Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii, lakini niseme kwamba wote tunakubaliana kwamba tunaipeleka nchi yetu kuwa ni nchi ya viwanda na nchi ya pato la kati. Kuipeleka nchi hii kwenye nchi ya viwanda na nchi ya pato la kati haitawezekana kama hatutazingatia kilimo ambacho kitamshirikisha kila Mtanzania kumwingiza kwenye uchumi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida moja ambayo tunatakiwa tuifute kwenye vichwa vyetu ya kujiamini kama sisi tunaweza, lakini kuwaamini Watanzania na wakulima wetu walioko kule wanaweza hata kuliko watu wanaotoka nje kuja kuwekeza katika nchi hii. Nikitolea mfano Wilaya ya Siha, ni Wilaya ambayo imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba na iliyozunguka Mlima wa Kilimanjaro; ni ardhi ambayo ukihesabu ekari zake ni karibu mara mbili ya idadi ya watu wa Siha wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ikiaminika kwamba sisi watu wa Siha hatuna uwezo wa kuwekeza wala wa kulima, inatakiwa waje watu wengine kutoka nje wawekeze ndiyo wenye uwezo huo. Leo, nashukuru maana jana nilikuandikia kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kuhusu Gararagua kidogo hukunijibu nikawa na hasira kidogo, lakini nilivyokuona umeshika ng„ombe hapa, nikakupenda bure, kwa hiyo, sikushughulikii! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo watu wameitana siri siri kule Mkoani kwangu, wanajadili kuuza shamba la Gararagua. Wanajadili kuuza ardhi ya Siha kwa sababu wanaamini sisi Watanzania hatuna uwezo wa kuwekeza. Bado tunazungumza kuwatoa watu wa Tanzania waingie kuwa ni watu wa uchumi wa kati, haiwezekani kama hatutafika mahali tukaamini Watanzania wanaweza na kupitia Watanzania tunaweza tukawekeza kwenye ardhi iliyopo Tanzania na tunaweza tukawekeza kwenye kila kitu na rasilimali zilizopo Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatusemi „tusikubali uwekezaji,‟ tunawapenda wawekezaji, tunapenda uwekezaji kutoka nje, lakini tunahitaji uwekezaji wenye maslahi kwa Umma. Tunahitaji uwekezaji ambao mwisho wa siku uwekezaji huo unamfanya mwekezaji huyo apate alichokuja kukichukua, lakini unafanya nchi ipate, lakini Mtanzania wa kawaida naye apate kutokana na uwekezaji huo. Ndiyo uwekezaji ambao tunausema na tunauhitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia masuala ya mifugo. Bahati nzuri Profesa jana alikuwa anasema ukifuga unapata sh. 8,000/=, lakini mimi nina kaka yangu anamiliki ng‟ombe zaidi ya 450 na kila miaka mitano anavuna mara nne na anavuna kila mwaka milioni 150. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi hoja za theses za watoto wa Kizungu wanaposoma Masters huwa mara nyingi hazitusaidii. Ninachoweza kusema ni kwamba tukiwekeza kwenye kilimo, kwenye mifugo tunachoweza kutupa tu ni sauti ya hiyo mifugo! Mifupa ni pesa, ngozi ni pesa, nyama ni pesa, kwato ni pesa, pembe ni pesa, damu ni pesa na kila kitu ni pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na wanaosema tunahitaji tufuge mifugo kwa kiwango kulingana na ardhi tuliyonayo, lakini kuna shida iliyotokea, wazee wetu huko nyuma walikuwa wanamiliki ardhi kimila, wanamiliki Communal Owned Land, lakini ilikuja ikaonekana kwamba ardhi hizo ni tupu na wawekezaji wakapewa. Wakulima wanakosa pa kulima, wafugaji wanakosa pa kufuga, matokeo yake wakulima na wafugaji wanakutana kwenye maeneo ambapo mkulima hana ardhi wala mfugaji hana ardhi wanaishia kugombana bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuseme, hata kama tunazungumzia popote ambapo kuna matatizo ya kifugaji; wafugaji kupigana na wakulima, wakulima na wafugaji ni ndugu, ni Watanzania wamoja ila ni mfumo umewafanya wagombane. Twendeni sasa kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, hebu amka nenda mkatusaidie sasa tuhakikishe wakulima na wafugaji hawapigani tena kwa sababu wanapendana, ni Watanzania wanataka kuwa wamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila ku-undermine kazi ambayo inafanyika na Wizara ya Kilimo kule Siha kutusaidia kuhakikisha tunamaliza migogoro, lakini niseme kuna suala la KNCU. KNCU imekufa! KNCU haifai! Leo wanataka kuuza shamba la Gararagua shilingi bilioni 12; walipe shilingi bilioni nne CRDB, shilingi bilioni nane ziende KNCU. Kama wameua KNCU, unawapelekea shilingi bilioni nane za nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, hata kama basi Serikali haina, Hazina ilipe shilingi bilioni nne. Kama inaonekana uwekezaji huo ni mzuri, wananchi wapate ekari za kuwekeza kwa pamoja. Waziri Mkuu nakushukuru, nikikueleza unanielewa na nimekueleza sasa hivi, umenielewa vizuri. Niseme tu kwamba, kama kuwekeza, tumesema tuna vijana wa Vyuo Vikuu wanamaliza, tuwekeze hicho kilimo kinacholimwa na huyo Mzungu, tuwape mikopo halafu walime, Watanzania waendelee na hiyo shilingi bilioni nne isiende KNCU. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. GODWIN A. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana, nawashukuru…