwa kwenye maji unaoga, akija mwendawazimu usimfukuze, chutama kwenye maji. Atakayewalipa ni Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu, unaona mpaka watu wanatembea, wanaongea na wanazungumza watakavyo ni kwa sababu ya amani. Watu wamekula, wameshiba, wanalala kwa amani mpaka sasa wanavimbiwa wanatukana ovyo. Kamanda Sirro na timu yake wasikate tamaa. Mti mzuri wa maembe ndiyo unaopigwa mawe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wanawake wa Tanzania ambao tumeachwa wajane kule Kibiti, ambao wameachwa wajane kule Rufiji, Albino wasiokuwa na hatia ambao wameachwa wajane au wameachwa yatima, sisi tunawaombea dua kwa Mwenyezi Mungu na ndiye atakayewalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiona watu wanapiga kelele, wajea wamewashika pabaya. Maana wamedhibiti kila kona. Madawa ya kulevya, waliokuwa wanafanya wengine wako hapa wengine wako nje, wamedhibiti. Mikutano isiyokuwa na tija, watu walikuwa muda wote maandamano, wamedhibiti, hongereni. Ndiyo maana leo unaona sasa kila anayesimama, wanawapiga kwa sababu wamewashika pabaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwatia moyo. Wasivunjike moyo, wasonge mbele, tunatambua kazi yao na Watanzania wanatambua kazi yao na ndiyo maana wanawaombea dua kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, Jeshi la Polisi limedhibiti ajali za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Jeshi la Polisi limedhibiti ajali za barabarani. Nani ambaye hajui kwamba kwa miaka ya hivi karibuni kulikuwa na ajali za kupitiliza? Kuna watoto wamebaki yatima, kuna wamama wamebaki wajane; kuna familia zimeondoka zote kwa sababu ya mwendokasi. Nani alikuwa hajui?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi wamedhibiti, wameweka mwendo wa taratibu, ajali zimepungua kwa kiwango cha asilimia 35. Nawapongeza, waendelee kuchapa kazi na wakaze buti. Wakiona tunapiga kelele wametushika pabaya, tukiwemo na sisi Wabunge tulikuwa ni miongoni mwa watu tuliokuwa tunakwenda mwendo kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeshamtangazia dereva wangu, tukikamatwa hiyo kesi ni ya kwako. Endeleeni kudhibiti ili kuokoa Watanzania wanaofariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa sababu wamedhibiti wahamiaji haramu. Nchi yetu ilikuwa inaelekea kubaya kwa sababu Tanzania ni barabara. Nampongeza Kamishna wa Uhamiaji, Mama Anna, kwa kazi nzuri anayoifanya. Wamewadhibiti, wametushika pabaya, kwa sababu baadhi ya wasioitakia mema nchi yetu, walikuwa wanawatumia wahamiaji haramu kuvuruga amani ya nchi yetu. Hongera sana, wapige kazi wala wasiwe na wasiwasi. Sisi tulio wengi tuko nyuma yao na Mwenyezi Mungu atawapa baraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara bada ya utangulizi huo, nimemsikia mtoto wangu Lema akieleza hapa. Mimi nimeita mwanangu, analeta propaganda mwanangu. Hivi watu 1,000 wafariki katika nchi hii ya Tanzania; familia za watu 1,000 zipoteze, watu 1,000, tuendelee kuwa hivi mwanangu! Jamani hebu semeni ukweli, msipotoshe umma. Jamani hata kama tunatafuta kick siyo kwa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani Mheshimiwa Lema aje na ushahidi atuoneshe. Kweli familia 1,000 watu wapotee halafu nchi ibaki kuwa hivi? Jamani, hebu waseme ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya utangulizi huo, nijielekeze kwenye michango yangu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naomba nizungumzie bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Tumeona kwamba kuna fedha zimepelekwa zaidi ya asilimia 78. Ninachokiomba ili Taasisi za Mambo ya Ndani ziweze kutekeleza wajibu wao sawasawa, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama yuko hapa anisikie. Hebu wapeleke fedha kwenye haya Majeshi waweze kununua vipuli kwa ajili ya magari, waweze kupata fedha kwa ajili ya kununua mafuta, waweze kupata fedha kwa ajili ya kulipa madeni. Taasisi zinafanya kazi kwa hali ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi ni sawasawa na hospitali. Shida haina hodi wala nini. Unapotokea uhalifu, Kamanda wa Mkoa hana mafuta, OCD hana mafuta, Mkuu wa Kituo hana mafuta, wote wanakuwa ombaomba. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake na Serikali iko hapa na Waziri Mkuu yuko hapa. Hebu waipe kipaumbele kinachostahili Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Zimamoto. Mfano tu ni Dodoma, wana magari mawili tu, moja liko uwanja wa ndege, moja liko hapa; na hapa ni Makao Makuu. Hivi gari mbili zinatosha kwa Dodoma? Vile vile bajeti ya kwenda kujenga nyumba za Askari hakuna. Naomba hebu Serikali ione Wizara hii ya Mambo ya Ndani ipewe heshima inayostahili ipelekewe fedha kwa ajili ya maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie nyumba za Askari. Naomba niungane na wenzangu kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali, lakini ni ukweli usiopingika, hali siyo nzuri katika nyumba za Askari wetu. Askari wetu wanaishi katika nyumba mbaya. