Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Alfredina Apolinary Kahigi

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami ili kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyotuletea mbele yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo imejaa mambo mazuri mengi, inasomeka na inaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nichangie hoja chache ambazo nimezipangilia. Nianze na upande wa kilimo. Mimi natokea Mkoa wa Kagera. Hatujamaliza mwaka mzima Mheshimiwa Rais amepunguza tozo ambazo zilikuwa zinabambikizwa wakulima wa kahawa lakini nami lazima niungane na Wabunge ambao jana walizungumzia zao la kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kahawa, sijui hao ambao wameleta kilio tena kwa mara nyingine wamepewa mamlaka na nani kushusha bei ya kahawa na kuirudisha kilo moja Sh.1,000. Wakulima wa kahawa sisi tunakaa pembezoni mwa nchi ya Uganda na kahawa nyingi huwa zinaenda sehemu ya Uganda, nina wasiwasi hata kama wakiweka ulinzi wa namna gani kahawa zitavushwa zitaenda Uganda na pato la Taifa litapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo, Waziri wa Kilimo yupo, naomba hili suala walishughulikie haraka sana iwezekanavyo kabla kahawa hazijavushwa kwenda Uganda. Binadamu ana akili kali sana huwezi kumzuia, hata ukiwa na bunduki atafanya njia zozote zile atavusha hizo kahawa. Toka juzi wamenipigia simu wanaomba hili suala tuliongelee kwenye Bunge. Sasa maadam tuko kwenye Bunge, kilio cha wananchi nimekifikisha, hivyo naomba hatua za haraka zichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi upande wa barabara, kuna Wilaya tatu ambazo zina barabara ambayo haina lami lakini barabara ni nzuri. Nashukuru Serikali ya Mheshimiwa John Joseph Magufuli imeshughulikia barabara na nchi yetu ni kubwa. Nishauri kutoka Muleba Kusini kwenda Bukoba Vijijini kwenda Wilaya ya Karagwe tuna barabara ya udongo. Niishauri Serikali kwa kipindi hiki ambacho tunaingia kwenye bajeti, barabara hiyo waitengeneze kwa kiwango cha lami maana ni kilometa 74. Naomba hilo walizingatie kwani barabara hiyo inasaidia Wilaya tatu, kuingiliana ni kitu cha maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Omurushaka - Murongo katika Wilaya ya Kyerwa, ina kilomita 120 inaungaisha nchi mbili, Tanzania na Uganda.Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu, naomba na barabara hiyo waishughulikie. Ukienda upande wa Uganda unakuta wana barabara ya lami, ukija huku ni barabara ya udongo. Mvua zikinyesha magari yanapita kwa shida sana, hivyo, kama wakitengenezewa wakawekewa lami itakuwa ni nzuri zaidi na itadumu kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke kwenye suala hilo nije kwenye afya. Kikao kile tulichomaliza niliomba Wilaya ya Bukoba Vijijini na sisi tujengewe Hospitali ya Wilaya kwani hatuna Hospitali ya Wilaya. Wilaya zote zina Hospitali za Wilaya, lakini ni Bukoba Vijijini peke yake ndiyo haina Hospitali ya Wilaya. Nina matumaini makubwa na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake waliniahidi kwamba watatujengea na sisi hospitali. Nimesikia wanasema Wilaya 27 watajengewa hospitali, sina uhakika kama na Wilaya yetu wameiweka, kama wameiweka nitashukuru sana na sisi kupatiwa nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina akili timamu, naongea kitu ambacho nakijua na wamekuwa na mazoea nikisimama kuongea wanaanza kubeza, lakini siyo wote ni wale ambao akili zao sijui zikoje. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika bajeti hii kweli waikumbuke Wilaya yangu, watujengee Hospitali ya Wilaya tuachane na kwenda kwenye hospitali za private na sisi tuwe na hospitali yetu ya kujitegemea moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka upande wa afya nakuja kwenye siasa. Sina vya sijui ni ukurasa gani na nini mimi natwanga tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika siasa tuna Msajili wa Vyama vya Siasa, nipende kumtia moyo na kumshukuru sana. Ni Jaji mwenye akili nzuri sana, ni mtiifu na nimshukuru Mheshimiwa Rais aliyemteua kumpa nafasi hiyo. Ujumbe nataka ufike kwa Mheshimiwa Rais; huyu baba hapaswi kumtoa katika nafasi hiyo, ni mvumilivu, ni mstahimilivu ametukanwa sana, lakini mimi nimemsikiliza sana ni baba mwenye moyo safi sana, baba anayependa kulea vyama vyetu, Mheshimiwa Rais aendelee kumweka katika nafasi hiyo mpaka tujue ustaarabu ni nini, anatukanwa bure baba wa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili na Mheshimiwa Mutungi alipo ajue kwamba Mama Kahigi nipo pamoja naye, Mheshimiwa Rais namshukuru sana kwa kutupa Msajili mwenye busara kama huyu, anatukanwa bure, Mungu atawaona. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niende kwenye miundombinu. Kwenye miundombinu naishukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mkoa wangu wa Kagera tuna uwanja wa lami ni mzuri mno, lakini hatuna taa za kwenye uwanja ndege haiwezi kuteremka usiku. Ni kitu kimoja tu hicho ambacho wanaweza wakatusaidia, wakatuwekea taa za ndege kuweza kushuka usiku vinginevyo uwanja ni mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.