Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Itoni Njombe – Ludewa -Manda imeanza kujengwa tayari kilometa 50 lakini ujenzi wake unaenda taratibu mno. Ikumbukwe barabara hii inaenda kwenye miradi kielelezi ya Mchuchuma na Liganga. Barabara hii ina vipande vinne vya ujenzi (lots), tunaiomba Serikali kwa umuhimu wa miradi hii tuongezewe kipande kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kandokando ya Ziwa Nyasa - Lupingu- Matema (kilometa 139). Eneo hili ambalo linapakana na nchi ya Malawi halina barabara kabisa na hivyo kufanya vijiji 15 kutokuwa na mawasiliano ya barabara. Hata hivyo, wananchi wameanza jitihada za kulima kwa kutumia zana duni za majembe, nyundo, mitalimbo, mapanga na kadhalika. Hivyo, tunaiomba Serikali kuchangia jitihada za wananchi kwa kutoa fedha kwa mfumo wa Force Account. Eneo hili lina tija kwa nchi, kwani lipo mpakani mwa nchi kwa hiyo lina umuhimu kiutalii, kiulinzi na kiusalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ndiyo pekee katika mpaka wa nchi ambalo halina barabara. Mbamba Bay - Lituli (kilometa 112) barabara ipo, Matema - Ikombe (kilometa 10) barabara ipo lakini eneo hili ambalo ndiyo katikati halina huduma ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ione sasa umuhimu wa kuunda Bodi ya TEHAMA nchini kutokana na kukua kwa teknolojia ya TEHAMA ili kudhibiti mfumuko wa watu wasiozingatia taratibu na kanuni za uendeshaji wa TEHAMA. Imefikia wakati sasa wa kuwa na Bodi ya Wanataaluma ili kutengeneza udhibiti na uendeshaji mzuri. Pia viwango vya elimu katika kada hiyo vizingatiwe ili kuepuka muingiliano na pia vifaa vilivyoisha muda wake viharibiwe ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeanza ujenzi wa minara katika Kata za Lupingu, Makonde, Kilondo na Lumbila. Tunaipongeza Serikali kwa zoezi hilo lakini imenza kazi hiyo katika Kata ya Lupingu, Vijiji vya Nindi na Ntumbati. Zoezi hilo ambalo limeanza katika vijiji hivyo linaenda taratibu mno. Tunaiomba Serikali iongeze msukumo katika ujenzi wa minara hiyo ya mawasiliano ya simu. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Engineer Nditiye kufuatia ziara yake aliyoifanya Jimboni Ludewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuiombe Serikali sasa kutupatia vituo vya kupakia na kushusha mizigo katika vijiji vya Nkwimbili (Yigha), Makonde, Nsele, Chanjale na Nkanda vilivyopo kando kando ya Ziwa Nyasa. Hii ni kutokana na umbali kati ya kijiji na kijiji na pia ndiyo njia pekee ya usafirishaji kwa maeneo hayo na usafirishaji wa mizigo hasa ya kibiashara umekuwa mgumu sana, imefikia wakati sasa wananchi kupitia Serikali kuondoa kero hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la wananchi walioachia maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa bandari kwa vijiji vya Manda na Lupingu katika Wilaya ya Ludewa. Ni lini fidia italipwa na ujenzi wa bandari hizo utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Shirika la Posta Tanzania, Serikali imekuwa ikilipa shirika hili mzigo wa kuwalipa pensheni wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta la Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupelekea shirika kuyumba katika uendeshaji. Mpaka sasa Serikali inadaiwa shilingi bilioni 4.7. Hali hii inaliyumbisha shirika kwa kiasi kikubwa. Je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa kuondoa kero hii kwani inafifisha uendeshaji wa shirika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TTCL, natoa wito kwa Serikali kulipa uwezeshaji shirika ili liweze kutengeneza mtandao mpana wa kimawasiliano nchini. Aidha, shirika hili lipewe nguvu za ushindani katika soko.