Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami nichangie kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano imetusaidia vituo vya afya viwili vinajengwa, kila kituo kimepata shilingi milioni 500, tunaishukuru sana Serikali, kusema kweli inastahili pongezi za hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi ina miaka 42 haina Hospitali ya Wilaya. Unakuta Wilaya zinaanza miaka mitano iliyopita au miaka 10 iliyopita zina Hospitali za Wilaya, lakini Wilaya ya Nkasi ina miaka 42 tangu imeanzishwa haina Hospitali ya Wilaya, ni kutuletea vituo vya afya tu, ndugu zangu haiwezekani na sisi tunastahili kupewa Hospitali ya Wilaya katika Wilaya ya Nkasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji, kila mwaka napiga kelele hapa, kila Bunge napiga kelele kuhusu miradi ya maji. Miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ndio mmefanya kokoro yaani ni wizi wa hali ya juu. Nashukuru Naibu Waziri wa Maji alikuja na Waziri mwenyewe alikuja na amejionea jinsi wanavyoshirikiana namna ya kuziiba hela za Serikali kupitia kwenye miradi ya maji, hasa Wilaya ya Nkasi. Serikali naiomba iendelee kuchukua hatua wote waliohusika, hata kama wamestaafu, wako wapi, wachukuliwe hatua, hata kama wamehamishwa wachukuliwe hatua, ili hela za Serikali zirudi wananchi wafaidike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara, tumepata barabara kule lakini barabara ndugu yangu haiunganishi Mikoa miwili ya Rukwa na Katavi. Barabara inaishia Kizi na inaishia Stalike, pale katikati hatujui itakuwaje hamna barabara ya lami. Serikali inasema kwamba Mikoa iunganishwe kwa lami, lakini Mkoa wa Rukwa na Katavi haijaunganishwa kwa lami miaka yote. Ukishafika Stalike hapo ndiyo mwisho wako na ukitokea huku kwangu mwisho wako kwenye Jimbo langu, Kizi ndio mwisho wa lami. Sasa pale katikati ndugu yangu hakuna lami, naiomba Serikali ifikirie sana kuipa lami hiyo barabara ili kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha VETA; namuomba Waziri wa Elimu, namshukuru sana Waziri wa Elimu na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kunipatia majengo yaliyokuwa ya wakandarasi kwa ajili ya Chuo cha VETA pale Paramawe. Watu wa VETA Kanda ya Mbeya wameshakuja kukagua wamekubali kabisa, walitaka tuwape eka 25 kwa ajili ya chuo hicho, sisi tumewapa eka 50. Sasa naomba Wizara ya Elimu iwape nguvu, iwape pesa kumalizia yale majengo, yako majengo 14 tena grade one kabisa yale majengo, wamefurahi. Kwa hiyo, naomba Chuo cha VETA kianzishwe haraka pale kuna kila kitu, umeme upo, maji yapo na tumewapa eka 50 badala ya eka 25. Kwa hiyo, ninaomba Waziri wa Elimu yuko hapa ananisikiliza, haraka iwezekanavyo ili Chuo cha VETA kianzishwe katika Wilaya ya Nkasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika. Nafikiri hata asubuhi kuna swali moja liliulizwa kwamba namna ya kupeleka bidhaa Kongo; ndugu zangu bila cheleo cha kuvusha mali pale kati ya Ziwa Tanganyika haiwezekani. Hakuna usafiri wa kuaminika katika Ziwa Tanganyika. Meli tangu Mjerumani, ndugu zangu ninyi wote hamjazaliwa hapa, bado linadurumiza katika Ziwa Tanganyika, haiwezekani, haiwezi kusaidia kupeleka bidhaa Kongo au Burundi au Zambia, haiwezekani. Tunahitaji meli kubwa mpya kwa ajili ya kuhudumia Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbolea. Asubuhi ndiyo nazungumza hapa kuna Wabunge wengine ndugu zangu wanakuja humu Bungeni hawana Majimbo, anazungumza kabisa Mbunge sijui anatoka wapi, anasema Serikali naipongeza iligawa mbolea kwa uzuri sana nchi hii, ndugu zangu, huyu analima au halimi? Ana wakulima au hana wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuingilia Rais Magufuli, ndiyo tunamshukuru, ndiyo mbolea kufika vijijini kwetu. Yeye anazungumza kwamba waligawa mbolea vizuri na kusifu Serikali tangu mwanzo mpaka asubuhi wakati hajui lolote, hajui hata mbolea inatumika wapi au namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tunazungumza mambo mengine kuhusu sukari na bidhaa mbalimbali. Haiwezekani mimi mkulima, Serikali ni sawa na familia nyumbani kwako, wewe unalima gunia 10 nyumbani kwako, matumizi yako nyumbani gunia 20 za mahindi, wewe utakuwa huna akili kiasi gani ukauze mahindi yako wakati matumizi yako gunia 20 na umelima gunia 10, utakuwa una akili au mwendawazimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuja hapa unazungumza habari ya sukari ya Zanzibar wakati hata sukari yenyewe wanasema ni magendo, kila siku mnakamatwa na karafuu mnavusha. Mnakamatwa na madumu kule Zanzibar, Tanga, mmegeuza huku Bara ndiyo uchochoro wa kuingiza bidhaa zenu. Madumu ya mafuta yanakamatwa kila kukicha, inakamatwa sukari kila siku, Bagamoyo mnapakia sukari chini mnaweka mchanga juu, nani hajui, Serikali mnaifanyia mchezo. Dawa yao hawa kunyang’anya vyombo vyao na yule tajiri kumtia ndani, kutaifisha kila kitu, majahazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mzalishe kule, hawa ndugu zangu hawalipi ushuru. Container la spare parts za pikipiki hawa wanalipa shilingi 5,000,000wakati Dar es Salaam vijana wauza Kariakoo wanalipa shilingi 40,000,000 container la spare za pikipiki na hakuna pikipiki kule wanaingiza makontena na makontena wanayavusha kwa jahazi kuleta Bara huku, nani hajui? Leo mnageuza uchochoro huku kwetu? Mnataka kututania? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari mnalima tani 8,000 kwa mwaka, matumizi yenu tani 17,000 mtakuwa na akili sawasawa muuze sukari wakati ninyi wenyewe haiwatoshi au hamnywi chai? Kama hamna pesa ya kununua sukari mseme tuwasaidie, siyo kusema sukari inawatosha, inawezekana hawana pesa za kuweza kununua sukari, maana sukari tani 8,000 matumizi tani 17,000 sasa inakwenda wapi hiyo sukari? Mnaagiza sukari za magendo kutoka Seychelles, kutoka wapi Mauritius, mnaingiza sukari kutoka Brazil sukari hailipiwi ushuru, wala haina vigezo, haitakubalika, haikubaliki, sheria ni msumeno.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Taarifa ni ya kwake, maana hajui hata kulima huyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikiliza kwa makini, nakueleza hivi Mheshimiwa, mimi ni mkulima nalima gunia 10, mahitaji yangu ya kula nyumbani kwangu gunia 20, naweza kuuza gunia 10 zile? Nitakuwa na akili? Niue familia yangu? Wewe uuze sukari huku, baadae uje kununua sukari Bara upeleke Zanzibar una akili kweli? Ndio nilisema hujui biashara, mimi nimeanza biashara wewe hujazaliwa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuambia haiwezekani na Waziri wa Fedha yuko hapa, ni lazima kuanzia Tanga mpaka kule Mtwara idhibitiwe barabara mipaka yeyote anayeingiza mafuta ya kula, anayeingiza sukari, anayeingiza spare za pikipiki, spare za gari, ataifishwe vyombo vyake na yeye mwenyewe kukamatwa. Haiwezekani, tunalipa kodi ushindani wa biashara utakuwa hakuna. Ushindani wanaagiza tani 20,000 Zanzibar ongeza tani 8,000 tani 28,000 matumizi yao tani 17,000 tani 11,000 mkamuuzie nani? Mnageuza dampo huku, hakuna cha dampo huku, ujanja ujanja huo hakuna bwana. Unaogea sabuni halafu unaitupa chooni sabuni unaokota unaenda kuogea tena, haiwezekani.

