Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii.

Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri wanazozifanya lakini pongezi za pekee zimuendee Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia kwa juhudi kubwa sana anazozifanya katika kuifanya Tanzania kuwa ya kijani. Kwa hiyo, tuendelee kumuunga mkono, tunamuona katika upandaji wa miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi hizi za mama yetu naona kama vile zinakinzana, yeye anasema tupande miti na miti inapandwa, lakini kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira, wengine wanaendelea kukata miti. Nitolee mfano kwenye Mkoa wangu wa Morogoro katika Halmashauri ya Morogoro, ile Milima ya Uluguru ndiyo chanzo kikubwa sana cha maji, lakini ukiangalia kwenye ile milima ambapo kulikuwa hakuna shughuli ya kibinadamu inafanyika lakini sasa hivi kuna ujenzi holela. Ukiangalia milima ile ya Bigwa, Kigurunyembe kuelekea Pangawe, ujenzi unaendelea tena wa nyumba za nguvu, nani anatoa vibali na hawa watu wanachukuliwa hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Morogoro leo tunakunywa maji ya chumvi? Kwa kweli, haikubaliki. Kwa hiyo, tunaomba juhudi hizi za Serikali ziungwe mkono mpaka huku kwenye halmashauri zetu maana ndiyo kwenye watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu kingine niseme uharibifu wa mazingira unasababishwa pia na shughuli za kiuchumi na maendeleo ya binadamu. Hatuwezi tukazuia maendeleo, lakini tunatakiwa tuwe na sustainable development. Kwa hiyo, kila aina ya maendeleo inayofanywa basi lazima tuhakikishe maendeleo haya yanakuwa rafiki kwa mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza kuhusu suala la Stiglers’ Gorge, hii haikwepeki, tunajua matatizo ya umeme ambayo tunapata katika nchi yetu na tunasema Tanzania ya viwanda lazima tuwe na umeme ambao ni sustainable. Ombi langu ni kwamba ile tathmini iliyofanywa (environmental impact assessment) vile vitu vizingatiwe ili isije ikaleta madhara, lakini mradi una umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nizungumzie uchafuzi wa mazingira ambao umekithiri na sasa hivi unatuletea madhara makubwa sana nchini. Tumeona mafuriko Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Arusha, kila sehemu, lakini tatizo kubwa hapa ninaloliona mojawapo ni taka ngumu hizi ambazo ni product za plastic bags pamoja na chupa. Kama Serikali tulifanya mkakati wa makusudi kuweza ku-ban viroba ambavyo pia vilichangia kuharibu mazingira lakini hata afya za watu, kwa nini tusifanye mkakati huo huo katika ku-ban uzalishaji wa plastic na matumizi haya ya plastic kwa sababu inaleta madhara makubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapata hasara, hivi ukiangalia kodi inayopata kwa vile viwanda na gharama inazopata ambapo wananchi wanapata hasara ya mali zao, magonjwa, miundombinu, hivi tukifanya cost benefit analysis, kweli hii plastic ina tija katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie kizazi cha leo na cha kesho kwa sababu inatengeneza pollution. Sasa hivi mito mingi Dar es Salaam huwezi ukanywa maji, inakuwa depleted. Maji hayatumiki, ardhi itafika mahali haitumiki, hewa yetu itakuwa haitumiki, sasa kitu kisipotumika maana yake kinakuwa depleted. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mazingira Mheshimiwa Waziri, pamoja na mikakati hii utekelezaji sasa ndiyo unaotakiwa kwa sababu, madhara, vyanzo, tumeshavijua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu kingine niseme kuhusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.