Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niongee katika Bunge lako Tukufu. Kwanza nianze na pongezi kwa Serikali yetu na kufuatia ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale Ludewa tarehe 26 Januari, 2017, imeleta matokeo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofika Ludewa aliambiwa juu ya taabu kubwa ya barabara, hasa ile barabara inayotoka Mkiyu kuja Madaba ambayo inapita kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma na pia kuna ile barabara ambayo inatoka Mchuchuma kwenda Liganga. Mpaka hivi ninavyozungumza, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeanza toka ile Julai, 2017 na unaisha mwezi Oktoba mwaka huu. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napongeza miradi ya REA inayoendelea katika Jimbo langu. Wakandarasi wapo na wanaendelea na kazi hivi ninavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali katika miradi hii ya Vituo vya Afya. Zile shilingi milioni 500 tumepata katika Vituo vya Afya viwili; Vituo vya Afya vya Manda na kule Mlangali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, alipita Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mheshimiwa Engineer Nditiye, tumeona impact ya ile ziara. Sasa hivi ninavyozungumza, minara nane ya mitandao ya mawasiliano ya Halotel imeanza kujengwa. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hatua ambazo inachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie na mambo mengine yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma ni mradi wa kimkakati. Napenda sasa kuiomba Serikali kwamba hii miradi lazima tuiwekee programu. Kwa sababu ni miaka mitano, lazima tuwe tunajua mwaka wa kwanza tunafanya kitu gani? Mwaka wa pili tunafanya kitu gani? Mpaka ile miaka mitano itakapofika na iweze ku-take off. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa naamini kwamba, hizi barabara zinazotengenezwa sasa kuelekea kwenye hii miradi miwili ni miundombinu wezeshi kuelekea huo mradi kuanza. Pia, tuna ule mradi wa Makambako – Songea, Madaba – Ludewa, kwa maana ya Gridi ya Taifa na yenyewe sasa hivi tayari imeshafika Ludewa, bado tu muda kidogo uende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itupe ule mpango kwamba sasa tutakapokuwa tumemaliza stage hii tunakuja stage hii, ili tuweze kuzifanyia assessment, hata tunapokuja katika Bunge hili, tuna uwezo wa kusema kwamba, okay, kwa namna tunavyokwenda basi, mradi huu utakuwa umekamilika kwa kiasi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi jinsi tulivyo, tunashindwa kufanya assessment kwamba sasa huu mradi umefikia wapi? Labda ningependa tu Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hili, tujue kwamba sasa huu mradi hasa hasa unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, kuna changamoto ambazo huwa zinaelezwa kwenye hotuba mbalimbali za Waheshimiwa Mawaziri, mwaka 2016/2017 na 2017/2018, lakini naamini kwamba zile changamoto ziko ndani ya uwezo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali ifanye jitihada na safari hii ije na majibu kwamba sasa mradi huu unaenda kwa stage hizi, mpaka itakapofikia muda fulani huo mradi utaanza, kwa sababu maswali yamekuwa mengi sana. Ikumbukwe tunaambiwa kwamba huu mradi ni wa kimkakati. Kwa hiyo, naamini mradi wa kimkakati ni lazima upewe kipaumbele kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tulivyo hatuna uwezo hata wa kutoa majibu sahihi kwa wananchi wetu wanapokuwa wanatuuliza kwamba huu mradi utaanza lini? Kwa hiyo, naamini kwamba Serikali itakapokuja basi, itakuja na majibu ili kuona namna gani ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mradi wa barabara ya Itoni – Njombe, Ludewa – Manda. Mradi huu vilevile una impact katika ile miradi mikubwa ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga, lakini unaenda kwa utaratibu mno. Hii barabara imepangiwa lots nne; mpaka sasa hivi tupo kwenye ile lot ya kwanza tu. Kwa hiyo, unakuta sasa inatuchukua mwaka wa pili ule mradi toka uanze, lakini barabara hii bado haijakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu hii barabara ni muhimu kwa ajili ya kufungua uchumi wa nchi, Serikali sasa itupatie na lot nyingine, hasa ile lot ya kuanzia pale Njombe kuja Lusitu ili tuweze