Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kumpa pongezi Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya; kwa muda wa miaka miwili na nusu hii amefanya mambo mazuri sana. Mwenyezi Mungu ambariki katika kazi zake zote anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kumpa pongezi Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri naye anayoifanya pamoja na watendaji wake wote wa Serikali, kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana; Mheshimiwa Jenista, Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu wote na wafanyakazi wote nawapa pongezi sana kwa hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ameitoka hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na mazuri sana ambayo yamefanyika katika Mkoa wangu wa Morogoro, nianze na viwanda. Katika Mkoa wangu wa Morogoro, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi naye juzi juzi alikuja kwenye kiwanda cha sigara, Mheshimiwa Rais ameweza kufungua kiwanda cha sigara. Kwa kweli Morogoro tunakwenda vizuri kwa upande wa viwanda, si mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa viwanda tuna 21st Century, tuna Mazava na viwanda vingine vyote vinaendelea vizuri. Ila hapa naomba vile viwanda ambavyo havifanyi kazi ambavyo vimekufa, naomba itafutwe namna ya kuvifufua na wale ambao hawawezi kuviendesha naomba sana waweze kunyang’anywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda cha magunia, wananchi wengi sasa hivi wanalima wanahitaji magunia ya kuhifadhi mazao yao, lakini hiki kiwanda hakifanyi kazi. Naomba sana Serikali ione jinsi ya kufufua hiki kiwanda cha magunia badala ya kuagiza magunia kutoka nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Morogoro tayari standard gauge inajengwa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na naamini kuwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro wataitumia vizuri sana; nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Kilombero; kwa kweli wananchi wa Morogoro tunashukuru sana kuona kuwa Daraja la Kilombero sasa hivi linafanya kazi na unaweza ukapita wakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shamba la miwa la Mkulazi ambalo linafaidisha sana hata wakulima wa nje (out growers), ambao tunaweza tukapata sukari, pamoja na shamba la Mkulazi II ambalo litaongeza sukari. Kwa hiyo kwenye matatizo ya sukari kuna kipindi ambacho huwa tunapata tatizo la sukari, naamini kuwa Watanzania tutaweza kupata sukari pamoja na ajira na mambo mengine; pia na umeme, tutaweza kuzalisha hata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimaliza hayo nakuja kwa upande wa TARURA; pale mjini Morogoro barabara kwa kweli zimeharibika, naomba watu wa TARURA waweze kutengeneza barabara za Morogoro Mjini kwa sababu Morogoro Mjini kuna barabara ambazo unapita zimekuwa mashimo, kwa hiyo naomba sana Serikali iweze kuwapatia hela ili waweze kututengenezea Mji wetu mzuri wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya; naomba niongelee hospitali yetu ya mkoa. Wabunge wengi wa Morogoro hapa Bungeni huwa tunaongelea hospitali ya mkoa, tunaomba kila siku X Ray. Hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Morogoro wakati pale anaangalia kiwanda pamoja na Mkulazi II niliomba X Ray na humu ndani Wabunge wenzangu wamekuwa wakiomba kuhusu X Ray. X Ray ya Hospitali ya Rufaa ya Morogoro haifanyi kazi vizuri. Pia tumeomba vifaa vingine kama CT Scan. Naomba muiangalie vizuri Hospitali yetu ya Morogoro, inahitaji kuboreshwa zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Morogoro kuna Wilaya ambazo hazina hospitali kwa mfano Wilaya ya Mvomero na Morogoro Vijijini. Unakuta Wilaya hizi wagonjwa wengi wanakuja kutibiwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Rufaa na wanarundika sana. Kwa hiyo, naomba kwenye bajeti nijue hii Hospitali ya Morogoro Vijijini ni lini itajengwa? Naamini hela kiasi ilipelekwa lakini hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haijengwi pale Mvuha iliposemekana basi naomba kiboreshwe Kituo cha Afya cha Dutumi au cha Tawa na kupata hadhi ya Hospitali ya Wilaya pamoja na Mvomero hatuna Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye upande wa maji, Mkoa wetu wa Morogoro Wilaya nyingi hazina maji safi na salama hasa Morogoro Mjini kwa kweli mitaa ipo, lakini unakuta kata nyingi hatuna maji safi na salama. Tuliambiwa kuwa Bwawa la Mindu litaweza kukarabatiwa na tukaambiwa kuwa usanifu tayari umefanyika, lakini mpaka sasa hivi haieleweke ni lini hili Bwawa la Mindu litaweza kukarabatiwa na tutaweza kupata maji, kwa sababu ukiongea na Mheshimiwa Waziri wa Maji inaonekana muda wake bado kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maji pia niongelee kuhusu Wakala wa Maji Vijijini. Naomba Wakala wa Maji Vijijini iweze kuanzishwa kusudi tuweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niongelee kuhusu Sh.50 kwa kila lita ya dizeli pamoja na petroli iweze kuwa Sh.100 ili tuweze kupata maji ya kutosha. Wananchi wote wanahitaji maji, hakuna hata Mbunge mmoja hapa ambaye hahitaji maji. Maji ni muhimu sana naomba Wabunge wote waunge mkono kuhusu jambo hili la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu asilimia nne ya akinamama, asilimia nne ya vijana na asilimia mbili kwa walemavu. Ni kweli Halmashauri zingine zinatoa lakini Halmashauri zingine hazitoi. Kwa hiyo, naomba kuwa tamko litoke hapa Bungeni tena Wakurugenzi waweze kutoa hizi hela bila kujali wanapata mapato ya ndani kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa nishati ni kweli Waheshimiwa Mawaziri wanafanya vizuri mdogo wangu Mheshimiwa Subira pamoja na Mheshimiwa Kalemani mnafanya vizuri kwa upande wa REA. Hata hivyo, kuna vijiji mbalimbali kwenye Mkoa wa Morogoro hasa Kimamba, Kitongoji cha Diwani Frola ambacho mmekipitia, lakini wananchi wote wanaokaa hapo hawana umeme. Kwa hiyo, naomba mkiangalie pamoja na vijiji vingine ambavyo bado havijapata umeme wa REA kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu, namshukuru Mheshimiwa Rais na viongozi wote wa Serikali kwa kweli elimu bure (bila malipo) ni nzuri sana. Hata hivyo, naomba mhamasishe kuchangia chakula cha mchana kusudi watoto wetu waweze kupata chakula cha mchana, naona wazazi wengi hawajaelewa. Kwa hiyo, naomba litoke tamko hapa Bungeni kuhamasisha kuchangia angalau chakula cha mchana kwa watoto wetu hawa wanaosoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Morogoro upande wa Walimu wa sayansi sekondari tuna upungufu wa Walimu 614 na kwa upande wa maabara tuna upungufu wa maabara 281. Kwa upande wa shule za msingi ambapo mara kwa mara huwa tuna Walimu wengi, lakini sisi tuna upungufu wa Walimu 4,643. Kwa hiyo, naomba wazifanyie kazi hizi takwimu ambazo nimezitoa ili tuweze kupata Walimu wa sayansi kusudi tuweze kwenda na sayansi na teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo hasa cha umwagiliaji, naomba tukiangalie. Tusiseme tu green house, green house, no, lazima tuangalie tutahamasishaje kilimo kwa sababu bila ya kilimo…

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ingawa muda ulikuwa kidogo, ahsante sana.