Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukupa pole kwa kuugua pia tunamshukuru Mungu kwa uponyaji wako. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na kutupatia Viongozi wazuri wenye nia njema ya kuleta maendeleo kwa Watanzania. Nampongeza sana Rais na Wasaidizi wake Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa ni kielelezo chenye kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wenye kuleta tija kwa jamii na Watanzania wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kusimamia shughuli zote za Serikali kwa umakini na umahiri mkubwa. Nawapongeza pia Mawaziri, Manaibu, Makatibu Wakuu na Watendaji wote wanaowasaidia katika utendaji wao wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi, naomba kuchangia mambo yafuatayo ambayo yamekuwa ni kero au changamoto kwa jamii katika maeneo husika:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Mkoa wa Dar es Salaam. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015 alipokuwa kwenye kampeni katika Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Segerea kwenye mkutano Vingunguti aliahidi kujenga barabara ya Segerea Seminari kuelekea Majumba Sita kupitia Kituo cha Polisi cha Stakishari kwa kiwango cha lami na kujenga daraja, lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote hata ya kukarabati ili wananchi wapite kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni mbovu watu wanapita ndani ya mto wakati wakielekea maeneo ya Ukonga kutafuta huduma mbalimbali kama Airport, Hospitali ya Ukonga ya Rugambwa, Mahakama ya Mwanzo Ukonga na maeneo mengine ya huduma. Eneo la Segerea Shell Oilcom (Kona ya Segerea Seminari) inahitaji mfereji wa kupitisha maji ya mvua kwa haraka ili kunusuru ile barabara isikatike kwa mvua inayoendelea maana hali ni mbaya katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya itoe fedha za bajeti kwa wakati ili kukidhi mahitaji katika sekta ya afya kwa muda unaohitajika. Kuchelewesha kutoa fedha kwa wakati husika kunasababisha maafa na kurudisha nyuma jitihada nzuri za Serikali za kuboresha sekta ya afya. Kwa mfano, Kitengo cha Moyo Muhimbili (Jakaya Kikwete Cardiac Institute), Kitengo cha Mifupa (MOI), Wodi ya Wazazi wanalala wawili kitanda kimoja na hii inasababisha maambukizi kwa watoto wachanga na kusababisha vifo. Hospitali zote za Rufaa na vituo vyote vya afya, naiomba Serikali kupitia sekta hii nyeti ya afya fedha zake zipewe kipaumbele, Wizara ya Fedha itilie maanani suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Madaktari wetu wanafanya kazi nzuri sana na ya kizalendo kwa kutoa huduma kwa kiwango cha Kimataifa hasa pale (Jakaya Kikwete Cardiac Institute) na Kitengo cha Mifupa (MOI) na pia Hospitali ya Kansa Ocean Road, Benjamin Mkapa Dodoma na Madaktari wote na Wauguzi nawapongeza wote sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.