Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, maana ninyi wote ni mashahidi, nimetembelea magongo hapa karibu miezi sita; lakini kwa vile Mheshimiwa Rais aliona kwamba afya yangu inatakiwa iimarike ili niweze kuwatumikia vyema wananchi wa Jimbo langu la Kigoma Kusini, akanipa kibali cha kwenda tena kupata matibabu nje ya nchi na hatimaye leo namshukuru Mwenyezi Mungu naweza kutembea bila kutumia magongo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nishukuru hivi kwa sababu mambo yalikuwa mengi, wako waliofikiri sasa nitakufa na Jimbo litabaki wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anayepanga maradhi ni Mwenyezi Mungu. Unaweza ukamwona leo huyu ni wa kufa kesho na asife na wewe ambaye ni mzima ukafa ukamwacha yule mgonjwa anaendelea kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba pia nimshukuru Mheshimiwa Rais, juzi wote tumeona kupitia Mfuko wa Falme za Kiarabu Mfuko wa Abu Dhabi tumepata karibu shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 51.1 kutoka Uvinza mpaka Malagarasi. Barabara hii siyo tu itakuwa ni faida kwa wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini bali pia itakuwa faida kwa Tanzania nzima kwa sababu malori yanayosafiri kuleta bidhaa kwenda Kongo na Burundi yanatumia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa haraka haraka pia nichangie kuhusu elimu ya msingi na sekondari. Tumepokea shilingi milioni 144 nashukuru sana Wizara ya TAMISEMI kwa kutupatia pesa hizo ambazo zitatusaidia kumalizia majengo yanayojengwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa sana wa Walimu. Sisi kwenye mgao tumepokea Walimu 32. Walimu 20 wanaume na Walimu 12 wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo lile ni kubwa, Halmashauri ile ni kubwa sana, ina mita za mraba 10,178 zaidi ya Mkoa wa Kilimanjaro. Mnapofanya mgao kwa Walimu, naiomba Serikali iangalie Halmashauri ya Uvinza tofauti na Halmashauri nyingine, kwa sababu jiografia ni mbaya, kuna barabara ambazo hazipitiki. Kwa mfano, sasa hivi tuna mvua nyingi, Walimu hata wanapokuwa na mahitaji muhimu hawawezi kusafiri mpaka msimu huu wa mvua uishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo majengo ya maabara kwa muda mrefu yamesimama kwa ukosefu wa pesa. Kwa hiyo, naomba Wizara husika ituangalie kwa jicho la huruma ili tusirudishe nyuma jitihada za wananchi wetu wa Jimbo la Kigoma Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya afya. Naishukuru sana Serikali kwa bajeti hii, tumetengewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya uanzishwaji wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Kwa niaba ya wananchi wangu, natoa shukrani za dhati, lakini tunatambua hivi karibuni Serikali mmetuambia mtatuletea ramani ya ujenzi wa hospitali. Tunaomba mharakishe ili basi ujenzi huo tuweze kuuanza mara moja baada ya kupitisha bajeti hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina vituo viwili vya afya; Kituo cha Kalya na Buhingu. Leo kumeulizwa swali hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI akajibu kwamba tulete barua ili waweze kutupatia Madaktari. Sisi tumepeleka barua tangu bajeti ya mwaka 2017/2018 kwamba tuna upungufu mkubwa wa Watumishi Idara ya Afya na Idara ya Elimu Msingi na Sekondari. Cha kusikitisha, mpaka leo hatuna Daktari kwenye Kituo cha Afya cha Buhingu, hatuna Daktari kwenye cha Kalya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI leo hii naomba, naona anatembelea halmashauri mbalimbali, namkaribisha Halmashauri ya Uvinza. Aje atufungulie rasmi Kituo chetu cha Afya cha Kalya ili yeye mwenyewe ajionee kilometa 250 wananchi wanatembea kutoka Kalya mpaka Kigoma Mjini. Hali ni mbaya kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeona juzi, kwanza tumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Utumishi kwa kutupa ufafanuzi kwa wale Watendaji wa Vijiji na Watumishi ambao wamewekwa pembeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali hivi mnavyovitoa, mnatupa vibali kuajiri Watendaji wa Vijiji watano au sita au kumi, wakati tuna upungufu karibu wa Watendaji wa Vijiji 30. Tunaomba Wizara ya Utumishi iliangalie hilo tupate vibali ili tuweze kuajiri Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata na watumishi wa kada nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naishauri Serikali. Watendaji wa Vijiji wapo waliofanya kazi zaidi ya miaka 20 mpaka 30, leo wamewasimamisha kazi. Kule vijijini wanaojua mazingira ya vijiji ni wale wananchi husika wa maeneo husika. Tunapotangaza ajira, wanakuja watu wa kutoka Kagera, Mwanza na kadhalika. Mazingira ya kule ni mabovu, badala yake wanaingia kwenye masuala ya rushwa na hawafanyi kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wawaangalie sana wale Watendaji ambao wamefanya kazi zaidi ya miaka 20 ili wamalizie kazi na hatimaye waweze kustaafu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mfuko wa
TARURA. Ni jambo jema…

TAARIFA . . .

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipokea lakini nilikuwa naliangalia kwa mapana zaidi na nilishashukuru kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusiana na barabara. Jimbo langu hali ya barabara ni mbaya sana. Kwenye bajeti ya mwaka huu tumetengewa shilingi milioni
400. Hivi shilingi milioni 400 tunafanya kazi gani katika mtandao wa barabara wa Halmashauri ya Uvinza? Naomba TARURA waongezewe pesa ili tuweze kujenga barabara zetu za Jimbo la Kigoma Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona vile vile kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri amezungumizia namna ambavyo tunaendeleza miji kwa maana ya miji 161 iko kwenye hatua mbalimbali ya kufanywa iwe miji midogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Nguruka kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo, takribani sasa miaka 10 tumeomba mamlaka ya Nguruka iwe Mamlaka ya Mji Mdogo lakini hadi leo utekelezaji unakuwa mgumu kwa sababu Kata ya Nguruka ina vijiji viwili, Kata ya Itebula ina vijiji viwili,
tunawezaje kuunda Mamlaka ya Mji Mdogo wakati kuna wakazi zaidi ya 50,000 kwenye eneo moja? Naiomba sana TAMISEMI iliangalie hili jambo ili ituruhusu tuweze kuongeza kata na vijiji ili Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nguruka uweze kuundwa na hatimaye shughuli za wananchi ziweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nimalizie tu kwa kusema, naishukuru sana Serikali kwa mambo mbalimbali hususan miradi ya maji. Miradi ya maji ya Nguruka, Uvinza, Ilaghala, Kalya na Kandaga inaenda vizuri, watu wanakunywa maji. Mradi wa maji wa Rukoma ndiyo utekelezaji haujulikani, sasa ni zaidi ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.