Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kuwapongeza sana Mawaziri wanaosimamia Wizara, hii kwa maana ya Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa na Makatibu Wakuu wote na watumishi wote wa Wizara hii ya Ujenzi kwa namna wanavyofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba miundombinu mingi inatengenezwa hasa barabara na mambo mengine ya viwanja vya ndege na bandari. Niwapongeze sana, wanafanya kazi kubwa sana ambayo itasaidia kusukuma maendeleo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haipingiki ni kwamba tunavyoboresha barabara, tunavyoboresha viwanja vya ndege, tunavyoboresha bandari na miundombinu mingine tunachochea kwa kasi kubwa sana maendeleo. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali, inafanya kazi kubwa sana. Tayari tumeshaona maeneo ambako barabara za lami zimefunguliwa, maeneo ambako kuna ujenzi wa reli na maeneo mengine ambapo miundombinu inatengenezwa, tayari kasi ya maendeleo imeanza kuonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali tuendelee bila kukata tamaa na kusikiliza maneno ya watu ambao wanabeza maendeleo haya. Tumwombe Mheshimiwa Rais aendelee kutusaidia kuhakikisha kwamba Watanzania tunatoka hapa tulipo tunaenda mbali zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuongelea kuhusu Jimbo langu hasa barabara ile ya Kibena – Lupembe – Madeke - Morogoro. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Njombe na Morogoro na ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, lakini pia kwa uchumi wa Mkoa wa Njombe. Katika eneo ambako barabara hii inapita, eneo lote la Lupembe na Jimbo zima tunazalisha mbao kwa wingi sana. Mbao mnazoziona Dodoma asilimia 40 zinatoka kule Lupembe lakini eneo hili pia tunazalisha nguzo za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hapa kwamba tunataka kila kijiji kiwe na umeme, nguzo zinatoka katika maeneo haya kwa asilimia kubwa sana. Eneo hili pia tunazalisha chai kwa wingi sana, kahawa, mahindi, maharage na aina zote za matunda kama vile parachichi, papai, nanasi, ndizi na matunda mengine mengi. Eneo hili lina mvua nyingi, takribani miezi nane katika kipindi cha mwaka mzima ni kipindi cha mvua. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwa namna gani ni muhimu sana hizi barabara za maeneo haya ziweze kutengenezwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, barabara hii ilipangiwa shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami na mwaka wa 2017/2018, tulipanga shilingi bilioni mbili na mwaka huu nashukuru sana Wizara na Serikali kwa ujumla tumepangiwa shilingi bilioni tano. Niombe sana bado barabara hii haijatangazwa kwa maana ya zabuni, haijatangazwa ili kuweza kumpata mkandarasi ili aanze kutengeneza barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba upembuzi yakinifu umeshakamilika, usanifu umeshafanyika lakini bado ujenzi wake haujatangazwa. Niombe sana Wizara hii ya Ujenzi itusaidie ili barabara hii iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami na hatimaye tuweze kusafirisha mazao haya niliyoyataja kwa urahisi zaidi ili yaweze kufikia soko kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukipoteza fedha nyingi sana hasa kwenye mazao haya ya chai, mbao na mazao ya matunda kama nilivyoyataja. Kwa mfano, mwaka huu tu kuanzia Januari mpaka sasa hivi mwezi wa kwanza wananchi wa Madeke walipakia nanasi tani 40 kwenda kuuza sokoni lakini tani hizi zote 40 zimeozea njiani kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo katika barabara hii yameharibika, magari hayawezi kupita mfano maeneo ya Mtakuja, baadhi ya maeneo ya Kidegembye na maeneo mengine mengi tu. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi tunavyopoteza uchumi katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki mbili zilizopita tumepakia maparachichi tani 30 katika vijiji viwili tu, unaweza ukaona ni shilingi ngapi hizo. Baada ya kuwaka jua kidogo tu siku mbili, tatu tukaweza kusafirisha tani 30 za parachichi kutoka kwenye vijiji viwili tu na parachichi kilo moja ni Sh.1,150. