Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kama ilivyo ada nianze kwa kuwapa hongera sana Ofisi ya Waziri Mkuu na timu yake kwa kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Serikali kupitia kwa Waziri Mkuchika kwa tangazo lake la asubuhi. Limetufariji sana kwa sababu maeneo mengi yalikuwa na shida, wenzetu wa Serikali hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mawili tu. La kwanza bahati nzuri nimeliandika kulipeleka kwa Mawaziri na watalaam ni kuhusu uraia. Nchi hii wananchi walio wengi wanaishi kwenye mipaka ya Taifa hili na katika mipaka ya Taifa hili upo Mkoa unaitwa Mkoa wa Kigoma. Sisi tumekuwa wahanga wakubwa wa ubaguzi wa waziwazi kabisa. Tumekuwa ni wahanga wa madhila na maonevu ambayo hayamithiliki kupitia wenzetu wa Idara ya Uhamiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu aje atueleze hawa wananchi wa Kigoma ambao wanasumbuliwa kwa sababu ya au maumbile yao, au sura zao, au lugha yao, kwa nini kila mara wanaambiwa wao siyo raia? Tunajua iko mikoa mingi, lakini jambo hili kwa Mkoa wa Kigoma limekithiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo kumetokea tukio la ajabu kabisa. Kuna mwananchi amekamatwa anaambiwa aende na wazazi wake wote wawili Uhamiaji wakati sisi tunajua kabisa ni mzaliwa wa pale pale. Haya madhila ni makubwa sana na tungeomba kwa kweli yatolewe ufafanuzi mzuri. Inawezekana pengine wenzetu wa Uhamiaji wamekosa tu weledi wa kutenda kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, litakuwa jambo la msingi sana wenzetu wa Serikali jambo hili wakilitazama na kwa kweli lipate ufumbuzi. Mbona hatusikii mambo haya kwenye mipaka mingine ya nchi hii kama Tanga, Mbeya au Kilimanjaro ni Mkoa wa Kigoma tu kwa nini? Hili jambo linatukera sana ningeomba lipatiwe majibu ya moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nitapitia ukurasa wa 44 wa hotuba ya Waziri Mkuu ambapo anazungumzia barabara na amebainisha wazi kabisa kwamba barabara zitakazojengwa zitakuwa na urefu wa kilomita 1,760. Sasa nina ushauri tu, katika barabara zinazopangwa kujengwa, najua Serikali ni moja jambo hili ningeweza nikalizungumza kwenye sekta ya ujenzi na kama alivyosema rafiki yangu Mheshimiwa Mgimwa pale, Waziri Mkuu ndiyo Kiranja wa Mawaziri wote, nataka nimpe angalizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi hii barabara ndefu kuliko zote ambayo haijajengwa kwa miaka 20 ni barabara inayoitwa Kigoma – Kasulu – Kibondo - Nyakanazi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati umefika barabara hii sasa ipewe kipaumbele. Kwa mfano, barabara hii ya Iringa - Dodoma imekuja sasa wakati barabara ya Nyakanazi ilikuwepo haijamalizika. Barabara ya Dar es Salaam - Mtwara imekuja sasa wakati barabara hii ya Nyakanazi - Kigoma haijakamilika. Barabara ya Singida - Minjingu imekuja sasa wakati barabara ya Kigoma - Nyakanazi bado haijajengwa kwa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mahitaji ya barabara ni muhimu sana katika nchi yetu, lakini barabara hii ndefu kuliko zote ambayo imesanifiwa miaka 20 iliyopita hata vipande vyake vya Kasulu - Kidahwe na Kabingo - Nyakanazi bado havijakamilika, wakandarasi wanadai fedha zao. Nimekuwa nikishangaa kupitia Wizara ya Ujenzi, wakandarasi hao walioko site kila wakiomba fedha zao wanalipwa kidogo kidogo na barabara hizi zimechukua muda mrefu sana takribani miaka 20 barabara haimaliziki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo hapa inasikia, tunaomba barabara hii ipewe kipaumbele vinginevyo tutachukua hatua ambazo hazipendezi sana kwa sababu hatuwezi kuona kabisa keki ya Taifa inagawiwa kwa ubaguzi wa dhahiri kabisa, kwa maana kwamba kuna maeneo mengine yanapewa kipaumbele na kujengewa barabara za lami na maeneo mengine yanaambiwa yasubiri.
Tumesubiri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Ndassa umerudi, jiandae Mheshimiwa Chuachua.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu bado.