Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia suala la ajira kwa wenye kiwango cha darasa la saba. Kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa kuona ni lazima kiwango cha ajira kianzie kidato cha nne. Ni jambo jema kabisa ndiyo maana ya kuanzisha elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu kwenye eneo hili, naomba kuishauri Serikali ione kuna umuhimu wa kuwarudisha kazini watumishi wote waliokuwa wameajiriwa kwa kiwango hicho cha elimu huko nyuma ili wafikie kipindi chao cha kustaafu na kupunguza gharama kubwa ya kuwalipa watumishi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hao wengi wao walioajiriwa kwenye kada za udereva, uhudumu na huduma mbalimbali katika ofisi za Serikali, kada ambazo hazihitaji utaalam mkubwa kwa level yao ya elimu. Najua Serikali ina nia njema ila kwa kipindi hiki cha mpito baada ya suala la elimu bure tunaamini mwamko wa kujiendeleza utakuwa mkubwa na hivyo kada hii ya elimu ya msingi itajifuta yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hifadhi ya mazingira; napenda kuipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango wa usafi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira. Pamoja na Serikali kuanzisha mpango huu na kuongeza idadi ya wakaguzi na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda unaozingatia utunzaji bora wa mazingira. Napenda kuishauri Serikali kuona ni namna gani ya kupiga marufuku

vifungashio vya plastic ili kuendelea kupunguza uharibifu mkubwa wa mazingira kupitia vifungashio vya plastic.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo. Nimekuwa nikifuatilia sana kwenye mikoa mbalimbali nchini ambayo imekuwa ni wazalishaji wakubwa wa chakula. Napenda kuishauri Serikali kuhusu suala la pembejeo ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa upande wa upatikanaji. Kwa kuwa, maeneo mengi yana Mawakala ambao wamekuwa na urasimu mkubwa kwa namna ya upatikanaji wa pembejeo. Ushauri wangu, ni kwa nini Serikali isione umefika wakati wa kusambaza pembejeo hizi kwenye maduka na kuhakikisha inatolewa bei elekezi ili kila mkulima apate pembejeo hizi kwa wakati kwa kuwa kumekuwa na upendeleo mkubwa wa upatikanaji wa pembejeo kwa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mazao ya biashara. Pamoja na Serikali kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao ya kahawa, korosho, pamba na tumbaku, kuna zao la apples katika Mkoa wa Njombe ambalo kama Serikali itaweka mkazo itasaidia upatikanaji wa apples kwa wingi katika nchi yetu na kuacha kuagiza apples Afrika ya Kusini ili kuongeza kipato kwa wakazi wa Mikoa ya Kusini na kuongeza mapato na uchumi wa Taifa letu.