Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi yangu. Nami nashukuru kupata fursa ya kuchangia kwenye bajeti hii kuu nikiwa nataka kujielekeza kwenye mambo manne ambayo nahisi yanaweza kuisaidia Serikali lakini kumsaidia Waziri sasa kuweza kujipanga zaidi katika kuhakikisha anapata mapato ya kutosha kutokana na vyanzo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwanzo ninalotaka kuzungumza ni suala zima la bandari bubu na magendo yanayofanyika kwa bandari zetu kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Biashara kubwa inayofanyika hapa ni mafuta ya kupikia. Hii biashara imekuwa ni kubwa na kama nchi hakujawa na utaratibu mzuri wa kudhibiti hizi bandari lakini kudhibiti zile bidhaa zinazoingia pale Zanzibar na kutawanywa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii inafanyika kupitia bandari ndogo ndogo mbalimbali na kushushwa katika bandari ndogo ndogo hapa Dar es Salaam na bidhaa nyingi zinazosafirishwa ni mchele, mafuta, sukari, mafriji yale used, redio, mipira used kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kinaikosesha Serikali mapato. Hii imetokana na mfumo mzima ule wa ukusanyaji mapato kule Zanzibar, double tax, ndicho kitu kinachosababisha wafanyabiashara kukimbia kulipa kodi mara mbili katika bandari yetu ya Dar es Salaam. Kwa sababu wao wanaleta bidhaa pale Zanzibar wakishashusha kwenye makontena wanalipishwa ushuru, TRA wanachukua chao na ZRB wanachukua chao, lakini mtu yule yule akisafirisha mzigo ule kuuleta bandari ya Dar es Salaam analipa tena kodi mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie wazi Mheshimiwa Waziri, kiwango kikubwa cha bidhaa zile au mafuta yanayoingia Tanzania Bara asilimia 80 yanapitia Zanzibar. Hiyo ni taarifa rasmi naomba aifanyie kazi na si hivyo tu, mipira used na vifaa vingine used vinavyoletwa kutoka nje vinashushwa tu Zanzibar lakini vinaishia Tanzania Bara na maeneo mengine kwa njia za panya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kujipanga sasa kuhakikisha hii kero inayotajwa kila siku kwamba tumemaliza tatizo la tozo ya ushuru wa mara mbili kwa biashara au kwa bidhaa zilizoko Zanzibar zinazoingia Bara bado halijamalizika na imekuwa maneno ya kila siku. Hili nimwombe Waziri ulifanyie kazi na tufike mahali iwe mwisho wa hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia eneo lingine ambalo Serikali bado ina nafasi kubwa ya kuwekeza na kuweza kujipatia mapato mengi. Nimeangalia bajeti vya kutosha lakini bado wito wetu tunaoutoa na kulia kila kwenye suala zima la uvuvi wa bahari kuu na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata samaki halina kipaumbele. Nimwombe Waziri hesabu za haraka haraka, sasa hivi duniani mpaka juzi nilivyokuwa natembea kwenye mitandao ndani ya soko la dunia kuna mahitaji ya tani 271,000 kwa mwezi za samaki ambazo zinahitajika zikiwa processed ambao ni cane fish.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama nchi ingeweza kuwa na hii tunaita pot fish moja tu au mbili zinaweza kutengeneza ajira zaidi ya watu 30,000 kwa kila meli inayo- land kwa kipindi cha miezi mitatu watu wale wanafanya kazi lakini pato linalopatikana kwa meli moja tumeshawaeleza mara nyingi pale ile process nzima ya meli moja ni zaidi ya dola 85,000, pesa zile zinakuwepo ndani ya nchi, zinasaidia Watanzania na watu wengine. Vilevile bahari yetu tumeshaeleza mara nyingi jamani, hivi sasa pamoja na mazingira mengine yaliyoko katika maeneo mengine current ya maji katika maeneo yetu ni very conducive kuliko maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Namibia current imechafuka, Mozambique current imechafuka, Tanzania current ni conducive. Kwa hiyo, stock kubwa ya samaki imekusanyika katika maeneo yetu na ndiyo maana meli nyingi za nje zinakimbilia kuvua katika maeneo yetu kwa sababu kuna mazingira rafiki ya kuishi. Si hivyo tu, wenzetu wa Philippine na Mataifa mengine ya nje yanakuja kumwaga vyakula katika maeneo ya Tanzania ili kuwavuta samaki kuwepo kwa wingi na kuvuna samaki wale kwa njia ya kirahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu nyingine tuendeleze uvuvi mpya unaoingia hivi sasa wa kutengeneza uvuvi wa kutumia cadge. Utafiti tayari umeshafanyika na cadge fishing imeonekana kuwa na mafanikio makubwa. Leo hii wavuvi wetu wengi walikuwa wanavua majongoo kwa kutumia gesi lakini leo baada ya kufanyika utafiti, wavuvi hawa wanaweza kuvua kwa kutega cadge tu ndani ya deep sea na cadge moja ina uwezo wa kuingiza mpaka milioni 24 kwa mvuo mmoja tu wa kipindi ambacho utaweza kufuga wale samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kusiwe na mipango mahsusi kuwawezesha wananchi hawa, wakawa na vyombo vya kisasa wakaweza kwenda kuweka cadge zao katika deep sea, wakavua kwenye deep sea na tukaweza kupata samaki wa kutosha lakini tukaanzisha viwanda vya kuchakata samaki na kufunga na kusafirisha nje, wakati soko sasa hivi linatafuta bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulisema ni kwamba bado tuna tatizo kwenye kilimo. Tunasema kilimo tumekipa kipaumbele lakini bado sijaona mikakati halisi ya kusaidia kilimo cha Tanzania kikaweza kuonesha mafanikio na kuwasaidia wakulima wengi katika nchi yetu. Nitoe mfano mmoja wa kahawa bado kuna urasimu katika soko la kahawa, soko la kahawa lazima uende Moshi, lakini tuna kiwanda kipo Mbinga kilianza kuchakata na kutengeneza Mbinga Instant, kahawa ile ikawa imepata soko kubwa tu katika nchi mbalimbali zikiwemo Ulaya hata Zanzibar na maeneo mengine lakini bado Serikali haikutoa msukumo wa kufanya eneo lile likaweza kuzalisha na kufanya canning ile kahawa iliyoko katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeweza kukianzisha kile kiwanda cha Mbinga kingehamasisha kilimo cha kahawa katika maeneo yote yale ya Mikoa ya Ruvuma lakini hata maeneo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara yale ambayo yanakubali kahawa ingeweza kuzalishwa, lakini Njombe ingepata fursa kubwa zaidi ya kuzalisha kahawa na ikaingia katika ramani ya maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa wa kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe vitu kama hivi Serikali itie mkono wake si tu kuiachia pengine kampuni au Halmashauri na wananchi wenyewe wakaweza kufanya kitu kama kile, lakini ile ile ingesaidia urasimu wa kutoa kahawa Mbinga kuipeleka sokoni Moshi. Vilevile ungesaidia urasimu wa kutoa kahawa Mbozi ukaipeleka Moshi, tunapoteza gharama kubwa ya uzalishaji bila ya sababu wakati huku tunasema Serikali inaondoa tozo lakini tunaanzisha tozo nyingine ambazo tunaweza kuzipunguza na... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)