Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti ya Waziri Mkuu. Kwanza nataka niseme tu mwanzo kwamba nahitaji kumpa pole Mheshimiwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, lakini pia pamoja na Wabunge wote wa Upinzani ambao kwa muda mfupi wiki mbili zilizopita wamepata matatizo na kashkash kutokana na Jeshi la Polisi kutumia nguvu, lakini pia viongozi wetu kuendelea kupata shida kwa sababu wanapigania haki katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji kujikita kwenye mambo machache tu na ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize kwa makini kwa sababu katika Mkoa wa Katavi tuna changamoto nyingi ambazo tangu mwaka 2008 mpaka sasa tumekuwa tukipigania mambo haya lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi inashindwa kutoa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 halmashauri ilitenga fedha kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu, lakini pia kuna fedha ilitengwa kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa hospitali ya mkoa katika Mkoa wetu wa Katavi. Hata hivyo, lakini projects hizi zimefeli, pesa zimepigwa, halmashauri iko kimya na sisi kama Wabunge tumekuwa tukipata hoja kutoka kwa wananchi kwamba ni kwa nini mambo haya, Mkurugenzi pamoja na Baraza la Madiwani 2010 mpaka 2015 walipitisha maazimio haya na fedha hizi zikawa zimetumika ndivyo sivyo, lakini tukihoji kwamba ni kwa nini michakato hii imeishia hewani, wananchi wanapiga kelele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo haya, kwa sababu ujenzi wa hospitali ya mkoa, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo katika Mkoa wa Katavi yalikuwa yametengwa katika eneo moja kwa maana ya Kata ya Kawajense. Kuna zaidi ya ekari mia tano lakini mpaka sasa wananchi wako pale, wamechukuliwa maeneo yao hawajalipwa fidia, wakienda kufuatilia kwa Mkurugenzi pamoja na Meya Serikali iko kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini tamko la Serikali ili tujue kwamba wananchi hawa ni kweli wameporwa maeneo haya na ni kwa nini Serikali iko kimya kufuatilia michakato hii? Kwa sababu maswali ya msingi nimekuwa nikiyauliza sana kuhusiana na wizi huu uliofanyika katika Manispaa ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Waziri Mkuu atakapokuja kuhitimisha, naomba kabisa kupitia jambo hili, kwa sababu ndiyo imekuwa kero ya wakazi wa Mkoa wa Katavi. Sasa kama Serikali ni sikivu na imekuwa ikitumbua majipu. naomba katika Manispaa hii ikasimamie jambo hili. Wizi uliofanyika katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo katika Mkoa wa Katavi, lakini pia wizi uliofanyika katika suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; nataka niongelee tu kidogo kuhusiana na ununuzi wa gari la taka. Baraza la Madiwani 2010 - 2015 lilipitisha fedha zaidi ya milioni mia moja kwa ajili ya ununuzi wa gari la kisasa la taka, lakini mpaka hivi tunavyoongea gari halijanunuliwa, matokeo yake Baraza la Madiwani linakuja kupitisha fedha nyingine kununua gari lingine jipya. Maana yake yule Mr. Kisira ambaye alipewa tenda kwa ajili ya ununuzi wa hilo gari la taka mpaka sasa hajarudisha hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zimepigwa, matokeo yake Baraza la Madiwani kazi yake ni kupitisha tu kwamba tunanunua gari lingine wakati tukiendelea kufanya mchakato huyu Mr. Kisira ambaye ndiye alikuwa mzabuni wa ununuzi wa hilo gari la taka alishindwa na hakuwa na vigezo vya kununua hilo gari la taka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nifahamu tu, kwamba kama Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu inashindwaje