Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SUZANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuwasemea Wanamwanza. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nami nitoe shukrani kwa chama changu ambacho kimeniteua kusimamia Mkoa wa Mwanza kwa sababu wamejua kwamba naweza na nitakitendea haki. Nawashukuru pia akinamama wa CHADEMA wa Mwanza kwa kuniteua mimi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuniamini na kunituma ili nishughulikie kero zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wanamwanza hasa wavuvi, wafugaji na wakulima wamenituma niwasemee yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wanathamini sana habari na taarifa ndiyo maana Wavuvi wakiwa katika uvuvi huwa wanasikiliza redio, wanakuwa na redio. Wafugaji wanapokwenda kuchunga wanakuwa na redio na wakulima vile vile na ndiyo maana kuna redio zinaitwa redio za wakulima. Wamenituma nije niseme kwamba kwa Serikali kukatiza kuonesha live Bunge ni kuwanyima haki yao ambayo inatokana na kukatwa kodi zao. Kwa hiyo, wameniambia kwamba nilisemee hilo na nimelisemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzetu wamekuwa wakiunga mkono kwa sababu wanajua ni nini wanakuja kukifanya. Wamefanya hili Bunge ni kama resting house. Wanalala, tunawaona kwenye magazeti wamesinzia na ndiyo maana wanaleta hoja ya kwamba Bunge lisioneshwe live kwa sababu wanajua adhabu itakayowapata na kuna wengine ambao adhabu hiyo imeshawapata, hawakurudi Bungeni hapa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kuwasemea wavuvi. Wavuvi wamekuwa wakinyang‟anywa nyavu zao na kuchomewa moto; lakini sitaki nionekane na-support ila swali langu ni kwamba je, hawa watu wanaouza hivi vitu na viwanda vinavyotengeneza si wanajulikana? Kwa nini Serikali inaendelea kuchukua kodi kwao na kuwanyamazia? Hii ni double standard! Ndiyo maana Mkoa wa Mwanza ulipotangazwa kwamba ni mkoa unaoongoza kwa watumishi hewa, matokeo yake Mkuu wa Mkoa alihamishwa na kupelekwa sehemu nyingine wakati yeye ndiye aliyekuwa anasimamia mkoa huu na anasimamia watumishi hao. Hilo lilikuwa ni jipu ambalo lilitakiwa kutumbuliwa mapema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uvamizi wa wavuvi na kunyang‟anya vifaa vyao vya uvuvi ambavyo wamevinunua kwa shida na kwa kujinyima. Naomba Serikali idhibiti hao wanaowanyang‟anya kwa sababu ulinzi umekuwa ukiwekwa kipindi tu ambacho sikukuu zinakaribia, lakini wanyang‟anyi hao wamekuwepo kila wakati. Kwa hiyo, naomba Serikali iimarishe ulinzi katika Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu vifaa vya uvuvi. Wavuvi wamekuwa wakiuziwa vifaa vya uvuvi kwa bei ghali sana. Kwa mfano, kama engine ya Boti imekuwa ikiuzwa shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni nne na nusu. Kwa mwananchi wa kawaida wa kipato cha chini hawezi ku-afford kununua engine ya shilingi milioni nne, kwa maana hiyo basi, tunaomba Serikali iwe inakopesha vifaa hivyo kwa wananchi wetu ambao wana kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu kilimo. Mawakala wamekuwa wakiwauzia wakulima mbegu ambazo zimeoza, ambazo hazisaidii kwa kilimo. Kwa mfano, tarehe 22 Februari, 2016, wakulima wa Pamba wa Magu walikuwa wakiilalamikia Serikali kuhusu mawakala kuwauzia mbegu ambazo zimeoza na hii ilisababisha kero kubwa sana, lakini sikuona Serikali kuchukua hatua yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inavunja nguvu wakulima wetu kwa sababu wanapotoa malalamiko kwa Serikali na Serikali kunyamaza kimya, inaonekana kama vile wamedharaulika. Tukizingatia kwamba tunaenda kuingia kwenye uchumi wa viwanda na hatuko serious na hiki kilimo, sijui hivyo viwanda tutaviendesha vipi. Naomba Serikali na Wizara iwe inasikiliza maoni ya wananchi ili tuweze kusonga mbele na tusiwavunje moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Kiwanda cha Mwatex. Kiwanda hiki kimekuwa kikifanya kazi kwa kusuasua; na hii ni kwa sababu ya tatizo la umeme. Umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara. Kwa maana hiyo basi, kama tunakwenda kuwa na uchumi wa viwanda, tunaomba kwanza tuanze na hivi viwanda vyetu ambavyo vilikuwepo vilivyokuwa vinatoa ajira kwa mama zetu, wakipeleka pamba; ilikuwa inawasaidia hata kuendesha maisha yao. Leo hii tunasema kwamba tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda huku viwanda vilivyokuwepo hamjavishughulikia. Tutakuwa kama vile tutacheza makida makida. Naiomba Serikali sasa iamue kwanza kukarabati viwanda ambavyo vilikuwepo Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumizie kuhusu ufugaji. Tanzania tuna mifugo mingi sana, lakini wafugaji wetu hawana elimu. Naomba Wizara husika itoe elimu kwa wafugaji hawa. Tunashindwa kuuza ngozi zetu katika masoko ya Kimataifa kwa sababu ngozi zetu hazina kiwango. Ng‟ombe anawekewa alama mwili mzima, sasa unapopeleka ngozi ya aina hiyo, huwezi kupata soko zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, naiomba Wizara husika itoe elimu kwa wafugaji wetu jinsi ya kutunza hizi ngozi. Kuna sehemu ya mwili wa ng‟ombe ambapo unaweza ukaweka alama na isiathiri ngozi. Kwa hiyo, waende mpaka kijijini wakatoe elimu hiyo ili tuweze kupata masoko mazuri katika masoko ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kiwanda ambacho kipo Mwanza, Ilemela, sehemu ya Saba Saba. Kile kiwanda kimekuwa godown. Sasa unashangaa yule aliyeuziwa alitoa nini kwa Serikali mpaka anashindwa kufuatiliwa? Kiwanda kimekuwa godown ya vyuma chakavu na Serikali inaangalia tu, mpaka najifikiria kwamba kulikuwa kuna nini hapo? Labda aliyeuziwa alikuwa ametoa kitu ambacho kinafanya Serikali inyamaze kimya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba viwanda hivyo vifuatiliwe kwa sababu ni aibu na ni dharau kwa Serikali. Mwekezaji anapewa kiwanda na anashindwa kukiendeleza na Serikali inanyamaza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba sisi Wasukuma sio wavuta bangi. Hapo nyuma kuna Mbunge alisema kwamba Wasukuma bangi huwa inatusaidia kupata nguvu za kwenda kulima. Mimi nimezaliwa Mwanza na ni Msukuma; ninachofahamu ni kwamba sisi huwa asubuhi tunakula ugali na maziwa, tunakwenda kulima na ndiyo maana hata miili yetu ukiiangalia unaiona imepanda; hakuna Msukuma ambaye ni legelege. Nina wasiwasi sana na huyu Mbunge inawezekana siyo Msukuma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.