Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kujadili hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Kwanza, nipende kumpongeza Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Profesa

Mbarawa, niwapongeze Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Injinia Nditiye na ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema Wizara inafanya kazi yake ipasavyo japo kuna upungufu kwenye maeneo mbalimbali. Nianze na barabara ya Itoni – Ludewa – Manda. Tukumbuke kwamba barabara hii inaenda kwenye ile miradi yetu ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma na ina kilometa 211 lakini mpaka sasa inajengwa kilometa 50 na ujenzi wake unaenda kwa kusuasua sana. Kwa hiyo, niwaombe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla wake waongeze nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna barabara ya Mkiu – Madaba na Mchuchuma – Liganga. Barabara hizi sasa hivi zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri na timu yake waanze kuiweka kwenye ule mpango sasa wa kujengwa kwa lami kwa sababu inaenda kwenye ile miradi kielelezo, miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara kupitia chombo chao kinachoitwa Tanzania Road Fund. Kwa kweli, kinafanya kazi nzuri na tumejaribu kuwa tunawasiliana nao kwa kina na hivi ninavyozungumza kule kwetu Ludewa tuna vijiji 15 ambavyo havijawahi kuona gari wala baiskeli lakini Wizara imekuwa sikivu kupitia mfuko huu. Leo hii tumeshapata fedha kidogo ambapo tunaanza kufungua angalau vijiji viwili, vitatu katika kipindi kijacho kifupi. Kwa hiyo, napenda kuwapongeza lakini tuendelee kuitia moyo Wizara iwakumbuke sana watu wa kule Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara inayotoka Lupingu - Matema. Barabara hi inapita mpakani mwa nchi na ina kilometa zipatazo 139 lakini haipitiki. Ndiyo maana sasa tunasema ifike mahali eneo la mpaka ni lazima tuwe na barabara na tuiombe sasa Wizara iingize kwenye mpango ili angalau mwisho wa siku tuweze kuwahakikishia usalama, ulinzi na kuongeza utalii kwenye lile eneo. Tuna ziwa letu zuri linalopita kwenye Bonde la Ufa, kwa hiyo, kuna haja sasa ifike wakati tutengeneze barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Nditiye, kwa mara ya kwanza amefika Ludewa na amezungukia vijiji 15. Moja kati ya vijiji ni hivyo ambavyo havijawahi kupata barabara. Ziara yake imekuwa na tija, leo hii tunajengewa minara nane ya mawasiliano kupitia effectiveness ya ile ziara yake. Leo hii tunapata angalau vituo vya kupakia na kushusha abiria vipatavyo vitano kupitia ile ziara yake. Kwa hiyo, nimshukuru na ikiwezekana aendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nipende kukwambia wewe na Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Nditiye amepewa Uchifu kule kwa sababu ya ile ziara tu iliyopita. Watu wameona jitihada za Serikali hii na wameona kwamba Naibu Waziri anafanya kazi zake nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Serikali kwa ajili ya barabara ambayo tumeipata ya Makonde – Mawenji. Barabara hii ilikuwa haipitiki kabisa lakini leo hii angalau tunaona zinakuja hela kwa ajili ya kuitengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ujenzi wa meli mbili za mizigo ambapo tayari umeshakamilika katika Ziwa Nyasa na kuna ujenzi ambao sasa hivi unakaribia kwisha wa meli za abiria. Kwa hiyo, tuiombe Serikali ifanye jitihada za haraka kwa sababu wale watu wanasumbuka sana usafiri umekuwa haupo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.