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kujenga nyumba za Askari; na kwa mujibu wa taarifa, zitajengwa nyumba 400. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, Jeshi la Polisi linalo Kitengo cha Ujenzi, Jeshi la Magereza linalo Kitengo cha Ujenzi; hebu imarisheni vitengo hivi. Sasa hivi vile vitengo vimekufa, matokeo yake sasa tunahitaji kutumia fedha nyingi zaidi tofauti na ilivyokuwa zamani. Na-declare interest kabisa, nami ni mtoto wa Askari na ndiyo maana nikiona mtu anamkejeli Askari huwa naingia na uchungu sana kwa sababu Askari ni mtu aliye mstari wa mbele kupambana usalama wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba, waimarishe hiki kitengo wakipatie fedha. Bahati nzuri kinao Watendaji wazuri, kinao mainjinia. Kwa sababu sasa hawana kazi, wengine sasa ndio ma- OCD. Mfano OCD wa Ileje, ni injinia yule lakini leo ni OCD; na watu wengine. Hebu waimarishe hiki kitengo kiweze kujenga kwa gharama nafuu ili kwa kutumia na nguvu ya wale wafungwa, tunaweza kuokoa fedha nyingi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie maslahi ya Askari wetu. Askari wetu wanafanya kazi ngumu sana katika mazingira magumu tena ya hatari. Wanaishi na raia na raia wengine wako humu ndani, wanaona jinsi wanavyozungumza. Hivi akikutana na Askari kwenye kona, itakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Askari hawa tuimarishe ulinzi wao, tuwajengee nyumba za kutosha, tuhakikishe maslahi yao yote wanapata, tuhakikishe wanapokwenda likizo wanapata haki zao, wanapopanda madaraja tunawapa fedha zao. Wapo Askari wamepanda madaraja, hawaongezewi mishahara, mpaka wanastaafu matokeo yake hata pension yao inakuwa ni kidogo. Askari huyu ambaye anatufanyia kazi nzuri, tunamlipa nini? Naomba sana, hebu waangalie kwa macho ya huruma katika jeshi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala zima la upandishaji wa vyeo kwa Askari wetu. Nashukuru sana Serikali hii na majeshi yote yameweka utaratibu. Kuna kanuni ya namna ya kuajiri na namna ya kuwapandisha madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kabisa, hebu angalieni na wale Askari waliofanya kazi kwa muda mrefu. Wamefanya kwa weledi, kwa uaminifu lakini hawana elimu ya juu. Hawa wanasuasua katika kupanda vyetu, utakuta ni Constable tangu ameanza; akisuasua mara amekuwa Corporal, mara amekuwa Seargent mara amekuwa Major kwa muda mrefu sana. Hivi kwa nini hawa wasipewe heshima kama ambavyo wengine wanavyopata? Kwa sababu wamefanya miaka 25, miaka 30 anabaki kuwa Constable. Hebu naomba hii kanuni iangaliwe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la posho za chakula cha Askari. Naishukuru Serikali, angalau wamewaongezea Sh.300,000/=. Namshukuru na Mheshimiwa Rais wetu amewapa Sh.100,000/= kwa ajili ya vinywaji. Askari wanashukuru. Nami nazungumza nao, nashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba, hebu Serikali ijaribu kuona uwezekano hata kuwaongezea tena laki moja moja hata zikawa shilingi laki nne, kwa sababu wanafanya kazi nzuri sana, kazi ambayo ni ya kutukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Askari wetu wanaishi uraiani, kwenye nyumba za kupanga; walikuwa wanalipwa posho asilimia 15 kwa ajili ya kulipa kodi ya nyumba, iliondolewa kwa maelezo kwamba wanahakiki. Nataka nijue, huu uhakiki utakwisha lini? Vile vile Askari wa Zimamoto
hawana nyumba kabisa; Askari wa Uhamiaji hawana nyumba kabisa, wa Magereza ndiyo usiseme, wengi wanaishi uraiani. Hivi hawa hii posho yao ya nyumba asilimia 15 ni lini wataipata? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na mafunzo ya Askari. Naipongeza Serikali inafanya kazi nzuri sana ya kuwajengea uwezo Askari wetu. Ombi langu, naomba sasa wajifunze namna ambavyo hasa wale CID wanaoweza kukabiliana na hii mitandao, kwa sababu sasa hivi wizi ulio mwingi ni wa kwenye mitandao. Hawa Askari wetu CID wanajengewaje uwezo ili waweze kukabiliana na changamoto za sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ambalo nataka nijue, nimepata habari kwamba sasa hivi Askari wanaokwenda kusoma CID, traffic na kozi nyingine wameambiwa sasa wanatakiwa kuchangia kila siku shilingi 7,000/=. Nataka kujua, huo utaratibu umeanza lini? Kwa nini wachangie? Hivi anapoondoka ameiacha familia yake, itakula nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.