Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliyenipa zawadi ya uhai na ametujaalia sisi sote kujumuika hapa leo na kuweza kujadili mambo yaliyo mbele yetu kwa maslahi ya nchi yetu. Vilevile namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjaalia afya njema Mheshimiwa Spika wetu kwa kumuwezesha kurudi salama. Tunamshukuru Mungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Mawaziri wote na Naibu Mawaziri wote, Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Serikali bila kusahau Wakuu wa Mikoa ambao wote kwa pamoja wamefanya kazi njema ambayo matunda yameonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Jaffo, Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake kwa kazi nzuri wanayoitekeleza. Tumewaona mara kwa mara wakikimbia huku na huku, na mara nyingine wamepata ajali njiani, kwa kweli tunampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nichukue fura hii kumshukuru na kumpongeza Waziri husika wa TAMISEMI ambaye ni Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kipindi hiki cha miaka miwili na nusu. Amefanya mambo mengi makubwa ambayo yamewashangaza Watanzania ambao wengi walikuwa wanabeza na wengi tukikumbuka walikuwa wanambeza sana Rais wetu wa Awamu ya Nne kwa kutokuchukua maamuzi mengine ingawa yeye pia ndiye aliyeweka mfumo mzuri, lakini pia yeye ndiye aliyetuchagulia Rais Magufuli. Yeye na wenzake walikuwa makini; akamchagua Mheshimiwa Magufuli ambaye leo amekuwa Rais wetu wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yamefanyika katika nchi hii. Kwanza wananchi wengi katika nchi hii wamebadilika kifikra na kimtazamo. Kumekuwa na miradi mikubwa ambayo imetekelezwa kwa kiwango kikubwa sana na mingine pia inaendelea kutekelezwa chini ya uongozi wa Rais wetu. Pia kumekuwa na mabadiliko ya kiutendaji kwa watumishi wa Serikali na taasisi za umma. Nidhamu ya kazi kwa watumishi na huduma nzuri zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje mambo machache tu ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miaka miwili na nusu.

Moja, kumekuwa na nidhamu kazini kwa watumishi wa umma na uwajibikaji; pili, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na udhibiti wa uingizaji wa dawa za kulevya. Mapambano dhidi ya ufisadi na uhujumu uchumi, udhibiti wa mapato ya Serikali na matumizi yake; mapato ya Serikali yameongezeka, kudhibiti rasilimali za taifa kama madini na kadhalika, ununuzi wa ndege sita na tatu zimeshawasili hapa nchini na wengi tumehudumiwa na wanaobeza na wao wanapanda hizo ndege.

Pia huduma ya maji imeboreshwa mijini na vijijini, sisi watu wa Dar es Salaam ni maajabu maana tulikuwa tunalalamika, lakini siku hizi changamoto sasa ni maji kupasuka huko mitaani, maji yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda vya madawa nchini na viwanda vingineā€¦

T A A R I F A . . .

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa kwa sababu kwa asilimia kubwa maji yameboreshwa. Kuna maeneo ya Kimbiji na Chanyika ambayo yanategemea mradi unaotoka kule Kigamboni, lakini kwa asilimia 70 maji Dar es Salaam yanapatikana (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za afya zimeboreshwa, lakini kumbuka Roma haijajengwa kwa siku moja. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda vya dawa kama nilivyosema, mradi wa umeme wa Rufiji (Stieglers Gorge) unaendelea, ulinzi na usalama umeimarishwa nchini, mauaji ya Kibiti yamekomeshwa. Amekaribisha wafanyakazi kushirikiana na Serikali kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuleta tija kwa Tanzania. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma sana, muda mfupi mambo mengi yamefanyika. Hiyo sipokei kwa sababu naangalia data.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zimejengwa, madaraja, flyover mmeziona Dar es Salaam, mji unabadilika unakuwa wa kisasa, mradi wa mabasi awamu ya pili, tatu unaendelea; ujenzi wa kiwanja cha michezo Dodoma unazinduliwa na kadhalika Ni mengi, ngoja niishie hapo maana itauma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote yaliyofanyika hapa nchini ambayo yanastahili pongezi, na dunia imeshangaa, mwenye macho haambiwi tazama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinapaswa kutiliwa mkazo au kufanyiwa kazi. Katika nchi zilizoendelea kiuchumi duniani ikiwemo nchi ya Marekani, suala la ulinzi limetiliwa mkazo na limetiliwa kipaumbele kuliko sekta nyingine kwa sababu jinsi uchumi unavyokua ndivyo uhalifu pia unavyokua. Kwa sababu hiyo hata nchi yetu ya Tanzania uchumi unakua lakini na mbinu mbalimbali za kihalifu nazo zinakua. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iongeze bajeti ya kutosha kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili ziweze kukidhi mahitaji ya vikosi vyetu au kwa vyombo vyetu vya usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto mbalimbali kama makazi ya askari, magari, mafuta na vifaa mbalimbali. Mafunzo ya ndani na nje ya nchi, kwa hiyo naiomba Serikali yangu itilie maanani katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kidogo niongelee Jeshi la Zimamoto. Tunaposema uchumi wa viwanda ujue viwanda ni rafiki wa moto kwa hiyo tunaomba pia bajeti katika eneo hilo iongezwe bila kusahau Jeshi la Zimamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema elimu bure ujenzi wa shule mbalimbali, umeme vijijini, ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji (Stieglers Gorge) na kadhalika, bila usalama haya yote hayawezi kutekelezwa. Kwa hiyo naiomba Serikali itilie maanani katika masuala ya ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea habari ya hospitali na naomba niipongeze Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya, pamoja na kwamba pongezi ambazo nilishazitoa hapo nyuma. Katika Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI), Kitengo cha Mifupa (MOI), Kitengo cha Dharura na Kitengo cha Akina Mama (Wodi ya Wazazi;) naomba fedha zipelekwe kwa wakati ili ziweze kukidhi na kuzuia maafa zaidi ambayo yanaweza kutokea katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na ukaguzi wa maeneo wakati wa kufanya usafi siku za Jumamosi kwa sababu siku hiyo akina mama wengi katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao wanafanya biashara ya kuuza maandazi na vitafunwa, chapati na kadhalika, muda wao wa kufanya biashara ni asubuhi mpaka hapo saa tatu. Sasa kule muda huo unakuwa umepigwa marufuku, hakuna kufanya biashara mpaka saa nne, na ikifika saa nne muda wa kunywa kifungua kinywa utakuwa umeshakwisha, kwa hiyo akina mama hawa wanaathirika sana.

Naomba Serikali husika, najua kero hii itakuwa si Dar es Salaam tu, hata mikoa mingine, iangalie eneo hili ili kuinusuru hali ya akina mama ambao wamekopeshana hela ndogo ndogo kutoka kwenye VICOBA vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba Serikali iongeze vyuo vingi vya ufundi ili kuwaweka vijana wetu tayari kwa ajili ya kuajiriwa katika maeneo ya viwanda. Bila kuwatayarisha vijana kutakuwa na changamoto kubwa katika kupata sifa ya kuajiriwa katika viwanda. Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.