Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia. Kwanza nieleze masikitiko yangu kwenye Wizara hii juu ya uamuzi wa Serikali wa kuvunja nyumba za wananchi wa Ubungo, Kimara na maeneo mengine ya Dar es Salaam hasa baada ya Mahakama kutoa amri ya kuzuia ubomoji ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubomoaji umefanyika kinyume cha taratibu na namwomba Waziri kwa kuwa nyumba za wananchi wa Dar es Salaam zimevunjwa na tayari Benki ya Dunia imesimamisha msaada kwa Serikali kwa ajili ya ujenzi wa hizo barabara, kwa kuwa ujenzi umekiuka taratibu, kanuni na haki za binadamu zimevunjwa, nataka Serikali iwafidie wananchi wa Ubungo ambao nyumba zao zimevunjwa bila kufanya tathmini ya kile kilichovunjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi uliopo ni kwamba sasa Serikali italazimika kulipa fidia ili mradi uendelee, lakini fidia hii ilinalipwaje kwa nyumba ambazo tayari zimevunjwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie utaratibu mzuri kabisa wa wananchi wa Ubungo kufidiwa nyumba zao zilizovunjwa. Nyumba hizi zimejengwa katika mazingira magumu, watu hao wengine walikuwa watumishi wa umma, wamejitolea katika Taifa hili wamelipwa kiinua mgongo chao, wamejenga mabanda yao, nyumba zimevunjwa kinyume na sheria ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza tumeona barabara inakatwa kutoka mita 121.5 katikati ya barabara. Wataalam wanasema mita 121 ni uwanja wa mpira. Kwa hiyo, hivyo ni viwanja vya mpira viwili ndiyo inajengwa barabara ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni juu ya barabara ambazo zimetajwa katika kitabu cha Waziri, katika ukurasa wa 203 imetajwa barabara ya Nzega, Tuge hadi Tabora. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, barabara hii ilishakamika miaka miwili iliyopita leo inatengewa fedha na Wabunge hapa wapo hapa ambao wana barabara zao hazijajengwa. Kule Rufiji barabara haijajengwa tokea wakati wa Bibi Titi Mohamed, Mbunge anasimama hapa analia asubuhi, anaomba ijengwe barabara, lakini barabara inapelekwa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ATCL. Wabunge wamezungumza na watu wengi wamezungumza kwenye nchi hii juu ya mchakato mzima wa ubinafsishaji wa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). Mchakato ulitawaliwa na viriba, ulitawaliwa na udanganyifu na haukufuata taratibu zozote za ubinafsishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shirika likabinafsishwa lakini baadaye Serikali ikalazimika kununua hisa zake ilizouza katika Shirika la Ndege la Afrika Kusini, Shirika likarudi Tanzania, Serikali ikamiliki hisa za ATCL, leo tunafufua shirika ni kazi nzuri nawapongeza kwa kufufua shirika mmefanya kazi nzuri. Sisi wazalendo wa nchi hii tulikuwa tunalililia shirika hili liwe shirika letu la umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wameingiza nchi hii hasara kubwa kwenye ATCL. Tarehe 9 Oktoba, 2007, ATC ilisaini mkataba wa ukodishaji wa ndege aina ya Air bus na Kampuni ya Wallis Trading Company. Taarifa zilizopo ukaguzi wa ndani haukufanyika kujua ubora wa ndege wala Shirika la Anga la Tanzania halikushirikishwa. Matokeo yake baada ya muda mfupi ndege ile ikafa na ikawa ATC inalipa kati ya dola 3,700 kwa kila mwezi hadi kufikia deni la shilingi bilioni mia mbili na milioni mia tano tisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege hii ambayo ilikodishwa na Serikali ya Tanzania ilifanya kazi muda mfupi sana hapa nchini. Hadi mwezi Juni mwaka 2009 ndege hii ilipelekwa matengenezo nje ya nchi na baadaye ikapelekwa Ufaransa. Makadirio ya matengenezo ya ndege yalifikia dola za Marekani milioni 593.6 na deni liliongezeka hadi kufikia shilingi milioni 3.039.

T A A R I F A . . .

