Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi jioni hii ya leo ili na nitoe mawili, matatu kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake na Watendaji wengine kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini bado naomba niendelee kumtia moyo sana Rais wetu nimefarijika sana kwa michango ambayo imeendelea kutoka kwa upande wa pili kwa sababu nimeona hakika msumari kwa kweli umeingia na ndiyo maana maneno ya kupinga kila kitu ambacho ni kizuri yameendelea kutoka ndani ya nyumba hii, hivyo naomba kuendelea kumtia moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze mawili, matatu. Kwanza nipongeze sana kwenye mpango uliopo katika kitabu hiki hasa kwa upande wa Mkoa wangu wa Singida, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Nianze na upande wa Daraja la Sibiti pamoja na barabara aliyoitaja kutoka Mbulu kuja Haydom hadi Sibiti kwenda Maswa. Fedha alizotenga kwa kweli ni ndogo sana sielewi hizo fedha ni za nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana barabara hiyo ya Sibiti pamoja na kwamba inaenda Mbulu, naomba itoke Sibiti ije Mkalama ije Nduguti ije hadi Iguguno iwe ya lami. Hatuwezi kujenga daraja zuri lenye kiwango kikubwa lakini barabara isiwe ya lami, naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Waziri ametaja daraja la Msingi, naomba sana daraja lile kuna madaraja mengine madogo madogo ambayo naamini TARURA itaenda kuyafanyia kazi, lakini naomba sana barabara ile ambayo imepita Kinampanda kushuka Msingi kwenda Gumanga imaliziwe iwe ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia barabara ya kutoka Singida Mjini kupita Sipuka hadi Ndago kwenda Kizaga. Ile barabara ni ya lami na ni ya ahadi ya Rais, naomba sana sijaona kama Mheshimiwa Waziri ameitaja, nashukuru kwa zile ambazo amezitaja, mimi nataja zile ambazo bado hajazitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru kwa kipekee naomba Mheshimiwa Waziri apeleke salamu kwa Mheshimiwa Rais, barabara inayotoka Tanga inayopita Kondoa inakuja kwa Mtoro inakuja Simiyu hadi Singida barabara ile ni kwa ajili ya Bomba la Mafuta ambalo litakuja kuinua uchumi mkubwa sana kwa wananchi wa Singida. Napongeza sana na nashukuru lakini fedha walizotenga hazitutii moyo sana, naomba atakapokuja atutie moyo kwamba zitamalizika lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuwapongeza watu wa mawasiliano. Nawapongeza TTCL kuna mmoja alizungumza kwamba Watanzania sasa tujivunie shirika letu, ni kweli na naunga mkono. Naomba sana TTCL wapewe uwezo mkubwa wa kutandaza mtandao nchi nzima ili wananchi walioko vijijini waweze kupata mawasiliano ya kutosha, lakini naomba hasa kwenye maeneo ambayo ni hatarishi kwa mfano Sekenke pale ukiwa unashuka ule mlima Sekenke hamna network, mtu akipata tatizo hawezi kuwasiliana. TTCL naamini wameshakuja vizuri wana-perform vizuri, wawezeshwe ili waweze kuweka mtandao nchi nzima wananchi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBA wamefanya kazi nzuri, naomba waongezewe bajeti ili waweze kukarabati na yale majengo ambayo yamechakaa sasa hivi. Kwa mfano ya hapa Dodoma wanayoishi Waheshimiwa Wabunge, yamechakaa waongezewe ili waweze kukarabati yale majengo. Wapeni nafasi waweze kujenga hapa Dodoma majengo ya Serikali kwa sababu majengo yao nikiyatazama ni yanadumu na ni imara, yanaishi kwa muda mrefu. Wawezeshwe ili waweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba sana kwenye upande wa barabara za vijijini kuna TARURA, TANROAD Mkoa na kuna Taifa. Mheshimiwa Waziri atakapokuja naomba aje atufafanulie vizuri barabara zipi hasa maana yake zile tunazozitaja, kwa mfano ukienda Singida kuna yale madaraja makubwa ambayo atasema hizo barabara ni za vijijini, lakini TARURA hataweza kwa sababu ya bajeti ndogo. Kwa hiyo, naomba sana watakapokuja hapa waje watufafanulie TARURA… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)