Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hoja hii iliyopo mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia RCC ya Mkoa wa Tanga na vikao vya Mfuko wa Barabara vya Mkoa (Road Board)kwa miaka miwili mfululizo tulikuwa tukipanga fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu (feasibility study) pamoja na detailed design barabara ya Lushoto hadi Mlalo kilometa 45. Hata hivyo, kwa mara zote ombi letu lilikuwa halipokelewi mara linapofika kwa Afisa Mtendaji wa Wakala wa Barabara wa Taifa (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi na ustawi wa maendeleo ya Mlalo. Ikumbukwe kwamba uchumi wa wananchi wa Mlalo unategemea sana kilimo cha mboga mboga na matunda. Matunda na mboga mboga ni bidhaa ambazo zinaoza kwa haraka sana. Hivyo basi, ili kujenga uchumi imara, tunahitaji barabara madhubuti ambazo zitafikisha mazao yetu sokoni kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara kwa mara barabara zetu zimekuwa zikijifunga nyakati za mvua kutokana na landslide (maporomoko) hivyo kwa dhati kabisa tunaiomba Serikali yetu sikivu isikie kilio chetu tupate barabara ya kiwango cha lami. Eneo hili ni kilometa 45 tu kutoka Lushoto Mjini hadi Mlalo ambapo ndiyo kituo cha mwisho cha mabasi yaendayo maeneo tofauti ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Mlalo – Mng’aro kilometa 20, imepandishwa hadhi hivi karibuni miaka ya 2012 na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete. Baadhi ya nyumba zilizopo pembezoni mwa barabara hiyo zimewekwa alama ya “X”, tunapenda kujua tafsiri ya alama hizo kwa sababu wananchi wanashindwa kuelewa hatma ya nyumba zao na wanashindwa kuziendeleza. Hivyo, tunaomba Serikali itoe tafsiri ya alama hizo ili wananchi waweze kujipanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mawasiliano ya simu za viganjani bado siyo rafiki sana, yapo maeneo ambayo yapo katika mabonde na yamefunikwa na vilele vya milima, mfano katika Kata ya Malindi hasa Kijiji cha Makose na kata ya Rangwi eneo la Longoi Mtaa wa Bustani na katika eneo lote la Mliifu Kata ya Manolo. Tunahitaji msaada huu kwa wananchi wa maeneo niliyoyataja ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Jimbo la Mlalo hususani Makose, Longoi, Mliifu, Hambayo na Viti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.