Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na namshukuru Waziri Mkuu kwa sababu kimsingi anatimiza wajibu wake kama nafasi yake inavyosema. Nitaanza na eneo muhimu sana la ukurasa wa saba kwenye hotuba yake amezungumzia habari ya kudumisha amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba amani huwa hailazimishwi na utulivu wa Taifa hauwezi kulazimishwa kutumia mtutu wa bunduki. Jambo hili ili lifanyike vizuri ni lazima liwe ni zoezi shirikishi. Katika maeneo haya ndiyo maeneo ambayo sisi kama viongozi wa upande wa Upinzani tunalalamikia sana kwamba kwa sasa hali ilivyo ni kama tumesahau kwamba Rwanda nini kilitokea baada ya chokochoko nyingi; ni kama tumesahau nini kilitokea Algeria na tunazungumza kana kwamba haya mambo hayapo katika mataifa mbalimbali baada ya maoni ya Upinzani na viongozi mbalimbali kupuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunaona kitendo cha kusema tunakuwa tunadumisha amani na utulivu katika nchi, lakini wakati huo huo viongozi ambao tunakaa katika Bunge hili tunajadiliana mambo ya kitaifa kwa upendo kabisa lakini tunawakamata kwa hila, chuki na tunawasweka ndani, tunawanyima dhamana na watu wengine kadha wa kadha wameumizwa katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye mimi namheshimu sana, kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ukiangalia picha ya yule Diwani wa Kilombero alivyokatwa mapanga kama una moyo wa nyama lazima ushtuke sana. Ukiangalia watu wanavyookotwa katika fukwe mbalimbali. Kwa hiyo, mambo haya tungeomba kwa moyo wa dhati kabisa, kama tunalipenda Taifa letu la Tanzania ambalo tunalipenda sana ni muhimu mambo haya yachukuliwe hatua. Msione kwamba sauti za watu wanaolalamika ni kwamba ni watu ambao hawana maana, hapana!

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ambayo yanaendelea tunaanza kuonesha picha mbalimbali za watu wamepigwa risasi, wengine wamepigwa visu, wengine wametupwa kwenye fukwe za bahari maana yake tunawafanya watu wetu wazoee hii hali na huko mbele hata kama hatutakuwepo, makaburi yetu yataulizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe kama Serikali iliyoko madarakani, Chama cha Mapinduzi mchukue hatua ili Watanzania waishi kwa amani na amani ambayo inazungumzwa ionekane ikitendeka kwa maana kwamba tuheshimiane. Kama kiongozi na Mtendaji Mkuu wa Serikali ukusara wa kumi Mheshimiwa Waziri Mkuu amenukuu maneno mazuri sana, anasema; kuna uhuru wa wananchi kujiunga katika vyama vya siasa, kuna chaguzi mbalimbali zimefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yetu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba tunapoitisha uchaguzi, yule kiongozi ambaye wananchi walio wengi wamesema ndiyo wanamtaka ndiyo chaguo lao, huyo atangazwe aapishwe na awe kiongozi na mwakilishi wa eneo lile ili kupeleka maendeleo na isiwe vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka Sheria za Uchaguzi zifuatwe, wananchi hawataki polisi wengi katika vituo vya kupigia kura. Hilo tunatoa rai lishughulikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 33 wa hotuba ya Waziri Mkuu, kwenye eneo hili amezungumzia habari ya mifugo na minada na ukurasa huo huo wa 34 amezungumzia mambo ya utalii. Naomba nitoe taarifa kwamba kule katika Jimbo la Ukonga kuna mnada mkubwa sana wa Pugu unaitwa Mnada wa Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Mifugo alikuja katika eneo lile. Lakini mnada ule pale ukifika, jina ambalo linazungumzwa kwamba ni Mnada wa Kimataifa haufanani na hali yenyewe ya mnada ule. Pale hakuna maji ya kutosha, hakuna sehemu ya malisho, hakuna uzio, hakuna huduma ya vyoo vya kisasa, ni vurugu match katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungeomba kama tunataka kupata mapato mengi ya Serikali na ule ndiyo mnada ambao unatoa huduma kubwa katika Mji wa Dar es Salaam basi mnada ule uboreshwe. Lakini sasa imeibuka hoja eneo lile kuna mgogoro unaibuka kati ya mnada na wananchi wa kijiji/Kata ya Pugu Station Mtaa wa Banguro. Hawa watu walipewa hati ya kuwa kijiji na kufanya shughuli zao mwaka 1976 na Mwalimu Nyerere, lakini sasa wameshaishi zaidi ya robo tatu ya eneo lile lote, lakini inaonekana kwamba Wizara ya Mifugo wanasema ni eneo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunomba ili kupunguza migogoro, Serikali itumie akili ya ziada, ikae na wananchi wale, tukubaliane. Kama kuna haja ya kuhamisha mnada kutoka eneo lile kwa sababu sehemu ndogo tu chini ya robo ndiyo unatumika kwa ajili ya mnada na sehemu nyingine zaidi ya robo tatu ndiyo wananchi wanaishi basi hiyo kazi ifanyike mapema ili watu waendeshe shughuli zao. Kwanza ilitangazwa kama kijiji, wana hatimiliki lakini Wizara wanasema ni eneo lao pia. Kwa hiyo, huo nao ni mgogoro ambao naamini kwamba ukianza kujadiliwa ilileta