Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha na mimi kufika mahali hapa na kuchangia bajeti hii iliyopo mbele yetu. Bajeti hii inakwenda kutekeleza mipango, miradi mbalimbali ya kimaendeleo, vilevile inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kuandaa bajeti nzuri yenye mrengo chanya wa kubadilisha sekta nzima ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na mipango mbalimbali ya kimaendeleo, mipango hiyo ni pamoja na miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) yenye urefu wa kilometa 1,219 uendelezwaji wa barabara zikiwemo za juu (flyover) pamoja na kununua meli na vivuko, pia kulifufua shirika letu la ndege na kuliwezesha sasa kuanza kutoa huduma ndani na nje ya mipaka kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongeza kwa Serikali kwa kuendelea kuboresha mtandao wa barabara nchini, ujenzi wa kilometa 776.45 za barabara kuu kwa kiwango cha lami umekamilika na kilometa 1,760 zikiendelea kujengwa. Vilevile barabara zenye urefu wa kilometa 17,054 zimekarabatiwa, ujenzi wa madaraja mbalimbali kukamilika na mengine kukarabatiwa, hizi ni hatua nzuri zilizofikiwa na Serikali katika kuhakikisha miradi hii inakwenda kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuja na mpango wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency-TARURA) mpango huu ni mzuri kwani unakwenda kurahisisha huduma za usafirishaji na kuongeza kasi ya wananchi kujiletea maendeleo, lakini bado tuna changamoto mbalimbali ambazo naishauri Serikali kuzichukua kama fursa na kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimboni kwangu na maeneo ambayo mradi wa barabara ya Bagamoyo – Mlandizi - Mzenga umepita hawajalipwa fidia mpaka leo na kukaa kwa muda mrefu bila kuwalipa fidia, hivyo kuwasababishia hasara kwani kiwango wanachotakiwa kulipwa kitakuwa ni kilekile ili miaka inavyozidi kusonga mbele gharama ya vitu inazidi kupanda juu.

Naiomba Serikali hasa katika bajeti hii kuwapa kipaumbele wananchi wangu niliowazungumzia hapo awali walipwe fidia zao na wao waendelee na shughuli zao za kimaendeleo, hata hivyo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha bajeti yake aje na majibu ya wananchi hawa ili waweze kusikia kauli ya Serikali juu ya lini sasa watalipwa fidia zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, Soga kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa reli, mradi ule umeleta ajira kwa wananchi wangu na wa maeneo mengine pia, lakini naleta ombi kwa Serikali tunahitaji barabara ya kiwango cha lami kutoka Kongowe - Soga ijengwe kwani kujengwa kwa barabara hiyo kutarahisisha shughuli za usafirishaji na kufikika kwa urahisi kwenda kwenye mradi husika na kuleta maendeleo kwa wananchi. Vilevile barabara ya Bagamoyo - Makofia – Mlandizi - Mzenga zijengwe kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za kibiashara kwani eneo hilo ni muhimu kiuwekezaji na pia naishauri Serikali kujenga bandari ya nchi kavu eneo hilo ili mizigo itakayoshushwa Bandari ya Bagamoyo iweze kuhifadhiwa mahali hapo na kuleta nafuu kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Kwala, Dutumi na Vigwaza barabara hiyo nayo tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za kimaendeleo na kuinua uchumi wa maeneo husika. Kama nilivyosema hapo awali kuhusu hizo barabara zina umuhimu sana kwa maendeleo ya Jimbo langu na kwa nchi kwa ujumla na zikikamilika zitasaidia kuleta maendeleo kwa haraka na kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mawasiliano ya simu yanavyosaidia katika nyanja mbalimbali katika dunia ya leo, hata hapa nchini kwetu tumeona jinsi mawasiliano ya simu yanavyoleta tija kwa watu wetu na hata kutoa huduma mbalimbali za kifedha kwa kupitia mitandao hiyo ya simu. Hata hivyo, teknolojia hii imeleta pia maendeleo mbalimbali kwa wale watu wanaotumia kwa mrengo chanya. Pongezi ziende kwa Serikali kwani wameendelea kuboresha maeneo mbalimbali, kama kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, hatua hii ni nzuri na imesaidia sana pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhia data.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo Jimboni kwangu wananchi hawana kabisa mawasiliano ya simu, kwa maana hakuna minara maeneo hayo ambayo ingewawezesha wananchi hawa kupata mawasiliano ya simu katika shughuli zao za kila siku, maeneo hayo ni Kata ya Boko - Mpigi, Mkalambati, Kata ya Doga - Kipangege, Misufini, Kata ya Kawawa - Kimara, Makazi Mapya, Makutupora, Msua, Mpelamumbi, Waya; Kata ya Mtongani- Madimia, Kisabi; Kata ya Kikongo- Ngeta, Mkino, Lupungo; Kata ya Ruvu - Kitomondo, Ruvu Station; Kata ya Dutumi - Madege, Dutumi, Muembe Ngozi; Kata ya Gwata - Mguruka, Vinyenze, Ndwati, Kigoda; Kata ya Magindu - Lukenge, Masaki, Miyombo, Lukalasi, Magindu Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua katika mpango wa Serikali kama ulivyoainishwa wa kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini. Je, maeneo hayo niliyoyaorodhesha hapo juu yatapatiwa mawasiliano katika mwaka huu wa fedha na kama si katika mwaka huu basi naomba kujua ni lini maeneo hayo yatapata mawasiliano na kuondokana na kero hiyo ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika mradi wa ujenzi wa barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam na kuishia TAMCO ni mpango mzuri wa kimaendeleo, lakini nina ombi na ushauri kwa Serikali yangu sikivu, mradi huu usingeishia tu tamko bali mradi huu ungeendelea mpaka Chalinze na kufika Morogoro kwani uhitaji wa mradi huo kwa maeneo hayo upo na utasaidia sana kuleta maendeleo kwa haraka, kurahisisha shughuli za usafirishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.