Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma kushambuliwa kwa sababu ya uraia. Kumekuwa na tatizo kubwa la wananchi wa Mkoa wa Kigoma kusumbuliwa na Maafisa wa Uhamiaji juu ya kukamatwa, kusumbuliwa, kuhojiwa, kuwekwa lock up na hata kuombwa rushwa ili misukosuko hiyo iishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Kakonko, Jimbo la Buyungu kila basi linasimamishwa na abiria wote kuulizwa vitambulisho, kuvuliwa nguo za juu yaani shati au blauzi ili kuona chanjo iko mkono gani yaani kushoto au kulia. Hali hii isipodhibitiwa italeta kuzorota kwa amani ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma. Mikoa mingine ya mipakani hatuoni mambo haya yakifanyika, hii ni sambamba na raia wengi wa Kigoma kuhojiwa juu ya uraia wao, mfano; Askofu Kakobe (wa Kakonko), Abdul Nondo (wa Ujiji) na wengine wengi, hii haikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za wakimbizi-Mtendeli Kakonko; kumekuwepo na athari za mazingira kwenye Kambi ya Wakimbizi Mtendeli kwa ajili ya ukataji miti na kuni. Awali Serikali iliahidi kutoa gesi ya kupikia kuokoa miti inayoharibiwa na wakimbizi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji jirani na kambi kunyimwa maji. TCRS/UNHCR walikaa kikao na vijiji jirani na Kambi ya Mtendeli (host community) ili watoe maeneo ya kuchimba visima virefu kwenye maeneo ya vijiji kwa makubaliano ya kuwapa maji. Vijiji hivyo ni Asanda, Nkuba, Kewe, Kazilamihunda na Juhudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maji kupatikana (visima virefu) kwenye vijiji hivyo, maji yalipelekwa kambini bila kupewa vijiji vilivyoingia mkataba na UNHCR/TCRS. Huu ni uporaji wa rasilimali za wananchi kwani kambini (Mtendeli) maji yaliisha na kambi ilikuwa ihamishwe sasa wamepata maji na kuwanyima wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki maana maji ya vijiji vyetu yakiisha wananchi watahamia wapi? Aidha, wananchi wameahidi kuharibu miundombinu ya maji hayo yanayopelekwa kambini ili wakose maji wote, yaani wananchi (host community) na wakimbizi. Serikali iingilie kati suala hili ili kupunguza hasira ya wananchi kwa kuchukua maji yao na kuyapeleka kambini (Mtendeli) kinyume na mkataba (NB: mkataba upo)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji iliyokamilika lakini haitoi maji (miradi minne). Kuna miradi ya maji chini ya NORAD iliyokamilika na kulipwa fedha zote mpaka retention fee lakini imetengenezwa chini ya kiwango hivyo haitoi maji kabisa. Miradi hiyo hewa ni:-

Nyagwijima, Kiduduye (Kata ya Mafufunzu), Katanga (Kata ya Katanga) na Muhanga (Kata ya Muhanga). Miradi hii ni kero kwa wananchi kwa sababu wanaona mabomba bila maji hata tone. Haya ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali/mfadhili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri; wahusika kufilisi miradi hii na wakandarasi wawajibike.