Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niwe mtu wa kwanza kuanza kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la elimu. Naishukuru tena Serikali kwa namna ambavyo imeanzisha mpango wa elimu bure, hivi sasa wanafunzi wamekuwa ni wengi sana katika mashule yetu. Kuna shule kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Makambako; Shule ya Ikwete, Shule ya Mashujaa na Shule za Juhudi. Shule hizi ni za siku nyingi, zimechakaa sana majengo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa namna ya kipekee kabisa ikishirikiana na wananchi nami Mbunge wao pamoja na Waheshimiwa Madiwani, tuone namna gani tunajiimarisha kuweza kujenga shule hizi ili zifanane na shule nyingine ambazo zipo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la pili la afya. Naipongeza sana Serikali kwa dhati kabisa kwa kazi nzuri inayofanya katika maeneo yetu kwa kutenga fedha nyingi kupeleka katika Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali. Kazi hiyo ni nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, katika Halmashauri ya Mji wangu wa Makambako tuna Kituo cha Afya kimoja, kinachoitwa Lyamkena. Tunaomba na sisi pia tupewe fedha kama ambavyo zimepewa Halmashauri nyingine ili nasi Kituo cha Afya hiki kiweze kufanya kazi za upasuaji na kama ambavyo vituo vingine vinafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha ambazo wamenipa kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Mji wa Makambako. Naishukuru sana. Pia katika Hospitali ya Mji wa Makambako niiombe Wizara au Serikali, Kituo cha Afya kilipandishwa hadhi tangu mwaka 2013 na kuwa hospitali, lakini mgao wa dawa bado tunapata kama Kituo cha Afya wakati ni hospitali. Naiomba sana Serikali itupe mgao wa dawa kama hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni maji. Naipongeza Serikali kwa dhati kwa namna ambavyo imenipa fedha za miradi katika Kijiji cha Ibatu, Usetule, Mtulingala, Mahongole na Mbugani - Nyamande, Kiumba na Ikelu. Hivi sasa shughuli za maji kule zinaendelea. Naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inataka kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali, kuna mradi mkubwa ule wa fedha za kutoka India ambazo zilitengwa kwenye bajeti. Mradi ule wa miradi 17, Tanzania Bara miradi 16 na Zanzibar mradi mmoja (1). Katika miradi hiyo na Makambako ipo na Njombe Mjini ipo na Wanging’ombe ipo. Naomba kujua, ni kitu gani kinakwamisha mradi huu usianzishwe? Kwa sababu tulipata taarifa wakati fulani, alikuja Waziri wa India pale Ikulu, alisaini mkataba huu. Tatizo ni nini? Kimekwamisha kitu gani mradi huu hauanzi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ione namna ambavyo itaanzisha mradi huu wa fedha za kutoka India ili kutatua tatizo la Mji wa Makambako katika suala hili la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu ujenzi. Alipokuja Mgombea ambaye ni Rais sasa, katika Mji wa Makambako, alituahidi kutupa kilomita sita za lami katika Mji wa Makambako. Mpaka sasa hata kilomita moja haijaanza. Kila nikiongea na Mheshimiwa Waziri, amekuwa akiniambia kwamba safari hii ilitengwa kilomita mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali angalau wangeanza kwa kilomita mbili hizi, angalau katika Mji wetu wa Makambako, ungekuwa ni mji unaopendeza kupitia barabara zake za lami. Siyo hivyo tu, naiomba pia TARURA, katika Mji wa Makambako kuna barabara ya kutoka pale Makambako kwenda Maguvani. Maguvani ni eneo la sekondari, pana korongo kubwa katikati. Naiomba Serikali itupe fedha za dharura kwa sababu hivi sasa wanafunzi wanaotoka ng’ambo kwenda katika shule hii ya Sekondari ya Maguvani wanazunguka Mjini Makambako ambako ni kilomita 10 wakati pale ni kilomita moja na nusu tu. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ione namna ya kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA vile vile, tuna stendi ya Mji wa Makambako. Stendi ile ndiyo stendi kubwa lakini maji yote yanapotiririka yanakwenda kwenye majumba ya watu na nyumba kadhaa zimeanguka. Naiomba Serikali ituwekee makalavati ambayo yatanusuru nyumba hizi za wananchi katika stendi kuu ya Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alipokuja Rais katika Mji wa Makambako alituahidi kutujengea uwanja wa mpira. Tumeshaandaa uwanja na mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Naiomba sana Serikali kuona namna ya kutimiza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais kwa wananchi. Kila wakati tumekuwa tukiwaambia kwamba muda bado, tunaiomba sasa Serikali ichukue jukumu la kuhakikisha uwanja huu unajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwenye suala la umeme kwa nchi nzima na hususan katika Halmashauri yangu. Vijiji vingi sasa Mkandarasi yuko site anaendelea kuweka nguzo. Naipongeza sana Serikali kuona sasa katika vijiji vyote vya Halmashauri ya Mji wa Makambako vitapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, katika Kijiji cha Kifumbe kwenda Kijiji cha Mtanga ni kilomita tano mpaka sita. Shughuli hii Mkandarasi anayoendelea nayo, kijiji kitakachobaki katika ukanda huo ni hicho peke yake. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, ione namna ya kuona kijiji hicho nacho kinaunganishwa katika awamu hii inayoendelea hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ione namna ya kuanzisha mashamba kwa ajili ya mbegu mbalimbali za kilimo hasa mahindi katika ukanda wetu. Tatizo la mbegu limekuwa ni kubwa sana. Utaona wakati fulani baadhi ya watu wamekuwa wakichakachua mbegu, ni kwa sababu mbegu hizi ni chache. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ione namna ya kuanzisha mashamba kwa ajili ya mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Mawakala waliosambaza pembejeo. Hivi sasa ni zaidi ya miaka mitatu, hawajalipwa. Naiomba Serikali kama kuna baadhi ambao walifanya kazi nzuri katika kufuatilia na katika kuhakiki, basi walipwe. Wale ambao walichakachua wakafanya udanganyifu waambiwe kwamba ninyi hamlipwi kwa sababu mmefanya udanganyifu, lakini wale waliofanya vizuri walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu fidia kwa soko la Kimataifa, Makambako. Wale watu sasa imekuwa ni tatizo kubwa. Naiomba Serikali, wakati fulani wameandamana, wamejaa kwenye mafuso kwenda Dar es Salaam na wakasema watashuka pale Ikulu, kama kuuawa wauawe. Nilimwambia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nilimwambia, nikawasihi. Naiomba sana Serikali, chonde chonde tuone namna ya kuwalipa fidia hawa watu. Zaidi ya miaka 21 sasa hawajalipwa fidia, kwa hiyo, imekuwa ni tatizo kubwa sana. Naomba sana walipwe fidia watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wakati nachangia suala la Mambo ya Ndani, naomba niseme kama ifuatavyo: Makambako ndiyo center. Unapozungumzia kwenda Mbeya, Makambako ndiyo center; unapozungumzia kwenda Songea, Makambako ndiyo center; unapokwenda Iringa, Makambako ndiyo center. Ni center wakati fulani baadhi ya wahalifu ndiyo wanakimbilia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hata wale waliokuwa wanafanya uhalifu kule Kibiti walipatikana baadhi ya wawili, watatu pale Makambako. Nikaenda mimi pale Polisi wakaniambia Mheshimiwa Mbunge njoo uwaone watu hao. Walikimbia kumbe wakaenda Songea. Walipoona Songea msako mkali, wakakimbilia Makambako. Kwa hiyo, naomba sana, tuone katika magari yatakayokuja ambayo Mheshimiwa Waziri jana alisema, katika mgao tuone… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)