Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Serikali kwa ujumla kwa hotuba nzuri iliyosheheni mambo mazuri yenye masilahi mapana kwa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo mengi ya msingi yamezungumzwa juu ya Sekta za Mawasiliano, Kilimo, Madini, Elimu, Miundombinu na kadhalika. Kwa leo napenda kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi; changamoto ya ardhi imeathiri maendeleo ya wananchi wetu hususan katika Sekta ya Kilimo na katika maeneo mengi ya nchi yetu. Migogoro hii ni baina ya Vijiji na Vijiji, Kata na Kata na Wilaya na Wilaya. Kwa sehemu kubwa Watendaji wetu wa Vijiji, Kata na kushirikiana na baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji wanakuwa ni chanzo cha changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la mgogoro wa mpaka baina ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, suala hili limechukua muda mrefu sasa. Binafsi nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye mwaka 2017 alifika katika eneo hili kwa kuambatana na Waziri wa Ardhi na TAMISEMI na kutoa maagizo kwa Wataalam kupitia upya mpaka huo kwa kutumia Government Notice No. 61. Taarifa hiyo toka mwezi Machi, 2017 ilitoka ikibainisha wazi wapi mpaka wa Wilaya hizi upo. Jambo la kushangaza, mpaka leo hakuna utekelezaji wa kuweka alama za mpaka wakati Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni mia moja kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa maeneo ya mpakani wa Wilaya hizi bado wanaendelea kusubiri hatima ya jambo hili. Vile vile shughuli za kilimo na mifugo kwa kiasi kikubwa zimesimama kusubiri hatima ya suluhisho la mgogoro huu na mara kadhaa wananchi wa maeneo haya wameendelea kugombana kwa sababu ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima. Ni matumaini yangu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kupitia Wizara hizi mbili (TAMISEMI na Ardhi) watakwenda na kuweka alama za kudumu ili kutoa suluhisho la kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kutoa mchango wangu ni suala la maji vijijini. Changamoto ya maji vijijini bado ni kubwa, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kutatua changamoto hii. Naipongeza Serikali kwa dhati kwa jinsi inavyohakikisha na kudhamiria kutatua changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya maji katika Vijiji na Miji yetu mingi inakosa ubora unaotakiwa. Hii inatokana na baadhi ya Watumishi wetu kwa kushirikiana na Wakandarasi kukosa uadilifu. Naishauri Serikali iweke utaratibu kwa Wizara zenye dhamana na Sekta ya Maji na TAMISEMI wahakikishe kuwa wanaunda Kitengo Maalum cha ufuatiliaji wa miradi hii ya maji, inajengwa kwa kiwango na kuzingatia thamani ya fedha (value for money) badala ya kusubiri hadi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kupitia hesabu za maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke fedha zikitengwa kutekeleza mradi fulani huchukua miaka mingi eneo husika kupata tena fedha kwa mradi wa maji. Ni vema kwa sasa Serikali ikawa na mpango thabiti wa kusimamia miradi hii na kuwadhibiti wachache ambao hawana uchungu na rasimali za nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa dhati kwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini. Uamuzi huu una dhamira ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika katika kipindi chote cha mwaka. Dhamira hii nzuri ya Serikali inatakiwa iende sambamba kwa kuwa na chombo cha ufuatiliaji wa kazi za TARURA kwa kuangalia ubora wa kazi za TARURA. Je, ni nani msimamizi wa kazi za TARURA? Uwepo wa chombo hiki utasaidia dhamira nzuri ya Serikali juu ya uanzishaji wa chombo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali sasa ione umuhimu wa uanzishaji wa chombo kinachofanana na TARURA kwa kuanzisha Mamlaka ya Maji Vijijini. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kero ya maji vijijini. Chombo hiki kitakuwa na usimamizi wa huduma ya maji vijijini tukikumbuka sehemu kubwa ya Watanzania wanaoishi vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.