Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kuwapa hongera Profesa na timu yake, Makatibu wake Wakuu, Engineer Nyamuhanga, Injinia Chamuriho na Injinia Sasabo kwa kazi nzuri. Vilevile niwape hongera Naibu wake wawili, Engineer Nditiye na Mhasibu na mbobezi ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu kwa sababu hii ni Kamati yangu, mambo mengi tumeshazungumza kwenye Kamati. Nianze na barabara ya Kidahwe – Kasulu – Nyakanazi. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri tu kwamba barabara hii ina miaka 26 tangu imefanyiwa upembuzi yakinifu na detail design, barabara haijengwi. Kwa taarifa tu ni kwamba ndiyo barabara ndefu ambayo haijawa paved for the last 26 years, ni barabara sasa ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Kabingo - Nyakanazi. Najua ziko juhudi zinazofanyika lakini quick match ndiyo tunayoitaka kuliko hii slow match.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa barabara hizi mbili za Kabingo -Nyakanazi na Kidahwe - Kasulu kwa kweli tunaomba zimekaa sana, zina miaka tisa sasa, hawa wakandarasi wanadai fedha wamalize zile barabara. Mheshimiwa Waziri haiingi akilini mkandarasi anadai shilingi bilioni 11 analipwa shilingi bilioni moja analipa diesel tu basi kazi inasimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, on a serious note nimshauri Mheshimiwa Waziri na timu yake, wafanye inventory ya barabara hizi, zile barabara ambazo zilianza na zina wakandarasi zikamilike kwanza kuliko barabara zilizoanza hazikamiliki, zinakuja barabara za katikati zinakamilika, hatuna sababu ya kuzitaja hapa kwa sababu kila mmoja anahitaji barabara. Naomba sana Mawaziri wapo hapo wafanye inventory ya barabara hizi, barabara zilizoanza zenye wakandarasi zikamilike ili tupige hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa 227 unazungumzia habari ya kitu kinachoitwa Lake Tanganyika Roads under Lake Tanganyika Transport Program. Sasa Lake Tanganyika ni mikoa mitatu tu Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Rukwa. Napenda watakapokuja kuhitimisha tujue ni barabara zipi hizi ambazo zimetengewa shilingi milioni 200 kwenye bajeti hii, ukurasa 227. Tusije tukawa tunazungumza barabara kumbe ni ya kwenda Chaguru au barabara ya Ilagala kwenda Kalya kumbe iko chini ya programu nyingine ambayo wanaita Lake Tanganyika Roads Program.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda niliseme na hili limenishangaza kidogo, nadhani wenzangu kwenye Kamati watakubaliana na mimi tulijadili sana, ujenzi wa hii reli ya standard gauge. Naona zimetengwa shilingi bilioni 100 kuanzia Isaka kwenda Rusumo, hiyo inatoka wapi? Nilidhani hoja ya sasa ingekuwa ni kuanzia Makotopora kwenda Tabora ili hatimaye reli hiyo iwe na maana ya kiuchumi uliokusudiwa. Sasa hii hoja ya kuanzia Isaka kwenda Rusumo eti kwa sababu mnajenga na Rwanda maana yake nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie vipaumbele vyetu na kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati yetu tunataka reli hii iwe na manufaa zaidi kwa Watanzania kuliko majirani. Majirani watanufaika baada ya kuwa Watanzania tumeanza kunufaika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niweke msisitizo, reli hii jina lake ni Dar es Salaam – Kigoma, ndiyo reli ya kati na ndiyo tafsiri yake. Sijui kwa nini tafsiri hii imekuwa ikipotoshwa na nashangaa sasa hiki kipande cha kutoka Isaka kwenda Rusumo wanakipa kipaumbele shilingi bilioni 100 wakati kipande cha Tabora – Dodoma bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nishukuru ujenzi wa uwanja wa ndege, jengo la abiria, nimeona shilingi bilioni mbili kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri. Napenda atakapokuja kuhitimisha hoja yake maeneo mengine ameeleza status mkandarasi amepatikana, lakini sisi imetengwa shilingi bilioni 2.3 lakini hawaelezi status ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambao naona ni jengo la abiria na maingiliano yake. Kwa hiyo, napenda atakapokuja kuhitimisha Waziri atueleze status ya ujenzi wa kiwanja hicho umefikia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni mawasiliano. Tumeshapeleka kwa Mheshimiwa Waziri orodha ya vijiji ambavyo havina minara, sasa huu mwezi wa nne. Tunataka tuone minara inajengwa, nadhani ndiyo hoja ya sasa. Hatuwezi kuzungumzia habari ya mawasiliano wakati maeneo mengine hayana mawasiliano.