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hajui analolifanya kwa hiyo nimemsamehe tu. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza historia na bila kuzungumza historia katika nchi hii, hatuwezi kujenga nchi, hakuna nchi isiyo na historia duniani, tunazungumzia ATC jinsi ilivyokufa, jinsi ilivyouawa na jinsi inavyofufuliwa. Kama hatujaangalia tulikotoka, tulikojikwaa, tutakwama mbele. Shirika hili huyo Mbunge haelewi kwamba tayari ATC imefunguliwa kesi nyingine London. Waziri wa Katiba na Sheria anajua, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajua, Balozi Migiro anajua, viongozi wa Serikali wanajua kwamba tuna kesi mpya imefunguliwa London mwaka huu tunadaiwa zaidi ya dola milioni 38 zaidi ya bilioni 80, anazungumza nini huyu? Anazungumza nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza ATC na tayari Serikali ya Tanzania imelipa pound elfu15 kwa malipo ya awali ya Mawakili, London. Tunazungumza ATC ambayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo alishauri mkataba usifungwe lakini ulisainiwa mkataba wa hii ndege na Kampuni ya Wallis bila kufuata taratibu. Leo watu wameenda London wamefungua kesi wanatudai kuna hatari ya Bombardier zetu zikakamatwa tena ndiyo kitu tunachokizungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza hatari ya ndege zinazonunuliwa na fedha za walipa kodi kukamatwa tena, kukamatwa kama ilivyokamatwa ile Q400 kule Canada. Tunazungumza anakwambia tujenge hoja, hizo ndiyo hoja. Tuna nia ya kujenga Taifa letu, tuna nia ya kujenga ATC mpya, lakini hatuwezi kujenga ATC mpya bila kusaidia shirika hili likaondokana na huu mzigo wa madeni ambao linao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shirika hili linadaiwa zaidi ya bilioni 100 kwa mujibu wa taarifa za Serikali yenyewe na Serikali imebeba huo mzigo wa madeni, ni vizuri, ni jambo zuri. Hata hivyo, ni lazima tuhakikishe ATC inakwenda vizuri, watendaji waliopo ATC wanapewa uwezo, wanapewa uhuru wa kuendesha ndege zao. Ni bahati wamepata Mkurugenzi mpya ambaye alikuwa Boss kule katika Mashirika ya Ndege ya Afrika, amerudi hapa amekuja kuongoza ATC alikuwa Engineer wa ATC kabla ATC haijabinafsishwa, amerudi kwa uzalendo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ina utaratibu mbaya wa kutumia watu wanaotoka nje, lazima waambiwe wasifanye mchezo huo. Wamemchukua Tido Mhando London BBC wakamleta TBC, amekaa mwaka mmoja wamemfukuza. Wamechukua mtaalam kutoka South Africa amekuja TIC amekuja hapa wamemu-harass ameondoka. Amekuja mtu Profesa Waziri wangu...

T A A R I F A . . .

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tido Muhando aliajiriwa BBC alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili labda Mheshimiwa Amina alikuwa hajui wakati huo kwamba Tido alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili. Amerudi hapa Tanzania akawa Mkuu wa TBC, ameondolewa bila mkataba wake kuelezwa. Mtu ambaye alikuja TIC ameondoka, Profesa. Kwa hiyo, ninachozungumza ni kwamba wataalam wetu wanaoletwa Tanzania ambao walikuwa wanafanya kazi nje ya nchi, wameacha kazi yenye mishahara mkubwa, wenye marupurupu mazuri, yenye usalama yakinifu, wakarudi Tanzania kuja kufanya kazi, ni lazima walindwe.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomuomba mtu aje kufanya kazi huwezi kumleta mtu halafu ukawa unambabaisha babaisha. Kwa hiyo, ili ATCL iendelee ni lazima wafanyakazi wapewe vipaumbele na Menejimenti iachiwe ifanye kazi yake bila kuingiliwa na wanasiasa. Ndege zinachelewa kwa sababu ya Wabunge sisi baadhi yetu tunachelewa Airport. Kwa hiyo, route ya ndege ya kutoka Mwanza …(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)