Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa miongozo yote ambayo amekuwa akinipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Vilevile nichukue nafasi hii kuweza kuwashukuru akinamama wote na wanawake wote wa Mkoa wa Songwe kwa imani yao kubwa kwangu ambayo inaniwezesha katika kutekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nichukue nafasi hii kuweza kuwashukuru Wabunge wote ambao wameweza kuchangia na hoja yetu, nami niseme kwamba, michango yao yote imekuwa ni michango ambayo ina tija sana na tunaahidi kwamba, tutaichukua na kuweza kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu baadhi ya hoja ambazo zimeweza kuzungumzwa, kwanza nianze na kujibu hoja za Kamati. Hoja ya kwanza ambayo imeibuliwa na Kamati ni juu ya usajili wa magazeti kwamba uko chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti yetu ya mwaka 2018/2019, Wizara tumejipanga kuendelea kusajili magazeti yote nchini, lakini vilevile kwa sababu ni takwa la kisheria chini ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 tumepokea ushauri wa Kamati na Wizara tutaendelea kuhakikisha tunaendelea kusajili magazeti ambayo yapo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema pia tukubaliane na Waheshimiwa Wabunge katika jambo hili kwamba, katika suala zima la usajili wa haya magazeti Wizara imefanya kazi kubwa sana kwa sababu ukiangalia ndani ya muda mfupi katika kipindi cha mwaka mmoja magazeti ambayo yamesajiliwa ni magazeti 169 ukilinganisha na magazeti 400 ambayo yamesajiliwa tangu kuanzishwa kwa sheria hii mwaka 1976.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba, jitihada kubwa zinahitajika, lakini pamoja na hayo, Wizara imefanya kazi kubwa sana na tunaahidi kwamba usajili wa magazeti tutaendelea nao katika mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili pia ambayo imeweza kuibuliwa na Kamati ni kuhusiana na Serikali kufanyia kazi andiko la TBC kwamba wanahitaji shilingi bilioni 80 kwa ajili ya kuboresha usikivu wa TBC. Serikali imeendelea kusaidia shirika hili la TBC katika kuboresha usikivu katika nchi yetu ya Tanzania, hilo limejidhihirisha kwa sababu ukiangalia bajeti ya mwaka 2016/2017, fedha ambayo ilitengwa ilikuwa ni shilingi bilioni moja, lakini kwenye bajeti ya mwaka wa 2017/2018, bajeti hiyo ya kuboresha usikivu ilipanda na kuweza kufika shilingi bilioni tatu. Kwenye bajeti hii sasa ambayo tunaomba leo Waheshimiwa Wabunge muweze kuipitisha Shirika la TBC limetengewa shilingi bilioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa kwamba kwa kuwa, Serikali katika fedha ambayo ilitenga mwaka uliopita shilingi bilioni tatu na fedha hiyo imeshatolewa yote, ni imani yetu kabisa kwamba, katika bajeti hii ambayo imetengwa ya shilingi bilioni tano kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, Serikali tunaahidi kwamba hiyo fedha itatoka na kwa namna moja au nyingine itasaidia sana katika kuboresha tatizo la usikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii vilevile iliweza pia kuchangiwa na Mheshimiwa Abdallah Bulembo ambaye alisema kwamba fedha hii ambayo imetengwa ni ndogo sana. Niseme tu kwamba Mheshimiwa Mbunge naomba tukubaliane kwamba Serikali ina nia ya dhati kabisa katika kuboresha usikivu na kulisaidia Shirika la TBC. Wanasema kwamba safari ni hatua, kwa hiyo tumeanza kidogo kidogo na sasa hivi tunaendelea vizuri kuhakikisha kwamba tunamaliza kabisa tatizo la usikivu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imeibuliwa na Kamati ni kutoa ushauri kwamba Serikali iweze kutoa fedha kwa TBC Redio ili iweze kusikika nchi nzima. Waheshimiwa Wabunge katika mwaka wa fedha 2017/2018 Shirika la TBC limefanya kazi kubwa sana katika kuboresha usikivu hasa katika maeneo ambayo ni ya mipakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukienda maeneo ya kule Namanga, Tarime, Kankoko, Nachingwea, Mtwara TBC inasikika vizuri sana. Hiyo yote ni kazi ambayo imefanyika

