Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana. Kabla sijaanza kuchangia nitoe tu ushauri wa jumla, tunapozungumza hapa kwa hisia kali kumkosoa Rais, tunashauriwa sisi Wabunge wa CCM mwambieni Rais awe anakosolewa. Ndugu zangu, hata kwenye familia zetu kuna wakuu wa familia, hivi huwa tunawatukana wale wakuu wa koo zetu? Tukitaka kuzungumza na wale wakuu wa koo zetu au wakuu wa familia zetu, huwa tunawajibu tunawatukana? Tunaongea nao taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu, naomba nishauri kwa nia njema kabisa; Rais ni Rais tu, ni mamlaka ambayo amepewa kwa mujibu wa Katiba, kwa hiyo lazima tumheshimu, lazima tufahamu kwamba waligombea wengi lakini Mungu alimpanga yeye awe Rais wa Tanzania. Kwa hiyo, tunapokuwa tunasimama jazba zetu kidogo tuwe tunazishusha chini halafu tunajua huyu ndiye Rais wetu, tupende tusipende tayari Mungu ameshamtukuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nianze kuchangia. Kwanza nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya katika Wizara hii, lakini pia nimpongeze ndugu yangu IGP kwa kazi nzuri anazofanya, kwenye mazuri hapakosi kasoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizizungumze kasoro, hususani katika Jimbo langu la Kigoma Kusini, Idara ya Polisi, Vote 28, nilikuwa naangalia kwenye Vote hii 28 naona mikoa mingine imetengewa pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za maaskari wa ofisi za ma-OCD, lakini nimwombe sana Mheshimiwa Waziri; amekuja Kigoma ameona hali halisi ya maaskari, niombe sana kwa nini hawatoi upendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Uvinza ni wilaya mpya, ina miaka sita sasa lakini OCD hana nyumba, OCD hana ofisi, hana gari, katika mazingira kama yale anafanyaje kazi? Naomba sana, nimeona wametenga magari lakini hakuna gari hata moja kwenye wilaya, gari ambalo tumepewa Halmashauri ya Uvinza ni gari lililokuwa linatumika kwenye Ofisi ya RPC. Hata hivyo, tunavyoongea leo hii hata pakitokea matukio ya ujambazi OCD lazima aombe gari mkoani ndiyo afanye kazi katika eneo lake la kazi. Niombe sana hebu wajaribu kumwangalia OCD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za maaskari; maaskari wetu wanaishi uraiani, tunawatuma waende wakakamate wahalifu; wanakamata vipi wahalifu wakati wanaishi nao uraiani? Kwa hiyo, kwenye bajeti ijayo wajaribu kuangalia watenge pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za maaskari jamani, wana maisha magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nichangie kuhusu Magereza, tunalo Gereza la Ilagala, gereza hili limechukua maeneo makubwa ya wananchi wa eneo la Ilagala. Mheshimiwa Waziri alikuja tukafanya kikao akatoa maelekezo tuhakiki mipaka ya wananchi na mipaka ya gereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakiki ule umeonesha ni dhahiri kabisa kwamba gereza wamehodhi maeneo ya wananchi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu tufikie mwisho. Wamechukua eneo kubwa karibu ekari 5,000, kwa nini wasitoe hata ekari 2,500 zirudi kwa wananchi na zile 2,500 tuwaachie wao waendeleze na masuala mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwa harakaharaka kwa sababu nataka nisimame sana kwenye Uhamiaji. Katika uhamiaji tuna kero kubwa sana na uhamiaji ndani ya Mkoa wa Kigoma. Katika Tanzania hii sio Kigoma peke yake ambayo inapakana na nchi za jirani, hata Arusha wanapakana na Kenya, ukienda Mtwara wanapakana na Msumbiji, lakini ukienda Kagera wanapakana na Rwanda. Leo wananchi wa Kigoma hatuishi na amani, kutwa kucha tunaitwa Banyamurenge, tunaitwa Wakongo, tunaitwa Warundi, roho zinatuuma sana sisi watu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, roho zinatuuma kwa sababu unaposikia wananchi wanavamiwa saa nane za usiku, hivi tujiulize, saa nane za usiku operesheni za kwenda kuvunja milango kwenda kukamata raia. Nane usiku wote tunafahamu sisi wanawake humu ndani, mwanamke saa nane usiku ndio anatafuta namna ya kujaza nyumba. Leo saa nane usiku watu wanabomolewa milango, inauma, naongea kama mwanamke, inaniuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapigiwa simu Mheshimiwa Mbunge tunavamiwa saa tisa, sasa hawa watu wakiwavamiavamia mwisho jamani wanaume wetu wale watashindwa kusimamisha mambo vizuri. Hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kwa uchungu. Operesheni zinazofanywa ndani ya Mkoa wa Kigoma sio sahihi, ile Kigoma ni Tanzania, wananchi waliopo ndani ya Wilaya za Kigoma ni Watanzania, leo tukisimama hapa tumechaguliwa kwa sababu ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe, najua kwamba Mkurugenzi wa Uhamiaji ni mwanamke, hali ya uhamiaji ndani ya Mkoa wa Kigoma ni mbaya ndugu zangu, lazima ifike mahali tuambiane ukweli. Abiria wa kutoka Mkoa wa Kigoma wanapanda basi saa 11.30 alfajiri, wakifika Uvinza mabasi yanasimamishwa wanateremshwa wote wanaanza kuambiwa wewe shuka tuone uraia wako, mbona maeneo mengine hawafanyi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshalalamika, nimeshaongea mpaka na Mkurugenzi wa Uhamiaji. Kwenye bajeti ya mwaka jana nilimwomba Mkurugenzi wa Uhamiaji pale nje kwamba hali ya operesheni zisizokuwa na ubinadamu hatuzitaki ndani ya Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma ni wa Tanzania, kama tunaongea lugha moja na Warundi isiwe sababu, ule ni Mkoa wa Waha, ni Mkoa wa Wamanyema lakini sio mkoa wa kusema sio wa Tanzania; nimeongea kwa jazba kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, NIDA, zoezi la vitambulisho vya uraia Tanzania linaendelea katika Mkoa wa Kigoma, lakini cha kunisikitisha, wanaambiwa watoe pesa Sh.15,000 ndiyo waweze kuandikishwa. Hivi hili zoezi la nchi nzima mbona hatukusikia watu wanaambiwa watoe hela; kwa nini sisi kule wanaambiwa watoe hela?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna mambo yanayoendelea ndani ya Mkoa wa Kigoma, kama sisi tusipowasemea hawana mtu mwingine wa kuwasemea. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, hebu ajaribu kuwasiliana na idara husika, huu uonevu unaofanyika katika Mkoa wa Kigoma hatuwezi kukubaliana nao; tunajua yeye ni mchapakazi, tunajua ni msikivu na mimi binafsiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.