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni namna gani hii barabara inavyochelewa kutengenezwa tunavyopoteza fedha nyingi na wananchi wanavyoingia hasara kutokana na ubovu wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali barabara hii tuipe kipaumbele ili angalau mwaka huu mara baada ya kupitisha bajeti hii, basi itangazwe, tupate mkandarasi aanze kutengeneza barabara hii. Kwa sababu tukiunganisha Mkoa wa Njombe na Morogoro na Mkoa wa Morogoro ni wazalishaji wakubwa sana naamini pato la Taifa litaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiunganisha kwa mfano, Mkoa wa Njombe na Morogoro, tukaunganisha Mkoa wa Njombe, Makete na Mbeya, tukaunganisha Mkoa wa Njombe kupitia Ludewa na mikoa mingine kimsingi tutapata maendeleo makubwa sana kwa sababu haya ndiyo maeneo yanayotegemewa kwa chakula na ndiyo maeneo yenye uchumi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hii barabara wananchi wetu wa Jimbo la Lupembe hawanielewi ni kwa nini barabara hii kandarasi haitangazwi wakati imesanifiwa muda mrefu na tayari ilitakiwa iwe imeshaanza kutengenezwa muda mrefu. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ashughulikie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna barabara moja ya Ilunda – Igongolo – Kivitu - Ilengititu – Kifumbe. Barabara hii inasimamiwa na TANROADS, lakini imekuwa ikitengenezwa kilometa tisa tu, imeishia sehemu fulani njiani, kule mbele haiendelei kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana TANROADS waongeze kipande kile kingine kwa maana waende Kijiji cha Kivitu kutoka Idonda, Igongoro waende Kivitu baadaye iende Ilengititu na itokeze kule Kifumbe ambako ni Jimbo la Makambako ili angalau tuweze kutengeneza mtandao mzuri wa barabara na hatimaye mazao ya eneo lile yaweze kusafirishwa kirahisi zaidi hasa wakati wa mvua. Kama nilivyosema Jimbo langu mimi linapata kipindi kirefu sana cha mvua, miezi nane mvua inanyesha, kwa hiyo inapofikia wakati wa kuvuna mazao haya hayawezi kufikia soko kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu minara ya simu kwa maana ya mawasiliano. Kuna kata kama tano hivi simu hazishiki vizuri hasa Kata zile za Ninga, Ikondo, Mfiga lakini pia na maeneo mengine ya vijijini ambako simu hazishiki vizuri. Nilishapeleka taarifa na nashukuru kwamba Waziri aliniahidi kwamba mwaka huu wa fedha watapeleka minara katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tujitahidi ili tuweze kufungua mawasiliano na hatimaye waweze kufanya biashara na shughuli zao za kiuchumi vizuri. Maana biashara za kilimo ni lazima uwe na mawasiliano ya karibu sana na soko. Kama hakuna mawasiliano ni vigumu sana kujua ni wapi bidhaa yako uweze kuipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwafungulia mawasiliano na tukawa tumetengeneza barabara hizi kama nilivyosema hasa barabara kuu hii ya Kibena – Lupembe – Madeke – Mlimba - Morogoro, kasi ya uchumi itakua na hatimaye maisha ya Watanzania yataboreshwa kwa sababu uzalishaji utakuwa umeongezeka na bidhaa zao zitazalishwa kirahisi zaidi kwa sababu barabara ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nirudie kuipongeza Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jitihada anazozifanya kuhakikisha kwamba anafungua mawasiliano katika nchi hii. Niwapongeze Mawaziri wote kwa maana ya Waziri Profesa Mbarawa na Naibu Mawaziri Mheshimiwa Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa. Pia nimpongeze Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo wanafanya. Niombe sana Mwenyezi Mungu awabariki ili waendelee kuwa na afya njema na hatimaye waweze kutuletea sisi Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.