Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangie katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa heshima ya pekee ningeomba sana kwa idhini yako Wabunge wote tugonge meza zetu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni mambo mengi ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo ndivyo basi, naanza kabisa kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja ili hata kama nikisahau niwe nishamemaliza kabisa katika suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya msingi ambayo yamezunguzwa sana katika hotuba hii kwa upande wa nishati ni mambo matatu. Pamoja na mambo mengine napenda sana nijielekeze zaidi katika hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vyazo vya kuzalisha umeme kwa upande wa gesi na suala la maji limetajwa kwa kiasi kikubwa. Napenda kuliondoa wasiwasi Bunge lako Tukufu kwamba vyanzo vya kuzalisha umeme kwa njia ya maji havijatajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi si kweli, Ilani imetaja vyanzo haijabainisha mradi kwa mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani yetu aya ya 43.A imeeleza vyanzo vya msingi ambavyo Serikali itajielekeza katika kuzalisha umeme wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu na vyanzo vya maji vikiwemo. Kwa hiyo, napenda sana niondoe wasiwasi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukurasa wa 81 umetaja bayana vyanzo halali, vyanzo vitakavyotupunguzia bugudha na tofauti ndogo ndogo na migogoro ya upungufu ya umeme ikiwemo vyanzo vya gesi asilia, maji, geothermal, makaa ya mawe pamoja na upepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuwaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapotaja vyanzo vya kuzalisha umeme kimsingi hatutaji mradi kwa mradi. Mradi kwa mradi utakuja katika mipango yetu ya maendeleo kisekta ambayo tutakuja kuiwasilisha itakapofika wakati wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nieleze kwa nini nasema hivyo. Kwanza kabisa Serikali haijatelekeza kutumia gesi asilia. Hivi sasa Wabunge wote tunatambua tunayo trilioni 57.5 ya gesi asilia na umeme tunaotumia kwa sasa hivi zaidi ya megawatt 787 zinatokana na gesi asilia. Kwa hiyo, si kweli kwamba tumetelekeza kutumia gesi asilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais tarehe 3 Aprili, 2018 alizindua mradi mkubwa wa kuzalisha megawatt 198 ambao unakwenda kutupatia megawatt 240 mwishoni mwa Juni, 2018. Kama hiyo haitoshi Desemba, 2018 tutaanza tena kutumia nishati nyingine ya gesi asilia ya megawatt 185 kutoka kwenye mradi mwingine wa Kinyerezi II nao unatokana na gesi asilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwakani tunaanza kujenga mradi mwingine wa gesi asilia kutoka Somanga Fungu wa megawatt 330, nao unatokana na gesi asilia. Mwaka huo huo Julai tutaanza kujenga mradi mwingine wa megawatt 300 unaotokana na gesi asilia huko Mtwara. Kinyerezi peke yake kuja kufika mwaka 2020 tutakuwa na megawatt 1,560 za gesi asilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kwamba matumizi ya gesi asilia bado ni mengi sana. Mbali na kuzalisha umeme, gesi asilia itatumika katika masuala mengine yafuatayo:-

Kwanza, jumla ya trilioni 8.8 itatumika kuzalisha umeme; trilioni 4.3 itatumika kwenye viwanda vya mbolea na petrochemicals; trilioni 1.2 itatumika kusambaza gesi majumbani na kwenye magari yetu na trilioni 1.1 itatumika pia kwa ajili ya viwanda vya vyuma. Kwa hiyo, niendelee kusema bado matumizi ya gesi asilia ni makubwa na Serikali inaendelea kuyazingatia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema kwenye mradi wetu wa LNG tutatumia tani milioni 10 kila mwaka za gesi asilia. Kwa hiyo, nipende kusema tu kwamba pamoja na vyanzo hivyo tuna maana kwamba bado tunaendelea kutumia kile kinachoitwa energy mix kwa maana ya kutumia vyanzo vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini sasa tunataka kuendeleza Mradi wa Stiegler’s Gorge? Nitumie nafasi hii kusahihisha kidogo, naomba Waheshimiwa Wabunge mradi huu tuuite Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rufiji badala ya Stiegler’s Gorge. Stiegler’s Gorge ilikuwa ni jina la Mzungu aliyefika maeneo yale na alishaondoka na hayupo. Kwa hiyo, si vema sana kuendelea kumuenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa, Mradi huu wa Maporomoko ya Mto Rufiji utakaoweza kuzalisha megawatt 2,100 ni mkubwa sana. Waheshimiwa Wabunge, tutambue kwamba tumekuwa tukitumia miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji tangu enzi za ukoloni na miradi hiyo tunaitambua; tuna Mradi wa Kidatu, Mradi wa Kihansi, Mradi wa Mtera na New Pangani Fall. Miradi hii ina uhai wa zaidi ya miaka 40 na imeshaanza kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi kueleza kwamba ni vema sana tukaanza sasa kutumia miradi mikubwa ambayo itatutoa kwenye changamoto za upatikanaji wa umeme. Kuanza kwa mradi huu kutakuwa na manufaa makubwa yafuatayo:-

Tukiingiza megawatt 2,100 kutoka kwenye zile tulizonazo na zingine tukaingiza kwenye vyanzo mbalimbali tuna uwezo sasa wa kujitosheleza hapa ndani na kuwauzia majirani zetu. Kwa hiyo, niombe Bunge lako Tukufu kwa pamoja tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa kuanzisha mradi huu. Kwa kweli tukifanya hivyo tutajenga sasa uchumi wa viwanda utakaotuondoa kwenye changamoto za umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ukijengwa pamoja na kupeleka umeme katika gridi ya Taifa lakini utaleta maendeleo makubwa sana. Moja ya maendeleo ni ujenzi wa barabara za viwango vya lami kuelekea kwenye mradi wenyewe. Maendeleo mengine kwa sababu bwawa hili litakalojengwa litakuwa na urefu wa kwenda juu takribani ghorofa zaidi ya 78, itakuwa ni chanzo kikubwa cha kuvutia utalii ambapo utaleta fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile bwawa hili litahifadhi maji ya kutosha hata kwenye kilimo cha umwagiliaji. Niwashawishi Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono juhudi za Serikali ili mradi huu uendelee kutekelezeka sambamba na miradi mingine ya kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye mradi….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye mradi wa LNG, unaendelea vizuri. Utekelezaji wa miradi unaenda hatua kwa hatua, tulishakamilisha hatua tatu za mradi huu ambapo tulishapata eneo la ukubwa wa hekta 2,071. Tulishafanya tathmini ya fidia ambayo ni takribani bilioni 3.3 na tumeshakamilisha tathmini kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kazi zinazoendelea sasa hivi kwenye LNG ni kukamilisha majadiliano ambayo yatakamilika Septemba 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii nimwombe sana Mheshimiwa Mbunge mwenzangu, Mheshimiwa Nape tuwahamasishe wananchi wa maeneo yote ya Mtwara na Lindi uwekezaji wa LNG bado uko pale pale na mwaka huu wa fedha tumeomba bilioni 6.5 Waheshimiwa Wabunge mkiidhinisha mradi utatekelezeka vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe wananchi wa Mtwara na wananchi wengine waendelee kwenda kuwekeza Lindi na Mtwara kwa sababu mradi huu bado uko pale pale na utakamilika ndani ya wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nichukue nafasi hii kusema kwamba mradi huu utaanza kujengwa ndani ya miaka mitano na ukikamilika manufaa yake yataanza …