Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa uliyonipa ya kuhitimisha hoja hii. Nianze kwa shukrani kwa Kamati zote kwa maoni, ushauri, mapendekezo waliyoyatoa. Pia nawashukuru Waheshimia Wabunge wote waliochangia idadi yao ni 45; Wabunge 30 walichangia kwa maandishi na Wabunge 15 walichangia kwa mdomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi na niseme tu kama alivyosema Naibu Waziri kwamba kama hatutayafikia yote, basi kwa ujumla kabla ya mwisho wa Bunge hili la bajeti, tutawawekea kwenye pigeon holes zenu majibu ya maswali yote mliyouliza. Hata hivyo, nizungumze mambo ya jumla ambayo yamezungumzwa na kubwa ni lile la kwanza la masuala ya biashara, vikwazo vya biashara na kwamba imetolewa kauli hapa na baadhi ya Wabunge ambayo kwa kweli sisi kama Serikali ni lazima tuielezee vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli yenyewe ni kwamba, baadhi ya wachache ni kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano haina dhamira ya kuisaidia Zanzibar kiuchumi na kwamba inabana fursa za biashara na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar sasa kauli kama hiyo haiwezi kubaki bila kutolewa maelezo na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu kwamba, kihistoria hata kabla ya mapinduzi, hata kabla ya uhuru, miaka mingi iliyopita, mahusiano kati ya bara na Zanzibar msingi wake mkubwa ulikuwa ni biashara na hata kabla Serikali hizi mbili hazijaundwa na kwa kweli Muungano umekuja kurasimisha tu mambo yaliyokuwepo tayari. Uhusiano mkubwa kabisa na mzuri kabisa wa kibiashara watu wengi wa bara ambao wamekuwepo Zanzibar miaka mingi kwa sehemu kubwa walienda kule kwa sababu ya biashara na watu wa Zanzibar wengi waliokuwa wamekaa bara kwa vizazi na vizazi sababu kubwa iliyowaleta ilikuwa ni biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fursa za biashara tunazoziongea sasa hivi ziko kwa namna mbili; kwanza, ni uwezo na urahisi wa kusafirisha bidhaa kati ya pande zote mbili, hiyo ni namna moja na ndiyo ambayo imechukua sehemu kubwa ya mjadala. Namna ya pili, ni uwezo na urahisi wa mtu yeyote kutoka upande wowote kwenda kuishi upande wowote kwa urahisi zaidi na kuanzisha biashara hiyo ni namna ya pili ambayo haikuzungumzwa sana lakini ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tunafahamu kwamba hii ya pili, uwezo wa mtu yeyote kwenda upande wowote wa Muungano kutengeneza makazi, kutengeneza maisha na kufanya biashara huu pia umekuwa msingi mkubwa wa uimara wa Muungano wetu na maingiliano yetu. Sidhani ndiyo maana haikuzungumzwa, kwa sehemu kubwa kabisa, tunapotafakari kuhusu mchango na hatua za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwezesha ukuaji wa uchumi na ustawi wa watu wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili pia ni muhimu kulitazama; je, ni rahisi zaidi kwa mtu kutoka Zanzibar kuja bara kupata mahali kuanzisha biashara na kushamiri na kusaidia nyumbani Zanzibar? Jibu ni ndiyo, ni rahisi na kwa nini ni hivyo? Ni kwa sababu ya Muungano. Kwa hiyo, huwezi kuuondoa Muungano katika ustawi wa watu wa Zanzibar unaotokana na urahisi wa watu wa Zanzibar kuja Bara na kufanya biashara na kushamiri. Kwa hiyo, hiyo ni manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili la pili na hili ni jambo jema kabisa na tunataka iendelee kuwa hivyo. Tunafurahi kuona Wazanzibar wengi zaidi wanakuja kuishi bara na kustawi na kusaidia Zanzibar na Wazanzibari walioko bara sasa hivi ni wengi zaidi kuliko Wazanzibari wote waliko Kisiwa cha Pemba. Miaka 20 au 30 ijayo, Wazanzibari kwa mwenendo tunaokwenda, Wazanzibari wanaoishi Bara wanaweza kuwa wengi kuliko Wazanzibari wote walioko Zanzibar na hilo ni jambo jema, ndiyo Muungano na tunaoutaka na ndiyo fursa na muingiliano sahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kwamba katika mazungumzo tunayozungumza hapa kuhusu ustawi wa Muungano wetu tusisahau uzuri na ukubwa wa fursa inayotokana na urahisi wa Wazanzibari kuja kufanya biashara bara. Wote tunajua kwamba katika maeneo yetu hasa ya Pwani, sisi tunaotoka Tanga, tunaotoka Dar es Salaam na kwingineko na hata katikati ya nchi yetu huwezi kwenda maduka mawili, matatu bila kukuta duka la Mzanzibari ambaye anafanya kazi na ananufaika na anasaidia Zanzibar hivyo hivyo. Kwa hiyo, kikubwa tu tunaomba kwamba wakija huku pia tujue wote ni raia wa nchi moja na pia wasaidie kwenda kujenga nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili la kwanza la urahisi wa kufanya biashara, urahisi wa kupeleka bidhaa; hakuna anayebisha kwamba kuna changamoto kabisa siwezi kusimama hapa kama Waziri mwenye dhamana ya Muungano nikasema hakuna shida yoyote kuhusu bidhaa zinazokwenda kwa pande zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafahamu kwamba kihistoria, biashara kati ya pande zote mbili haikuwa rasmi sana na baada ya sisi kuunda Serikali, kufanya Muungano na katika historia ya maendeleo ya uchumi wa nchi yetu na biashara, kumetokea hatua mbalimbali za kurasimisha uchumi na biashara na zile hatua zililazimika kuunda Taasisi mbalimbali na baadhi ya Taasisi hizo ni Taasisi za udhibiti zikiwemo TFDA, ZFDA, TBS, ZBS, sasa TRA ambayo haikuwepo mpaka mwaka 1996 ndiyo ilianzishwa TRA.

Sasa katika utendaji kazi katika hizi mamlaka na mamlaka ikishaitwa ya udhibiti wakati mwingine lile neno udhibiti linapitiliza mipaka. Inadhibiti siyo kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri bali inadhibiti hata kuhakikisha mambo yenyewe yanafanyika. Kwa hiyo, sisi tunafahamu kwamba sasa hivi tunapitia kipindi cha tunaweza kusema readjustment ya hizi mamlaka kufahamu wajibu wake na kufahamu kwamba zina wajibu wa kusaidia masuala ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa imezungumzwa hapa kwamba nilifanya ziara mahususi kule Zanzibar mwezi wa Oktoba na hili suala la biashara na vikwazo vya biashara, sisi Serikali tulianza kulifanyia kazi kabla halijazungumziwa Bungeni hapa. Nimeenda Zanzibar, mkutano wangu wa kwanza mkubwa kabisa tulikuwa na Zanzibar Chamber of Commerce ambao kulikuwa na mamlaka nyingine na Taasisi zingine pale za wafanyabiashara kama vile Zanzibar Freight Bureau, Zanzibar Exporters Association na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikutana na wafanyabiashara wanaohangaika kufanya biashara kila siku kati ya Bara na Zanzibar na wakanieleza kwa kina na kwa umahiri mkubwa jinsi biashara kati ya Bara na Zanzibar inavyofanyika na changamotozo zilizopo katika biashara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukazungumza structure ya uchumi wa Zanzibar kwamba kwa sehemu kubwa ni service oriented, utalii na biashara na structure ya uchumi wa Bara ambao kwa sehemu kubwa ni diverse; kuna madini, kuna kilimo, kuna ufugaji, kuna uvuvi na kadhalika na kwamba currency ya nchi yetu ambayo pia inasaidia wafanyabiashara wa Zanzibar kuagiza bidhaa kutoka nje, stability yake inategemea na mix kati ya hizi chumi mbili ambazo lazima ziwe interdependent, lazima ziwe zinategemeana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata ustawi wa uchumi wa Zanzibar vilevile kwa kiasi kikubwa unategemea diversity ya uchumi wa Bara kwamba sisi na hata control ya inflation ya Zanzibar inategemea stability ya currency inayotokana na diversity ya uchumi wa Bara. Kwa hiyo, haya mambo lazima yatazamwe katika upana wake na tukazungumza na wafanyabiashara kuhusu hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikafanya ziara bandari ya majahazi na mahali kwingineko, tukazungumza kuhusu ughali wa kuleta mizigo Zanzibar kutoka siyo tu Bara bali kutoka kote duniani na ni kwa namna gani tutarahisisha uagizaji wa Zanzibar wa bidhaa usiwe ni through transshipment kwa Bara kwamba mzigo unashushwa mahali kwingine ndiyo unachukuliwa na majahazi au meli ndogo kuja Zanzibar. Ni kwa kiasi gani Zanzibar inaweza kuagiza mzigo directly yenyewe moja kwa moja kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikafanya ziara TRA kwa upande wa Zanzibar, ZRB, Mamlaka ya Bahari Kuu, nikakutana na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na vijana na tukakusanya mambo yote ambayo yanawakwaza Wazanzibari kuhusu biashara na tarehe 23 Oktoba, nikakutana na Waziri wa biashara wa Zanzibar, Mheshimiwa Amina Salum Ally na jopo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nilimwomba Waziri Ummy anipe mtu wa TFDA na Waziri Mwijage anipe mtu wa TBS ili wawepo kwenye ule mkutano, tukapitia hoja moja mpaka nyingine inayosababisha watu wa Zanzibar iwe vigumu wao kufanya biashara na tukazichukua zile hoja, tukazitengenezea matrix.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 27 Oktoba, tukamuomba Mheshimiwa Makamu wa Rais atuite wote, Wizara ya Fedha Zanzibar, Wizara ya Fedha ya Muungano, Wizara ya Biashara ya Zanzibar na mamlaka zote za udhibiti mpaka TRA tukapitia hoja moja bada ya nyingine ya vikwazo vya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Biashara akaelekezwa kwamba aende na wataalam wake Zanzibar akakutane na Waziri mwenzake wapitie hoja moja baada ya nyingine na kikao hicho kikafanyika tarehe 22 Machi na matrix hapa ninayo na mambo yote yaliyoorodheshwa ikiwemo ya VAT, ikiwemo hizi Mamlaka mengine yalitatuliwa katika mchakato huu na mengine yataendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikutana na Waziri wa Fedha wa Zanzibar ambaye alieleza masuala ya biashara kwa upande wa fedha. Kwa hiyo, baada ya kueleza hizi jitihada ambazo tumefanya sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kukutana na wafanyabiashara kwa makundi na mmoja mmoja, kukutanisha sekta, mimi kukutana kama Waziri wa Muungano na Waziri wa Biashara inaniuma sana akisimama Mbunge akisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano haina dhamira ya kutatua changamoto za biashara kwa upande wa Zanzibar, kwa sababu najua kabisa kazi ambayo tumeifanya na siyo sahihi kabisa kusema hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na inawezekana hatuna uhodari sana wa kuyatangaza haya mambo ambayo tunayafanya, lakini kwa kweli tunayafanya. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge tusaidiane mawazo hapa, nini zaidi yatulichofanya kinafaa kufanywa zaidi na sisi tuko tayari. Nimesikitika kwamba wakati baadhi ya Wabunge wanaeleza shida zilizopo na hizo shida zinathibitishwa na Wabunge wengine kunakuwa na makofi ya kufurahia kwamba shida zile zimekuwa confirmed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani siyo sawa, tusifurahie kunapokuwa kwamba tume-confirm, nadhani kuzomea na kuzodoa ni rahisi zaidi kuliko kushauri, lakini kazi yetu ni kushauri na sisi tuko tayari kupokea ushauri wowote ambao utasaidia tuondoe haya mambo kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge muamini kabisa kwamba suala la biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalijua, imelishughulikia na inaendelea kulishughulikia. Nimetengeneza marafiki wengi sana wafanyabiashara wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara yangu na nimekutana nao akina Mohamed Masoud Rashid, Omar Hussein Mussa, Abdallah Abbas Omar, Wakili Awadh Ally alikuwepo kwenye mkutano na kuna baadhi ya mambo tuliyashughulikia pale pale, wale waliniambia kwamba Benki Kuu imetoa waraka kwamba minimum ya kiwango cha bureau de change ni milioni 300 na kwamba bureau de change za Zanzibar ni ndogo ndogo wanaomba tusaidie kwa upande wa Zanzibar kufanyike exception na tulifanya. Tulimpiga simu Governor Ndullu akasema ataenda. Kwa hiyo wakati mwingine haya mambo tunayafanyia kazi wakati huo huo tukiwa kwenye ziara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo alizungumza Ndugu Jamal na ningependa kujibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu terminal two, ni kweli kumekuwepo na changamoto pale ya extension kuongeza mkopo mwingine kwa ajili ya kumaliza lile jengo na limekuwa ni jambo kubwa la lawama wakati anazungumza watu wakapiga makofi kwamba ni kweli kabisa mkopo umenyimwa. Hata hivyo, nataka kusema kwamba mchakato wa kutoa mikopo kwenye Serikali una hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya hatua za mwisho mwisho kabisa, ni mkopo ule kupitishwa na Kamati ya madeni ya Taifa. Kwa hiyo, nataka niwambie Mheshimiwa Jamal na Wazanzibari, rafiki zangu, ndugu zangu wapendwa kwamba mapema mwezi huu Kamati ya madeni ya Taifa ilipitisha na kukubali Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikope dola milioni 58 zaidi kwa ajili ya kumalizia jengo lile le terminal two pale uwanja wa Ndege wa Zanzibar. Kwa hiyo, jambo hilo litakwisha, litakuwa siyo hoja tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Bandari ya Mpigeduri. Taarifa tulizonazo sisi kutoka kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha na Zanzibar na hapa barani kwamba bado kuna maelezo ya ziada ya kitaalam na kibiashara na kuchumi yanahitajika ili kuweza kujenga hoja nzuri zaidi hata kule tunakokopa pesa, lakini Serikali ya Jamhuri haina dhamira ya kunyima uwezo Zanzibar kujitengenezea Bandari yake ambayo ni mhimili wa uchumi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hapo hapo kuna mradi wa e-government, kuna mkopo, nadhani masuala haya ni muhimu yazungumzwe vizuri kwa sababu mikopo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokwenda kufanya miradi Zanzibar bado marejesho ya fedha zile yanalipwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ndiyo maana kuna ushirikishwaji mkubwa na ushirikiano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna miradi mingine ya maendeleo Zanzibar, hospitali ya Mnazi mmoja, SUZA, Barabara ya Chake-Wete hadi Gando kupitia mifuko mbalimbali kama vile Saudi Fund, Quwait Fund na BADEA, yote hiyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasaidia na inashiriki kuwezesha fedha zitoke ili kazi hiyo ifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kodi na usumbufu, tumesikia na ni kweli ni changamoto. Dada yangu Tauhida nimekusikia, nakubali na nimekuelewa, nitapanda Boti ya Azam lakini nadhani MV. Mapinduzi basi siku moja nitapanda tujionee nini kinaendelea. Hata hivyo, tumeelezewa changamoto nyingi zilizopo pale na kuna mambo mawili pale yanayojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni kweli kwamba nchi yetu sisi vituo vya forodha vipo popote ambapo unaweza kuingia kutoka nje ya nchi ikiwemo Zanzibar na tunapaswa kuwa na mfumo wa pamoja wa forodha kwamba ukiingiza bidhaa kwenye kituo cha forodha cha Zanzibar labda umechukua gari kutoka Dubai iwe sawa na umeingiza Tanga kutokea Dubai. Yote hiyo inategemea mfumo wa pamoja wa uthamini wa kodi. Sasa tumesimika mfumo wa pamoja wa kuthamini kodi lakini hatujaanza kuutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfumo mpya unaitwa TANSIS ambao ndiyo una database ya thamani ya bidhaa zote duniani ili kodi iweze kuthaminishwa kwa pamoja ili usilazimike kuonekana kama umelipa mara mbili, ukija Bara kumbe umelipa tofauti. Sasa ukadiriaji unaotegemea macho ya mtu, akili ya mtu moyo wake ndio unasababisha tuwe na changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo tunalijua na bahati nzuri kuna kikao tarehe 28 mwezi huu hapa na limezungumzwa sana na kuna baadhi ya mambo madogo tu ya kitaalam yamebakia ili tuwe na mfumo wa pamoja wa kuthaminisha bidhaa. Huo mfumo ukiwekwa, basi hizi shida zote zilizozungumzwa hapa zote zitakwisha, kikubwa ni hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi, kwa hiyo, nipande upande mmoja wa mfumo. Upande wa pili ni watu kwamba wakati mwingine kwenye vituo hivi vya forodha kuna watu wakorofi tu ambao kazi yao ni ku-harass watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona kabisa kwamba huyu mama ametoka Zanzibar, amefungasha khanga na kuna watu wa kutoka kule Makunduchi anakotoka Mheshimiwa Wanu, wakienda kuoa, basi wanabeba masanduku na masanduku ya khanga, kuna jina lao wanatumia, nimelisahau. Wakifika pale, unaona kabisa akinamama wa watu wamepaka hina, unaona wanaenda harusini, unaona wako kundi na wanakuelezea, lakini mtu hataki kukubali. Sasa inawezekana mtu akili hana, lakini hata macho ya kuona hana, kuona kwamba hapa hili jambo ni la wazi kabisa kwamba hawa watu ni mizigo binafsi na wala siyo biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili tumezungumza na wenzetu wa mamlaka ili tuwe tunaambiana. Kama kuna wafanyakazi wakorofi ambao wanawasumbua watu, basi watupe majina ili waweze kubadilishwa kwenye vituo hivyo. Mchango wa watu binafsi kwenye kuharibu mambo upo na ni mkubwa. Kwa hiyo, tunaweza tukaja hapa tukalalamika sana kumbe ni mtu tu utashi wake kwenye kusumbua watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine ni mambo makubwa sana yanatokea. Nitatoa mfano wa jambo moja ambalo tumelishughulikia ambao ulikuwa ni uamuzi wa mtu mmoja tu. Zanzibar inapata watalii wengi kutoka Italia, nadhani nusu ya watalii wa Zanzibar wanatoka Italy. Siku moja Afisa mmoja wa Ubalozi wetu kule Roma akaamua kuandika kwa Travel Agency wote Italy kwamba kuanzia mwezi wa Kwanza tarehe moja ukitaka kwenda Zanzibar visa huipati kule, lazima uje Ubalozini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu Italy wanatoka miji mbalimbali; wengine wanatoka Nepals, wengine Frolence, wengine wapi; kwa hiyo, ukiwaambia kwamba walazimike kwenda Roma, maana yake utafanya usumbufu na kupunguza watalii Zanzibar. Sasa ilipokuja ile habari, wote sisi, Waziri wa Muungano ndio unaaambiwa, namtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye anahusika na masuala ya Uhamiaji, kumwuliza, hana habari. Waziri wa Mambo ya Nje mwenye Ubalozi, hana habari, kwamba jambo kubwa kama hili limeamuliwa lakini hana habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe ulikuwa ni uamuzi wa mtu mmoja. Sasa wenzetu Wazanzibari, baadhi walivyolipata wakajua tayari ni siasa hapa, tunaminywa, wanataka kutuua, wanataka kutumaliza, utalii ndiyo uchumi wetu, hawatupendi. Ikawa jambo kubwa! Kumbe kuuliza, hamna mtu yeyote mkubwa wa Serikali anayelijua. Ni Afisa mmoja tu. Kwa hiyo, tukalazimika kubadilisha ule uamuzi ili utaratibu ule wa zamani wa kupata visa on arrival uendelee pale pale; na unaendelea mpaka sasa hivi. Hatukutangaza kujitutumua kwamba tumesaidia, kwa sababu ni mambo ya kila siku ya kawaida ya utendaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kuna kikao kikubwa kinakuja cha tarehe 28 mwezi wa Nne, baadhi ya mambo ambayo Waheshimiwa Mbunge wameyazungumza; mambo ya VAT na mifumo ya kodi yatazungumzwa na kumalizwa na Mawaziri wa Fedha pamoja na wataalam wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kombo amezungumza kwamba uchumi wa Zanzibar unakufa, uchumi unasimama, mfumo mbovu. Sasa nadhani tueleze, maana nimemsikiliza kwa makini sana na nilichokisikia ni lawama, nikawa na kalamu yangu nangoja aniambie nini sasa tufanye ili tuweze kufanikiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usajili wa meli, ni jambo ambalo wote tunalijua na kuna hoja hapa kwamba Zanzibar sasa inanyang’anywa usajili wa meli. Bahati nzuri nimeshughulika nalo hili mwenyewe binafsi. Ambacho kinataka kufanywa ni kwamba zoezi la usajili wa meli liwe
shirikishi. Tufahamu kwamba hizi meli zinabeba bendera ya Tanzania ya nchi yetu. Wote tunajua meli kadhaa zimekamatwa na mihadarati, nyingine zinabeba silaha, nyingine zinatia nanga katika bandari zilizozuiwa, nyingine zinakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imeitwa na kuaibishwa mara nyingi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tumetishiwa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi kama nchi. Wasiwasi wetu mkubwa ni kwamba hizi meli zimekutwa na silaha na mihadarati, Mungu epusha siku ingekutwa na watu (human trafficking) ndiyo ingekuwa shida kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wote tunajua kwamba Mamlaka ya Kusajili Meli za Nje ni mamlaka ya nchi, lakini huko nyuma kulikuwa na makubaliano kwamba Zanzibar itafanya kwa niaba ya Tanzania na itabaki na hayo mapato, kabisa. Hili ni jambo ambalo wengi hawajui. Iliamuliwa kwamba Zanzibar ifanye kwa niaba yetu wote na ibaki na mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukatokea utaratibu pale kwamba wamemtafuta Agent Dubai, ndio ana muhuri wa Tanzania. Fikiria nchi kubwa ya Tanzania, mtu pale Dubai ana kaofisi, ndio anawakabidhi watu bendera ya Tanzania. Hatumjui ni nani? Sasa kilichofanyika na bahati nzuri mimi nilishiriki, tumesema, sawa, sahihi iendelee kuwa ya Waziri wa Zanzibar, lakini vyombo vya usalama vishiriki, meli zinazoomba bendera ya Tanzania tuzijue zinatoka nchi gani? Zinataka kufanya shughuli gani ili tulinde sifa na heshima ya nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu yangu akija kusema hapa kwamba tumewanyang’anya na nini, nadhani hatutendei haki na anatulaumu bila haki kabisa kwa kweli. Tunachotaka kufanya ni jambo zuri kabisa ambalo siyo litaisaidia tu Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hata Zanzibar yenyewe itaisaidia. Kwa sababu tungenyang’anywa huu usajili kama nchi kutokana na makosa ya hizo meli, hata Zanzibar haya mapato yasingekuwepo. Kwa hiyo, hili linafanyika kwa nia njema na kwa ajili ya manufaa ya watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Pondeza namshukuru kwa pongezi. Ni kweli kuna changamoto kwenye kiwango cha deni la umeme na wote tunajua masuala ya VAT, tunajua calculations zinazotokana na uwekezaji wa miundombinu na jambo hili bahati nzuri Wizara zinakaa na zinaendelea kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la usajili wa vyombo vya moto, bahati nzuri AG yupo hapa. Suala lile limeshughulikiwa muda mrefu. Sisi tunataka gari yoyote ikisajiliwa Zanzibar iwe sawa na imesajiliwa Bara na ikisajiliwa Bara iwe sawa na imesajiliwa Zanzibar. Nasi Ofisi ya Makamu wa Rais, jambo hili tulilisukuma sana na mimi binafsi kwa nguvu zangu zote na Mawaziri wahusika wanajua; na viongozi wetu Wakuu, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wametuunga mkono. Tulifikisha jambo hilo mpaka kwenye vikao muhimu vya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri jambo hili lina dimensions za masuala ya kodi na hicho kipengele kimeenda kutazamwa. Imani yetu ni kwamba katika mabadiliko ya sheria mchanganyiko, miscellaneous amendment ni kwamba jambo hili litaingizwa ili tuweze kubadillisha hizi sheria ili magari yaruhusiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nami nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge, ni aibu kwa gari ya Zambia kutembea kwa urahisi Tanzania kuliko gari ya Zanzibar. Hilo jambo hamna anayeona aibu kulisema, hata sisi tunaona ni aibu vilevile. Tutalirekebisha, kwa sababu Serikali imeonesha utayari na lilishaingia hadi kwenye vikao vikubwa vya Serikali na lilipitishwa huko nyuma muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vikao, tangu kwenye mchango wa hotuba ya Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanazungumza kwamba mnakaa vikao, kero haziishi. Labda Waheshimiwa Wajumbe watupe njia mbadala ya kuzungumza zaidi ya vikao, kwa sababu vikao ndiyo mahali pakubwa ambapo tunaweza kuzungumza na kufanya maamuzi na yakafuatiliwa utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alizungumza katika kuhitimisha hotuba yake kwamba kikao kikubwa ni kile cha Kamati ya pamoja chini ya Mheshimiwa Makamu wa Rais na maamuzi ya kila kikao ni maamuzi ya kiserikali yenye nguvu ya kiserikali na sisi kazi yetu ni kuyafuatilia na kuhakikisha kwamba yanatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata mchango wa Mheshimiwa Machano na tunapokea mapendekezo na ushauri aliotupa kuhusu fursa za utalii na kwenye simu na kuhusu vyombo vya moto, nimelizungumzia. Malipo ya ujenzi wa Ofisi, hili limewekwa kwenye bajeti kwa sababu ni deni na litaendelea kulipwa. Ahadi za viongozi, tutazifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale awali, kwamba yale ambayo hatujayazungumza, tutayajibu kwa maandishi; yapo mambo ya mifuko ya plastick kwenye masuala ya mazingira. Dhamira yetu ya kuzuia kabisa mifuko ya plastick ipo pale pale na tutalitekeleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwisho kabisa kwa kusema kwamba mwaka 1965, mwaka mmoja baada ya kuwa na Muungano wetu, kulikuwa na Mkutano wa Pamoja wa TANU na ASP wa kupendekeza Mgombea Urais wa Muungano. Kwenye ule Mkutano Mheshimiwa Karume alimpendekeza Mwalimu Nyerere kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule Mkutano, Mwalimu Nyerere aliuhadithia ule mkutano na hadithi hiyo aliirudia mara nyingi jinsi Muungano huu ulivyokuja. Aliwaambia Wajumbe na Mzee Karume akiwepo kwamba Shehe Karume, ninyi Wazanzibari mkiwa tayari kuungana, Wabara nasi tutakuwa tayari. Marehemu Mzee Karume akajibu, wewe unazungumzia utayari wa nini? Hii habari ya kuwa tayari ya nini? Sisi tuko tayari. Ita Waandishi wa Habari sasa hivi, tutangaze sisi ni nchi moja, wewe Rais. Mwalimu akasema, hapana, mambo haya yanahitaji sheria, na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nazungumza hili tujue kwamba urithi wa Muungano wetu chanzo chake ni nini? Dhamira ya Muungano wetu ilitokana na nini? Ilitokana na nyoyo, dira na maono ya viongozi wetu Wakuu, Waasisi wa Taifa hili kwamba tumetawaliwa na tukaleta mapinduzi na tukaleta Uhuru. Tunao uwezo kabisa wa kutengeneza mipaka mipya ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi Watanzania hatujui thamani tuliyonayo duniani kwamba ni nchi pekee iliyotengeneza mipaka mipya kama nchi, tunachukulia hili jambo la mzaha tu. Tumetengeneza mipaka mipya na Taifa jipya kwa utashi wetu. Sasa hii habari ya kwamba mkopo umechelewa, hiki kimechelewa, naomba sana tusiweke doa kwenye jambo hili kubwa katika changamoto ambazo kabisa tuna uwezo wa kuzimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kwamba mtu unaoitwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na unapata manufaa kutokana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, halafu unakuja unaupaka masizi Muungano ambao wote sisi ni warithi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, imani yangu kwamba tutapitisha bajeti hii ili baada ya hapa tuendelee kufanya kazi kwa pamoja kuimarisha Muungano wetu, nchi yetu hii iendelee kupata sifa kubwa iliyonayo duniani. Kama nilivyosema asubuhi kwenye hotuba yetu ni kwamba sisi sote tutaondoka hapa duniani, lakini legacy yetu kubwa ni kuondoka Muungano huu ukiwa imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wote, wana CCM wenzangu ambao sote tunasema kwamba tunataka kumsaidia Mheshimiwa Rais, namna kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba anamaliza wakati wake Muungano huu ukiwepo na ukiwa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.