Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, pili niwashukuru wana Nkasi Kusini kwa kunichagua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wenzangu wanaounga mkono hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo na naunga mkono pia jitihada zote zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na kuangalia utekelezaji wa bajeti iliyopita, Fungu namba 99, Mifugo na Uvuvi. Katika fungu hili Serikali ililenga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 25.9 kutoka kwenye maeneo haya kama kwenye naduhuli ya Serikali. Hadi Machi 2016 eneo la uvuvi, Serikali imekusanya zaidi ya bilioni 12 sawa na asilimia 108. Katika eneo la mifugo ilikusanya zaidi ya asilimia 70. Kwa ujumla katika fungu hili mafanikio ya maduhuli yaliyokusanywa ni zaidi ya asilimia 85.7, ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hoja yangu ni nini? Ni kwamba katika miradi ya maendeleo katika fungu hili zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 40. Kati ya hizo zaidi ya asilimia 40 ilielekezwa kwenye maendeleo ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 19.3. Kwenye utekelezaji, maendeleo ni sifuri, hakuna chochote kilichokwenda. Sasa hapa ndiyo unaweza kuona namna ambavyo sekta ya mifugo na uvuvi haikushughulikiwa kabisa kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rahisi kukusanya na wamekusanya fedha kirahisi tu, lakini katika mwaka uliopita hawajapeleka kitu chochote kuimarisha uvuvi, hawajapeleka kitu chochote kuimarisha ufugaji, trend hii ni hatari. Kwa msimamo huo, kama tutaendelea kujidai kwamba bajeti ya maendeleo ni asilimia 40 na Mheshimiwa Rais aliwatangazia wananchi kwenye sikukuu ya wafanyakazi kwamba ameweka mkazo kuhakikisha kwamba asilima 40 inaenda kwenye maendeleo, kwa utekelezaji huu hakuna kitu, tuwe na nidhamu katika utekelezaji wa bajeti. Kwa kuwa na nidhamu ya bajeti itatusaidia sana, nashauri tusiendelee na utaratibu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya kilimo, mimi Jimbo langu limegawanywa katika maeneo mawili, kanda ya juu na kanda ya ziwani. Kanda ya ziwani ina Kata nne za Kizumbi, Wampembe, Ninde na Kala, zote zinategemea uvuvi. Mpaka ninavyozungumza hivi hawajawahi kuona hata mara moja ruzuku yoyote inayoelekezwa kwenye mambo ya uvuvi, ni historia, kwa hiyo, tusiwe tunazungumza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu atanisaidia sana, nina miaka mitano hapa Bungeni na nimekuwa nikizungumza jambo hili, lakini mpaka sasa ninavyosema hakuna hata harufu ya mchango ulioelekezwa kwa wavuvi wa mwambao wa Tarafa nzima ya Jimbo langu katika Kata nne. Hakuna mialo iliyojengwa, hakuna barabara zinazotengenezwa, hakuna fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuwakopesha watu wapate vyombo vya uvuvi wa kisasa, kwa hiyo ni changamoto kubwa. Watu wanapoona pengine nguvu zinaelekezwa kwenye kilimo peke yake hawaelewi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mkoa wa Rukwa na Mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini inategemea mahindi kama zao kuu na eneo lile ni conducive kwa uzalishaji wa mahindi. Kwa maana hiyo, mahindi kwetu ni chakula na ni biashara. Usipotusaidia katika suala la mahindi katika mambo ya uzalishaji na uuzaji wake hujasaidia Kanda hiyo nzima na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napitia bajeti ya mwaka jana, nimekuta kwenye akiba yetu tulikuwa na tani 370,973.6 za akiba ya chakula kwa mahindi kabla ya kupeleka kwenye soko na kusaidia maeneo yenye njaa. Mpaka sasa ulivyotoa umebakiza stoo tani 61,315, kwa maana hiyo kuna sababu ya mwaka huu kununua mahindi ya kutosha kwa sababu maghala yako wazi sasa na mahindi yanahitajika kama unavyoona mwaka jana yalivyotumika mengi, kwa hiyo, kuna sababu ya kununua mahindi mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu nimesikia japo siyo rasmi kwamba Serikali imepanga kununua tani 100,000 hii maana yake nini? Serikali hii ndiyo inaingia madarakani, wapiga kura wengi walikuwa ni wakulima na wafugaji hawa. Unaposema unanunua tani 100,000 maana yake unawaacha wakulima ambao wanachangia population ya Tanzania kwa asilimia 70 na shughuli yao kubwa ni kilimo, wanaendesha kilimo lakini hawajui namna watakavyouza mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali isijiondoe kwenye jukumu lake la kutafuta soko la wakulima, mkifanya hivyo mtakuwa mmekosea. Tunahimiza, tunatoa mbolea za ruzuku ili watu wazalishe, sasa uzalishaji upo na Sumbawanga upo, Namanyere kwa Nkasi peke yake tutakuwa na zaidi ya tani 55,000, sasa usipozinunua hatuwezi kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu Ranchi za Taifa. Kule kwetu kuna Kalambo Ranchi, wafugaji wachache wamepewa blocks kadhaa lakini block hizo zimekuwa zinaachiwaachiwa yaani mtu akikosa uwezo anamuachia mwingine kienyeji kienyeji, kwa hiyo, inapoteza maana, naomba utaratibu mzuri uwepo kushughulikia ranchi hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Ranchi ya Kalambo inashangaza, wananchi walifukuzwa katika maeneo hayo kuanzisha ranchi ili wafuge, lakini sasa hivi wao wanakodisha ranchi hiyo kwa wakulima wakubwa. Sasa hivi kuna mkulima amelima zaidi ya ekari 1,000 na kuleta malalamiko kwa vijiji vya Nkana, Sintali, Nkomanchindo na Ntaramila kwamba kwa nini wao walifukuzwa badala yake Serikali imetafuta mwekezaji ambaye amelima ekari zaidi ya 1,000 maeneo ya ufugaji, dhana ya kufuga na kulima haieleweki sasa kwa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba kuchangia kuhusu SAGCOT. SAGCOT inalenga kuimarisha kilimo kwa maeneo ya Kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na kupeleka mbolea, kuimarisha barabara na vitu kama hivyo ili kuboresha kilimo, lakini katika bajeti hii sijaiona.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mtusaidie kuhakikisha kwamba miradi inayoanzishwa isiwe inatajwatajwa, iwe inaanza kushika kasi, SAGCOT inatamkwatamkwa hakuna kitu kinachoendelea. Maeneo ya wakulima yasipofikika, tutapataje pembejeo? Sasa hivi tunahimiza sana utumiaji wa pembejeo zinazopatika hapa nchini kama Minjingu, kwa nini tusione umuhimu wa kuboresha miundombinu ya usafiri wa maeneo haya ili kufikisha pembejeo hizo kwa maana ya mbolea za kupandia na mbegu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba mbegu zinazalishwa katika maeneo ya uzalishaji. Ipo tabia ya kutoa nje mbegu za mazao ya wakulima, kwa nini? Wakati ardhi ya kutosha tunayo na wataalam ninyi mpo na wafanyabiashara wapo. Kwa nini tusiweke utaratibu wa kuzalisha katika maeneo yetu sisi wenyewe ili kujihakikishia usalama wa mbegu na ubora wake kuliko hali ya sasa ambapo unataka mbegu kutoka Kenya na sehemu nyingine, mwisho tunapata mbegu zenye tabia ambazo hazihimili mazingira yetu.