kwenda kutatua mgogoro huu ambao umekuwa ni kero kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi, lakini mpaka hivi tunavyoongea wananchi wa Mkoa wa Katavi Manispaa ya Mpanda wanachangishwa shilingi elfu mbili kila kaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takataka zinazagaa kwenye maeneo yao, Manispaa iko kimya, ukimuuliza Mkurugenzi hana majibu, Meya hana majibu. Sasa tutaendelea kupongeza mambo kama haya ikiwa manispaa ni chafu? Mnatumbua maeneo mengine Manispaa ya Mpanda mnaiacha na wananchi wanachangishwa fedha. Sasa mtueleze tu kwamba gari hili la taka, mimi kama Mbunge nimeshindwa kupata majibu ya msingi niende nikawaeleze nini wananchi wa Manispaa ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niongelee kidogo kuhusiana na masuala ya viwanda. Bado tuna changamoto za viwanda katika Mkoa wa Katavi na hazikidhi na ukizingatia Mkoa wa Katavi tunalima sana, kwa maana ya mazao ya biashara pamoja na mazao ya chakula. Sasa tunavyoongea ni kwamba hatuna viwanda ambavyo vinaweza kukidhi kuzalisha ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda cha alizeti ambacho kiko katika Kata ya Makanyagio, Kiwanda cha Mpadeku. Kiwanda hiki kiko dormant, tunalima alizeti lakini hawazalishi hata zaidi ya tani moja, matokeo yake tumekuwa tunatumia gharama kubwa za uzalishaji, kitu ambacho kinasababisha sasa tunatumia gharama kubwa ya uzalishaji lakini hatupati masoko, lakini pia hatupati faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba tu, kwa sababu mnajinasibu ya kwamba ni Serikali ya Viwanda, basi ningeomba tu sasa mtuongezee viwanda kwenye Mkoa wa Katavi kwa sababu viwanda vingi ambavyo viko kule tukitegemea vingeweza kuzalisha mazao mbalimbali tungeweza kusindika mazao hayo kwenye viwanda vidogo vidogo lakini imekuwa ni tofauti, kwamba wananchi hawaoni matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika changamoto hizo za viwanda, Manispaa ya Mpanda imetenga eneo la Kata ya Misunkumilo, eneo hili wamechukua wajasiriamali wadogo wadogo ambao wamewatoa katika maeneo mbalimbali kwenye Manispaa ya Mpanda. Wamewafukuza kwenye maeneo ambayo wanafanya kazi wakiwepo wanaokata mbao maana ya viwanda vya mbao kwenye Manispaa, lakini wakiwepo wakata vyuma, wale mafundi welding.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe tu wajasiriamali hawa wadogo wadogo wamepelekwa katika eneo la Misunkumilo, Manispaa wametenga eneo hili, lakini wamepelekwa kule, hakuna umeme, hakuna maji lakini pia miundombinu yake ni mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali hii ni sikivu ningeomba ingeweza kuwasaidia wananchi hawa kwa sababu wanapigwa, wanafukuzwa kwenye manispaa wanapelekwa kwenye eneo ambalo hakuna miundombinu, sasa niombe tu kama mko tayari kweli kuwasaidia wananchi kwa ujumla na wakazi wa Mkoa wa Katavi mpeleke kwanza miundombinu ya maji pamoja na umeme na si kukurupuka tu kuwafukuza wananchi kuwapeleka kwenye maeneo ambayo hakuna miundombinu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tu suala la mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake, wazee pamoja na walemavu katika Mkoa wetu wa Katavi. Mikopo inayotolewa katika manispaa ninayotoka mimi, Manispaa ya Mpanda Mjini, leo hii tunavyoongea vijana wamekopeshwa fedha, baadhi yao kwa maana ya kwamba sasa hawa Maafisa Maendeleo na watendaji ambao wanahusika na masuala mazima ya kutoa mikopo hii, kuna baadhi ya vikundi vinatoa malalamiko kwamba pesa hizi zinatolewa kwa ubaguzi kwa maana ya kuangalia itikadi zao za vyama na mambo mengine. Kwa hiyo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)