kuona kwamba sasa ile miradi tunayoizungumzia ya Mchuchuma na Liganga inaweza ika-take off kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuimarika kwa miundombinu hiyo ya barabara itawezesha wananchi kujiandaa na ujio wa hiyo miradi. Kwa sababu impact ya miradi ile inatarajia kuleta watu wasiopungua 300,000 ndani ya Ludewa na Mkoa wa Njombe kwa ujumla wake. Kwa hiyo, maana yake ita-stimulate uchumi, mazao ya wakulima wetu yatapata tija, kwa maana ya bei na kwa maana ya mzunguko wa biashara. Kutakuwepo na usafirishaji wa aina nyingi na barabara zitakazotumika ndiyo hizi ambazo tunazizungumzia sasa hivi na pia tutaanzisha hivyo viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa ambazo tutakuwa tunazizalisha kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuisihi Serikali na kuiomba kwa moyo mkunjufu kabisa, ituongezee lot ya pili kwenye barabara ya Itoni – Njombe, Ludewa – Manda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye eneo la afya. Kwenye eneo la afya tuna upungufu mkubwa sana wa wahudumu au wafanyakazi wa afya. Kwa kweli, tatizo hili limeshakuwa kubwa na bahati mbaya zaidi ni kwamba hata ujenzi unaoendelea kwenye maeneo mbalimbali bado unahitaji sana nguvu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, sasa hivi kule kwetu Ludewa tunajenga Vituo vya Afya 17 na sasa hivi vipo kwenye viwango mbalimbali; na hizo zote ni nguvu za wananchi. Wananchi wale wana uwezo wa kujenga mpaka kufikia kuezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali sasa hebu itupie jicho kule, ikiwezekana iwasaidie hawa wananchi na wadau mbalimbali ambao wanashughulika na ujenzi wa hivyo Vituo vya Afya. Wananchi wameingiwa na hamasa kubwa kwa ajili ya utekelezaji ambao Serikali inaufanya. Kwa hiyo, naamini kwamba wakiungwa mkono ile sera au Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayozungumzia Kituo cha Afya Kila Kata, ina uwezo wa kutekelezwa kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye upande wa elimu, bado tuna upungufu mkubwa wa Walimu katika nchi nzima. Tuna upungufu wa Walimu 90,000 nchi nzima kwa data ambazo tunazo sasa hivi. Kwa hiyo, Serikali ijaribu kuona uwezekano wa kupata Walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la juu ya ubora wa elimu ambayo inatolewa sasa hivi. Ukijaribu kuangalia kwa kiasi kikubwa, matokeo mabaya yanayoipata nchi sasa hivi kutokana na hii mitihani ya NECTA, vilevile inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa Walimu. Kwa hiyo, wakati mwingine tunaweza tukawalaumu wanafunzi, lakini vilevile kuna tatizo la msingi kwa Walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali, umeshafika muda sasa kwa sababu, elimu ni profession kama zilivyo professions nyingine za Uhasibu au Sheria, tuunde sasa chombo madhubuti, Teachers’ Profession Board, ambacho kila Mwalimu atakapokuwa ame-graduate, lazima apite huko kwa ajili ya kupata utaalam zaidi na kupimwa, kufanyiwa assessment kabla hajaenda kuwafundisha watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini tukishafanya hivyo, tutapata quality ya Walimu ambao ni wazuri na product itakayotoka kwa wanafunzi wetu, itakuwa ni product nzuri. Ilishafika wakati kwamba Ualimu ilikuwa ni kimbilio la kila mmoja. Kwa hiyo, lile kimbilio la kila mmoja nadhani sasa hivi wakati wake umeshapita. Kwa hiyo, nashauri tupate chombo madhubuti kitakachosimamia quality ya elimu. Kwangu nashauri tuwe na Teachers’ Profession Board.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado miundombinu ya shule zetu ni chakavu. Wananchi wanajitahidi na wanaendelea vizuri na ile dhana ya kusema elimu bure imeleta sokomoko kubwa kwa wananchi wetu. Hivyo, bado naiomba Serikali na sisi Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu, tujaribu kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili baadhi ya yale mambo ambayo hayapo kwenye elimu bure, basi wananchi wetu wayachukue na ile itawatengenezea ile sense ya ownership.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwambia mtu elimu bure kila kitu, anaondoka na anaacha kila kitu. Tukitengeneza ile sense ya ownership, maana yake mtu anajua kile kitu ni chake na atakuwa na uwezo wa kukisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi.