Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ussi Salum Pondeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chumbuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijalia afya njema, lakini la pili nataka nizungumzie zaidi hii Wizara yetu ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mambo ambayo humu kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa kuna Kamati ile ya SMT inayashughulikia, lakini muda mrefu umepita na kila siku tunapata majibu ya kuwa kero hizi zinashughulikiwa. Nataka nijielekeze sehemu moja tu katika huduma ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasemwa Zanzibar tunadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 131, lakini ukweli uliokuwepo hazifiki hata shilingi bilioni 40. Kila mwezi tumekuwa tukilipa current bill still wenzetu upande wa pili ambao ni TANESCO wamekuwa wakituwekea bill ile ile ya kutuambia tunadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 130. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, hivi juzi juzi tu tulipokuwa katika Kamati ya Nishati na Madini tuliweza kui-raise hoja hiyo, Mheshimiwa Waziri upande wa huku akawaita na watu wa Zanzibar, lakini wamekaa bila kupata muafaka wa kusema juhudi hizi zinaendelea kuchukuliwa. Ukweli uliokuwepo na ushahidi upo sisi hatudaiwi zaidi ya shilingi bilioni 133. Cha kushangaza kila mwaka imekuwa kelele Zanzibar inadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 130, Zanzibar hatulipi umeme, lakini ushahidi upo ambapo tunalipa lakini hii kero imekuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kulisema hili kwa sababu hii ni kero ambayo inawakera sana Wazanzibar kwa maana kuna baadhi ya watu hufikia stage ya kusimama humu ndani ya Bunge na kuanza kusema Wazanzibar tunawabeba tu, umeme wanatumia hawalipi, kuna baadhi ya mambo hivi na hivi wao kazi yao ni kupewa tu. Ukweli uliokuwepo hizi kero zingekuwa zinashughulikiwa kwa muda kama ilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri basi haya yote yasingekuwa yanajitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili imekuwa ni kawaida kuambiwa kila siku vinakaa vikao baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, lakini hakuna hata mara moja ambapo unakuja mrejesho kwamba watu wamekaa na wameamua hivi na kero hii imeisha na imebaki kero hii. Sisi tunaelewa kero ni sehemu ya maisha na changamoto ni sehemu ya maisha, lakini tupewe zile kero ambazo kweli zinatuhusu sisi Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofika mahali jambo tunalifanya kwa kutimiza wajibu wetu, lakini leo hii wenzetu upande wa pili wanafika mahali wakaona kama labda sisi tunasaidiwasaidiwa tu bila kuwa na nguvu yetu wenyewe kusema kweli hatuwezi kujisikia vizuri upande wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumze ni kuhusu mambo ya biashara. Kwenye ufanyaji wa biashara kuna utozaji wa kodi mara mbili. Zanzibar ukinunua mzigo Dar es Salaam let say Tanzania Cable unapeleka Zanzibar huku unalipa VAT na ukifika Zanzibar pia ulipe VAT. Hili suala linawaumiza wananchi wetu wa chini kwa sababu tunalipa VAT mara mbili maana yake tunalipa VAT asilimia 36. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili mwaka 1995 mpaka 2000 halikuwepo, kulikuwa na utaratibu baina ya Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar kubadilishana zile tax invoice kwa ajili ya kudai upande wa pili lakini unalipia VAT sehemu moja last destination. Leo hii ukitoa mzigo Zanzibar ambapo umelipia kila kitu ukifika Dar es Salaam lazima pia ulipe. Sasa hili linaonesha jinsi gani sisi upande wa pili tunapata uonevu au tusiseme uonevu tuseme labda kuna jambo ambalo halijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri katika kikao cha tarehe 28 basi hili ni jambo moja la msingi lichukuliwe kwa umuhimu wake na kwa ufasaha kabisa tupate majibu ya haraka. Kwa sababu wananchi wetu wanafika mahali wanaudharau Muungano wanasema una faida gani maana mtu akinunua tv Dar es Salaam akienda nayo Arusha halipi kodi lakini ukichukua tv Dar es Salaam ukienda nacho Zanzibar inabidi uilipie tena kodi. Hivi ni vitu ambavyo vinaturudisha nyuma sisi kama Wazanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba kuna mambo ambayo yana faida ya Muungano lakini hayaelezwi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya Muungano ambayo na sisi tunakiri inatusaidia kama MIVARP, tumepata masoko, barabara zimejengwa zote zile ni faida ya Muungano, lakini wananchi wa chini hawana habari kama hivi vitu vinatoka kwenye Serikali ya Muungano. Wanafika mahali wanakwambia kwa style hii sisi Muungano hatuuoni faida yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mzanzibari namba moja nakubali Muungano huu ni mzuri isipokuwa unahitaji kurekebishwa na kero hizi ndogo ndogo ndizo ambazo zinazaa haya mengine yote ya kusema tuna kero na kuona Muungano hauna faida lakini kiukweli una faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri January Makamba kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Kuna baadhi ya mambo mengi ambayo ameyatatua yeye kwa kipindi chake ambayo yalikuwa ni kero kubwa ambazo sisi tunazifahamu.

Tunampongeza sana na tunataka tu kumwambia kwamba, aendeleze juhudi zake kutoka hapa alipofika na haya mengine inshallah Mwenyezi Mungu atamjalia ayamalize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliseme ni kuhusu kodi ya magari. Ukitoa gari Zanzibar lina namba ya ZNZ ukifika nalo Dar es Salaam unazuiwa lakini ukitoa gari Tanzania Bara ina namba za STK, TZD zote zinaenda Zanzibar na zinatumika. Magari yetu Zanzibar yakija Tanzania Bara wanaya-treat kama magari ya nje kitu ambacho siyo cha maana kweli kweli na hii yote ni nchi moja. Unapokuja hapa ukisema nchi yetu ni ya Muungano lakini magari ya Tanzania Bara yakija Zanzibar …

T A A R I F A . . .

MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naipokea taarifa hiyo kwa sababu ndiyo kitu nilichokuwa nakisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la ushuru hizi ni zile kero ndogo ndogo ninazomwambia Mheshimiwa Waziri January Makamba azitazame. Zile kero ambazo zinatukabili ambazo zinatakiwa kuuweka sawa huu Muungano wetu basi ni kama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sioni sababu kwa nini gari ikitoka Zanzibar inakuwa treated kama gari ya kutoka nje, lakini gari ya Kenya au Uganda ikifika hapa inapewa kibali na mtu anatumia mpaka anamaliza shida zake. Kwa nini sisi Zanzibar na sisi tusiwe hivyo na hii ni nchi moja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafika mahali tunajiuliza aah au sisi huku tumeegemeaegemea tu, tunabebwabebwa, lakini sisi tuna haki zetu na tumesimama kwa miguu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo Mheshimiwa Waziri nakuomba unapokuja kuhitimisha basi moja ya mambo ambayo tunataka utupe ufafanuzi Wazanzibar ni kuhusu magari na mizigo yao inavyokuja na kwenda jinsi gani VAT inachukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.