Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijaalia kusimama hapa siku hii ya leo ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda moja kwa moja kwenye suala linalohusu usafiri wa anga. Usafiri wa anga kutoka Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya Songea, Mtwara kwenda Dar es Salaam. Tulikuwa tuna usafiri wa anga kwa maana ya ATCL lakini kwa masikitiko makubwa, usafiri huu umeondolewa kwa maelekezo ambayo tumepata kutoka kwenye Wizara kwamba uwanja unafanyiwa ukarabati lakini uwanja huo umetengewa karibu miezi 18 kwa ajili ya ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona hizi ni siku nyingi sana kwa ajili ya ukarabati na isitoshe usafiri huu umekuwa ukichochea uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na Mtwara kwa ujumla. Kwa hiyo, niombe huu ukarabati badala ya kufanyika kwa kipindi cha miezi 18 basi ufanyike kwa kipindi cha miezi sita ili uweze kurahisisha shughuli za wafanyabaishara na wananchi wote kwa ujumla kwenda kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii sasa niende kwenye barabara ambazo ziko ndani ya Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya wilaya mbalimbali zilizoko katika Mkoa wa Ruvuma. Kuna barabara ya Madaba – Ludewa inayounganisha Madaba na Ludewa ambayo tayari inaonekana imetengewa pesa na mwaka jana ilionekana hivyo hivyo, lakini bado utekelezaji haujaanza. Niiombe Serikali yangu iweze kufanya hima ili huduma hizi ziweze kufanyika kwa wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ambayo iko Wilaya ya Namtumbo, ya Mtwara – Pachani – Lusewa kwenda mpaka Nalasi. Ahadi hii ilikuwa ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne lakini mpaka sasa hivi naona mpango mkakati unaendelea, mchakato unaendelea bado haijaingia kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Mbarawa akaze misuli ili hii barabara iweze kutengemaa na wananchi waanze kuitumia kwa sababu inaunganisha wilaya mbili; Wilaya ya Namtumbo na Wilaya ya Tunduru ikipitia kule Nalasi, naomba atusaidie sana. Mwaka jana nilisimama hapa nilisema nitatoa shilingi na kweli nilitoa shilingi, sasa mwaka huu nitaondoka nayo kabisa niende nayo Ruvuma kama hatakuja na muafaka juu ya barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Namabengo - Mbimbi – Nalwehu yenye urefu wa kilometa 11. Naomba nayo pia iweze kuanza kutekelezwa kwa kipindi hiki cha mwaka 2018/2019. Hizi barabara zote zinapatikana katika hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ukurasa 220. Kuna barabara ya Lumecha – Kitanda – Londo – Kilosa – Kwampepo, hii barabara nimekuwa nikiimba sana, inaunganisa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro. Tunaomba sana barabara hii iunganishwe itakuwa ni shortcut na itarahisisha sana uchumi kati ya mikoa hii miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niende kwenye barabara ambayo iko katika Manispaa ya Songea, hii ni bypass, ina urefu wa kilometa 11 ambayo ilikuwa katika package ya Mtwara Corridor na inatoka katika Kata ya Sidifamu - Msamala – Ruhiko, ni kilometa 11 tu. Namwomba Mheshimiwa Mbarawa, atupie jicho hapo ili tuweze kupata ile bypass.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kumekuwa na msongamano mkubwa sana katika Halmashauri ile ya Manispaa ya Songea. Malori yanapita hapo hapo, pikipiki na magari madogo, kwa hiyo, imekuwa ni tafrani, hapakaliki, hapaeleweki. Kwa hiyo, tunaomba tupate hiyo bypass ambayo itasaidia kupumua yale magari angalau hata mjini pale pakaweza kutazamika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende Songea Vijijini kwenye barabara yenye urefu wa kilometa 32 ambayo inatoka Mletele - Matimila - Mkongo. Naomba barabara hii iweze kufanyiwa matengenezo ili iweze kurahisisha pia shughuli za wakulima waweze kusafirisha mazao yao vizuri ipasavyo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima, naunga mkono hoja.