katika mwaka huu wa fedha na bajeti ambayo ilitengwa katika mwaka huu ambao unaenda kumalizika, bajeti ya 2017/2018, maboresho hayo yamefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 TBC ilikuwa inasikika katika Wilaya 81 tu, sasa hivi tumefikia Wilaya 100 ambazo TBC inasikika vizuri. Kwa hiyo, niseme kwamba, ushauri tumeupokea lakini kama ambavyo nimezungumza awali kwamba fedha inaendelea kutengwa na sasa hivi bajeti ya maendeleo ya TBC imepanda kufikia bilioni tano tunaamini kwamba tatizo hili litaenda kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa na Wabunge wengi ni kuhusiana na suala zima la Wasanii pamoja na BASATA, kwamba BASATA inafungia nyimbo pale ambapo nyimbo zinakuwa tayari zimekwishapigwa, halafu BASATA inakuja kufungia nyimbo hizo baadaye. Hoja hii imejadiliwa na Mheshimiwa Tauhida na pia Mheshimiwa Amina Mollel ameizungumzia vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Filamu kwa maana ya Bodi ya Filamu, Sheria ya Bodi ya Filamu pamoja na kanuni zake inataka wasanii wote ambao wanatengeneza filamu kabla hawajapeleka filamu zao sokoni wahakikishe kwamba filamu hizo zimepita Bodi ya Filamu kuweza kuhakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwa Bodi ya Filamu hata kanuni ambazo tunazo katika chombo ambacho kinasimamia sanaa kwa maana ya BASATA, tuna kanuni ambazo zinawataka wasanii wote kabla hawajapeleka nyimbo zao kuanza kurushwa katika vyombo mbalimbali vya habari, wahakikishe kwamba nyimbo hizo wanazipeleka BASATA ili ziweze kupitiwa na kama zina marekebisho ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo tunayo katika nchi yetu lakini kwa wasanii ni utii bila shuruti. Wasanii wengi hawapeleki kazi zao, nyimbo zao BASATA wala hawapeleki filamu zao. Hii ndiyo sasa imekuwa changamoto inapelekea BASATA wanakuja kushtukia tayari kazi imeshaingia sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii pamoja na changamoto mbalimbali ambazo tulikuwa nazo BASATA, lakini Serikali haina ugomvi wowote na wasanii. Ugomvi ambao Serikali inao na wasanii ni juu ya mmomonyoko wa maadili. Nichukue nafasi hii kusema kwamba Serikali na Wizara hatutaacha kulisimamia niwaombe wasanii wote kuhakikisha kwamba kazi zao kabla hawajazipeleka sokoni wanazipitisha katika vyombo hivi ambavyo nimeweza kuvitaja ili kazi hizo ziweze kuhakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo limezungumziwa pia na Kaka yangu ‘Profesa J’ Mheshimiwa Joseph Haule amesema BASATA imekuwa haina mahusiano ya karibu na wasanii badala yake sasa BASATA imekuwa kama chombo cha kuwachukulia hatua na adhabu wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BASATA imekuwa ni chombo ambacho kipo karibu sana na wasanii. Katika kudhihirisha hilo kuanzia mwaka 2010 BASATA imeandaa makongamano na matamasha mbalimbali ambayo wasanii wengi wamekuwa wakishirikishwa. Mpaka sasa wasanii zaidi ya 30,000 wameweza kushiriki makongamano hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yamewasaidia wao kama wasanii pia kuweza kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mwaka huu wa fedha BASATA imeweza kukutana na wasanii zaidi ya 2,000 na kuweza kujadili changamoto zao mbalimbali. Tatizo linalojitokeza ni kwamba baadhi ya wasanii ni kutokushiriki pale ambapo hivi vikao vinaitishwa na hivyo wanakuwa hawajui kwamba BASATA ina msimamo gani na mambo gani ambayo wao kama wasanii wanapaswa kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna hoja nyingine pia imeibuliwa hoja ya uhakiki wa video. Waheshimiwa Wabunge suala la uhakiki wa video ni suala ya Bodi ya Filamu kama ambavyo nimezungumza awali kwamba Bodi ya Filamu imekuwa ikifanya kazi nzuri sana kuhakikisha kwamba inaendelea kuhakiki kazi zote za sanaa. Mpaka sasa hivi tunavyozungumza katika mwaka huu wa fedha zaidi ya filamu 689 za Kitanzania na 155 filamu ambazo zinatoka nje zimehakikiwa. Kwa hiyo niendelee tu kusisitiza kwa wasanii kuhakikisha kwamba wanapeleka kazi zao ili ziweze kuhakikiwa na kuepusha matatizo ambayo yanaweza kuwapata hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa ni kuhusiana na vazi la Taifa. Hii ni hoja ambayo imeibua mjadala mkubwa, Mheshimiwa Lucy Owenya ameweza kuchangia pia kwa maandishi na kudai kwamba ni lini sasa mchakato wa vazi la Taifa utaweza kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa Vazi la Taifa ni mchakato ambao tayari ulikwishaanza tangu Serikali ya Awamu ya Nne ikiwa madarakani. Changamoto kubwa ambayo ilitokea katika mchakato huo ni ulipofika katika Baraza la Mawaziri na kama tunavyojua kwamba nchi yetu ni nchi ambayo ina makabila zaidi ya 120, hivyo inakuwa ni vigumu sana kuweza kujua