shida katika kukwaza shughuli za kimaendeleo, lakini pia kupoteza mwngi sana wa viongozi kwenda kujadiliana katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 44 na 45 inazungumza habari ya barabara. Ninapozungumza sasa maeneo mengi sana ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga Mwenyekiti unafahamu, unatoka Ilala. Sasa hivi Dar es Salaam ile wakati wa mvua haipitiki na bahati mbaya ile mvua ikinyesha kwa muda mchache sana maana yake inaonesha ama miundombinu imechakaa au kazi haikufanyika vizuri. Lakini tunazo barabara kutoka Kitunda - Kivule - Msongola ambapo mkandarasi yupo zaidi ya miezi kumi amechimba mashimo pale. Nimemwambia Waziri anayehusika, nimewaambia watu wa TANROADS pale. Huyu mtu amekaa miezi kumi, amesababisha kero kubwa katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, kuna hoja inazungumzwa hapa ya TARURA, mimi kwa maana ya Manispaa ya Ilala, hawa watu walipokuja wamefanya kazi kubwa sana pamoja na kwamba kuna ugumu wa fedha. Kwa hiyo, nilikuwa naomba na maoni yetu ni kwamba ingewezekana hii fedha ya TARURA ya TANROADS ikawekwa asilimia 50 kwa 50 kwa sabau barabara nyingi ziko vijijini. Ili barabara zetu zitengenezwe na wakati wa mvua kuwe na mawasiliano iweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe tu kumekuwa na mambo mengi sana hapa lakini mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya TAMISEMI na Utawala. Tumepata taabu ya kujadili hii habari ya Tunduma. Ningemuomba Waziri Mkuu na Mawaziri wanaohusika kitendo cha ile Halmashauri kukaa zaidi ya miezi kadhaa kutokuwa na vikao hata bajeti ambayo imeletwa maana yake bajeti ile haikujadiliwa na Baraza la Madiwani na Mbunge na wananchi wamelalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitokea kuna uharibifu wa mali maana yake Madiwani wanajitoa, watumishi ndiyo wanapata lawama katika utendaji. Hili ni jambo ambalo halikubaliki, lifanyiwe kazi, hatua zichukuliwe. Wawakilishi wa wananchi wafanye maamuzi kwa kodi ya Watanzania wao ili waweze kujipelekea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bajeti ya Serikali, maji yamepata asilimia 25.32, afya ilipata asilimia 25, kilimo ni asilimia 18, TAMISEMI yenyewe ni asilimia 31. Katika mazingira hayo ndiyo maana Wabunge wanasema ni muhimu fedha ya maendeleo iliyotengwa mwaka wa fedha 2017/2018 ipelekwe ikamilishe Miradi ya Maendeleo vinginevyo tutakuwa tunapoteza muda hapa. Tunajadili bajeti ya muda huu lakini bajeti iliyopita haijatekelezwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu atakaposimama awaambie Wabunge na Watanzania mpaka sasa fedha ya maendeleo imepelekwa kiasi gani katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 48 unazungumzia habari ya elimu. Mimi nimpe ujumbe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana katika eneo hili kwamba kwanza hatuwezi kuboresha elimu kama tunatunga maswali ya kuchagua mpaka hata maswali ya hesabu kwenye mitihani ye sekondari na kisingizio kikubwa ni kwamba hakuna muda. Haiwezekani tukapunguza uelewa kwa sababu ya kusingizia muda. Tupunguze maswali lakini wanafunzi wetu wapimwe uelewa. Kwa mfano, katika shule zetu za msingi na sekondari, tuna upungufu mkubwa sana wa matundu ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kweli inatakiwa Serikali ije na mkakati. Kwa sababu kwa karne hii, Taifa la Tanzania kuzungumzia habari ya matundu ya vyoo kwamba kuna upungufu mkubwa maana yake unawaambia watu kwamba watu wetu wengi, wanafunzi na walimu wanaenda kujisaidia porini na kwa hiyo, wanachafua mazingira, walete kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha tuna upungufu wa matundu ya vyoo, shule za msingi 239,716; sekondari 19,122, madarasa maana yake watoto wanakaa chini, tuna upungufu wa madarasa 107,547, nyumba za walimu shule ya msingi peke yake ni upungufu wa nyumba 178,435; sekondari 69,816.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inamaanisha bado tunayo safari ndefu sana ya kuboresha elimu. Ukizingatia Sera ya Elimu ni kama kuna mkanganyiko mkubwa sana lakini ningeomba ili tuboreshe elimu mi lazima tunzingatie mambo ya msingi ya mahitaji. Upungufu wa walimu wa sayansi, vitabu, maabara na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa dhati kabisa, kuna hoja imeletwa nzuri sana ya elimu bila malipo lakini jambo hili limekuwa na mkanganyiko. Tukubaliane, kwa mazingira yaliyopo Serikali haitaweza kujenga madarasa yote yaishe, huo ndiyo ukweli! Serikali haiwezi kutoa chakula kwa wanafunzi wote mashuleni kwao, lakini ni lazima tukubaliane tuwe na lugha nzuri. Tushirikishe wadau mbalimbali ili tuboreshe elimu ya Tanzania. Kumekuwa na hoja hapa ya shule za private na shule za sekondari. Ningeishauri Serikali iweke msimamo kuboresha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)