Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango wangu. Leo nilivyokuwa nikijiandaa kuchangia niliona ni vyema kupitia Ilani za Uchaguzi za vyama vitatu vilivyoweka wagombea wa Urais mwaka 2015 ili kuona sintofahamu ambayo imekuwa ikitokea mara kadhaa hasa hasa humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nimekiona ni jambo moja kubwa tu kwamba hatupaswi kushambuliana kwa sababu Mheshimiwa Rais anafanya mambo ambayo hata wapinzani walipaswa kumpongeza. Leo nitatoa mifano kadhaa kudhibitisha hili, naomba mnisikilize kwa makini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa kwanza Shirika la Ndege la Kitaifa; katika Ilani ya Uchaguzi wa CCM aya ya 41 tuliahidi naomba kunukuu

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo Chama cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali kufanya mambo yafuatayo; kuimarisha huduma za Shirika la Ndege la Taifa.” mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani ya Chama cha UKAWA, ukurasa wa 40 eneo la miundombinu walisema naomba kunukuu:

“Kujenga Shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida.” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani ya Uchaguzi ya ACT Wazalendo, aya ya 5.23, ukurasa wa 20 waliahidi naomba kunukuu:

“Kuunda upya Shirika la Ndege la Taifa ili iwe chachu ya kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amehakikisha anafufua Shirika la ATCL kwa kununua ndege sita ili kuongeza njia, kukuza biashara, kupata faida na mapato ya fedha za kigeni. Rais ametekeleza Ilani ya CCM, UKAWA na ACT Wazalendo kwa mpigo, haunganishi nchi huyu? Anaunganisha jamani. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimwa Mwenyekiti, mfano wa pili ni reli, Ilani ya Uchaguzi wa CCM ukurasa wa 56 tuliahidi naomba kunukuu:

“Kuanza ujenzi wa reli zifuatazo kwa kiwango cha Kimataifa (standard gauge) kama ifuatavyo:- Dar es Salaam, Tabora, Kigoma, Mwanza, Uvinza, Msogati, Burundi na Isaka mpaka Kigali Rwanda, Mtwara, Songea, Mbambabay na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga, Tanga, Arusha, Musoma, Kaliuwa, Mpanda, Kalema”.

Ilani ya uchaguzi ya CHADEMA, ukurasa wa 40 waliahidi, nanukuu:

“Kujenga reli mpya kukarabati zilizopo kwa viwango vya kisasa.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amehakikisha ujenzi wa reli ya kisasa ya kimataifa umeanza. Rais ametekeleza matakwa ya CCM na ya UKAWA, Rais anaunganisha nchi, huu sio muda muafaka wa kumpinga Rais, huu ni muda muafaka wa kumuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri kwa ndugu zangu wapinzani waibue masuala mapya yale waliyokuwa wakisema kila mwaka tumepata Rais ambaye anayatekeleza. Haitakuwa mbaya wao wakiona wameishiwa hoja wafunge milango, wahamie kwetu, haitakuwa mara ya kwanza wala hakuna atakayewacheka. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema miaka ya 1960 kuna chama kinaitwa United Tanganyika Party, waliokuwa enzi hizo watakijua, kilifunga ofisi kikahamia TANU kwa kuonekana hawana hoja za msingi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1963 kulikuwa kuna Chama kinaitwa ANC cha Zuberi Mtemvu mtakuwa mnakijua miaka hiyo kilifunga ofisi na kuhamia TANU kwa kuwa hakikuwa na hoja. Kwa hiyo na wao kama hawana hoja mpya, tunawakaribisha CCM, tujenge nchi na tutawapokea vizuri kwenye Ukumbi wa JK, barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu anafanya kazi kwa bidii, anajitahidi huu sio muda muafaka wa wao kumbeza, kumdharau, kumdhoofisha badala yake ni kumuunga mkono kwa bidii na Rais anatekeleza matakwa ya Watanzania wote inapokuja suala zima la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.