kwamba ni vazi gani ambalo Watanzania tunaweza kulitumia kama vazi letu la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni vigumu kuweza kuamua kwamba ni vazi gani ambalo linafaa kuweza kuwa Vazi la Taifa, hivyo maamuzi ambayo yalifikiwa ni kwamba ni vema kwamba vazi la Taifa likatokana miongoni mwa mavazi ya jamii husika. Mpaka sasa hivi mchakato huo umeachwa kwa Watanzania wenyewe ili waweze kuamua kwamba ni vazi gani ambalo litawafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara tumeendelea pia kutoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari, lakini vilevile kwa kutumia tovuti yetu ya Wizara ili kuwapa nafasi sasa Watanzania waweze kujadili namna gani ambavyo wanadhani kwamba vazi gani ambalo litafaa kuwa ni Vazi la Taifa, lakini mpaka sasa hivi ni mchakato huo umeachwa kwa jamii yenyewe kwamba vazi litokane na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa ni suala la usikivu wa TBC ambapo Mheshimiwa Ramo Makani Mbunge wa Tunduru Kaskazini amezungumzia tatizo la usikivu wa TBC eneo la Tunduru. Napenda tu kuchukua nafasi hii kuweza kumhakikishia Mheshimiwa Ramo Makani kwamba katika Wilaya ya Tunduru tayari mtambo wa TBC umekwishafungwa na sasa hivi maboresho yanaendelea kufanyika. Tunaamini kabisa kwamba maboresho hayo ifikapo mwezi wa Tano maboresho hayo yatakuwa yamekwishakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna tatizo pia la usikivu wa TBC katika Wilaya ya Lushoto ambapo Mheshimiwa Shaabani Shekilindi pia ameweza kuzungumza. Niseme kwamba katika Wilaya ya Lushoto wote tunafahamu kwamba kuna changamoto ya milima ambayo kwa namna moja au nyingine imekuwa ikiathiri mawimbi ya TBC FM pamoja na TBC Taifa. Mpaka sasa hivi ninavyoongea tayari tumeshapata eneo ambalo litatumika kufunga huo mtambo na tunaamini kabisa kufikia mwezi Mei, tatizo la usikivu wa TBC katika Wilaya ya Lushoto litakuwa limeshakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Machano Othman Said pia amezungumzia tatizo la usikivu Zanzibar. Nichukue nafasi hii kuweza kumhakikishia tu Mheshimiwa Machano kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019, tayari Zanzibar imewekwa kwenye kipaumbele katika kuonesha kwamba tunaboresha usikivu wa TBC na siyo tu kwa Zanzibar peke yake, kuna mikoa mitano ambayo ni Mkoa wa Songwe, Mkoa wa Simiyu, Katavi pamoja na Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine pia ambayo imeibuliwa na Mheshimiwa Rhoda Kunchela ambaye amesema kwamba Serikali iweke ofisi za usajili kila mkoa kwa ajili ya wasanii kuweza kununua sticker za TRA. Ni kweli Mheshimiwa Rhoda kwamba mpaka sasa hivi sticker za TRA zinapatikana katika Mkoa mmoja tu ambao ni Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tayari jitihada za makusudi zimeanza kufanyika na mpaka sasa hivi ninavyoongea Kamati ya Urasimishaji imekwishakaa na sasa hivi tunaandaa utaratibu mzuri kabisa ili kwamba sticker hizo hata wasanii ambao wanapatikana mikoani waweze kuzipata kwa njia ya kununua hizo sticker kwa njia ya mtandao. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba hili litakapokamilika itakuwa ni njia mojawapo ya kutatua tatizo la usumbufu wa kuwatoa wasanii kutoka mikoani kuja kununua sticker hizo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imejadiliwa ni hoja ambayo ameizungumza Mheshimiwa Peter Lijualikali ambaye amesema kwamba kama Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kukarabati viwanja vyake ni vema viwanja hivyo vikarejeshwa Halmashauri. Mpaka sasa hivi Chama cha Mapinduzi hakijashindwa kukarabati viwanja vyake na nasema hilo nikiwa na ushahidi na uhakika kwa sababu hata ukiangalia katika Mkoa wa Singida kiwanja ambacho kinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi Kiwanja cha Namfua kimeshakarabatiwa na kipo kwenye ubora wa kisasa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Uwanja wa Sokoine Mkoa wa Mbeya ambao nao upo kwenye ukarabati. Vilevile kuna uwanja mwingine ambao pia Mheshimiwa Mbunge ameweza kuuzungumzia Uwanja wa Samora Iringa. Kwa hiyo, siyo Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kukarabati viwanja vyake, nasi ndani ya Chama cha Mapinduzi kuna msisitizo kuhakikisha kwamba chama kinakarabati viwanja vyake, lakini ni vema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.