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuzungumzi habari ya Muungano. Tunazungumza habari ya ulipaji wa kodi na ukwepaji wa kodi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mneemeke kwa kuleta bidhaa zenu ambazo hazilipiwi ushuru, ushidani wa biadhara uko wapi? Haiwezekani, kwanza ninyi nawauliza swali moja, mfumo wa kodi wa Kimataifa jiungeni, jiungeni na mfumo wa kodi wa Kimataifa, lakini mmekaa hamjiungi na mfumo wa kodi wa Kimataifa kwa sababu mmezoea kukwepa ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Khatib alikuwa anazungumza hapa, mimi nilinyamaza nikawa kimya, sasa nakujibu mapigo...

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mtu mwenye busara unalima mikungu miwili ya ndizi, unakula mitatu, unauza ndizi zote watoto wako wale nini?

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa yake na yeye naona akapimwe akili, maana anaacha watoto wake wana njaa anasaidia watoto wa jirani, akapimwe akili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaeleza namna ya ukwepaji wa kodi. Hawa jamaa wamezoea kutuletea bidhaa, nafahamu container la spare za pikipiki linatozwa shilingi milioni tano hadi milioni sita. Nenda TRA pale Dar es Salaam milioni 40 vijana wa Kariakoo wanalipa, tutalinganishaje biashara? Mnateremsha kwenye majahazi usiku, nani hawajui wengi mnaweka bidhaa chini mnaweka mchanga juu, nani hajui? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima iwe macho kuangalia uhujumu wa namna hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wamekamata mafuta Tanga, nani hakuona kwenye television?

T A A R I F A . . .

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana na naipokea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara ya Fedha kuanzia sasa iwadhibiti watu hawa, kila siku kutolewa kwenye television mafuta yanakamatwa, inakamatwa sukari, sasa ni kutaifisha vyombo vyao na wenyewe wafunguliwe mashtaka, wafilisiwe mali yao, wataacha kuleta mchezo wa kukwepa kodi. Kukwepa kodi ni kosa ndugu zangu, tunahitaji barabara, tunahitaji dawa katika hospitali, tunahitaji kila kitu kutokana na kodi, hii nchi inaendeshwa kwa kodi, acheni kukwepa kodi ndugu zangu tuwe macho.