Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwa muhtasari tu hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa na za dhati na za makusudi katika kuhakikisha nchi hii inafikia malengo yake ya kujitegemea kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuomeona hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ilivyoainisha na kuonesha makusudio mazima na dhamira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutaka kufanya nchi hii wananchi wake waendelee kukiamini Chama kinachotawala sasa, Chama cha Mapinduzi kwa maana ya CCM. Ndiyo chama ambacho huwezi kuacha kuihusisha nchi hii na chama hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake ya Wizara ya Fedha kwa kuona na kutambua wananchi wanyonge ambao walikuwa wananyanyasika kwa kusumbuliwa sana na hususan katika kodi mbalimbali hizi ndogo ndogo, ikiwemo ya kusafirisha mazao kidogo chini ya tani moja, kutoka Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine, lakini kutambua sekta isiyo rasmi ya akinamama Lishe na wajasiriamali wadogo wadogo ili nao wawe na mchango katika uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuishauri Serikali kidogo hasa katika kuhakikisha nchi inajitegemea katika suala zima la chakula. Ni vizuri sasa tukaanza kufikiria na kuondokana na utegemezi huu wa kilimo kinachotegemea mvua. Nchi hii tumekuwa tunategemea sana kilimo kinachotegemea mvua. Skimu za Umwagiliaji ziko kidogo sana na ziko maeneo ambayo yana uasilia wa mito labda na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sasa tukatengeneza miundombinu ya makusudi, yakiwemo mabwawa madogo madogo kwa maana ya malambo, kuhakikisha wananchi sasa wanalima kilimo cha umwagiliaji kutokana na hali ya hewa ambayo inabadilika badilika. Kumekuwa na changamoto ya tabia ya nchi, wananchi wetu na maeneo yetu mengi, ikiwemo mwaka huu maeneo mengi ya hali ya chakula siyo nzuri sana, ikiwemo Mikoa ya Kati, hata Mikoa ya Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya juhudi za makusudi za Serikali kuwekeza katika kilimo hiki cha umwagiliaji. Ni vizuri sasa na sisi tutoke tukajifunze kwa baadhi ya nchi zilizofanikiwa nchi ambazo zilikuwa maskini wenzetu lakini sasa wametoka kabisa huku ambako tupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kusaidia wakulima ambao ndio wengi katika nchi hii, lazima tuhakikishe mbolea yetu inawekewa ruzuku. Kulikuwa na mpango hapa wa Waziri wa Kilimo aliyekuwa ametoka kwenye nafasi yake sasa amepewa Wizara nyingine ya kulinda watu wetu na mali zao; ni kwamba kulikuwa na mpango wa kuhakikisha mbolea yote ambayo inaingia katika soko inawekewa ruzuku. Hii itaondoa kufuatanafuatana; kazi kubwa itakuwa ya kudhibiti kwamba hii mbolea sasa badala ya kutumika ndani isitoke tu nje ya mipaka yetu, iuzwe kama bidhaa nyingine ambazo mkulima anaweza kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na ruzuku ya mbegu iwe wazi iingie masokoni ili mkulima akienda kwenye duka, mbegu iwe tayari ina ruzuku. Kama Serikali haitathubutu bado wakulima wa nchi hii wataendelea kusumbuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nchi hii tuna tatizo la maji. Naomba Serikali ifanye juhudi za makusudi mazima kuhakikisha upatikanaji wa maji vijijini. Tumediriki sana katika miji yetu mingi, tumeona juhudi kubwa za Serikali kupitia Wizara ya Maji kuhakikisha miji inapata maji, lakini vijiji vingi vina tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Serikali ifike mahali ione na ichukue mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Wameongeza Sh.40/= katika kuhakikisha tunaziba mapengo ambayo yatatokana na misamaha ambayo wametoa. Naomba basi iongezeke hata Sh.10/= tu ambayo itasaidia kuongeza katika Mfuko wa Maji ili miaka hii iliyobaki tuweze kutekeleza vizuri ilani ya chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina dhamira njema ya kuunganisha Mikoa yote kwa lami, ukiwemo Mkoa wa Singida ambao natoka mimi. Tuna nia ya kuunganisha Mkoa wa Singida na Mbeya, kunabaki kilomita 413. Kilomita hizi ni nyingi. Naishukuru Serikali kwa kuanza kutaka kujenga sasa kilomita 56.9 kutoka Mkiwa, Itigi hadi Noranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hii ya Ujenzi, kwamba ukijenga kilomita 57 hizi takriban, bado utakuwa umebakiza kilomita 300 na zaidi. Ikiwezekana, ni vizuri basi speed ikaongezeka, lakini Waziri wa Fedha aone, awasaidie. Ule Mradi Mkandarasi hadi sasa hajafika, hatumjui mpaka sasa hivi, lakini tunaambiwa tunajengewa kilomita 56.9 takriban kilomita 57.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu kupitia daraja la Simbiti ni jambo ambalo tunataka tuone sasa wananchi wa Mikoa hii wanasafiri lakini wanapita katika barabara kama wenzao wanaotoka maeneo mengine. Napongeza kwa sasa kumalizia kipande cha barabara ya kutoka pale Chaya mpakani kwenye Mkoa wa Tabora maeneo ya Nyahuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeze Serikali pia kwa kusimamia kutaka kujenga reli hii ya Kati, kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, lakini dhamira ni kufika Makutupora katika Mkoa wetu wa Singida. Vile vile kuna reli hii ya Kati ambayo ni kutoka Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza, ina tawi lililoanzishwa na Mheshimiwa Mwalimu Nyerere Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa hili kutoka Manyoni kwenda Singida, haizungumzwi hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ilikuwa na msaada mkubwa katika uchumi wa nchi hii. Sisi ni wakulima na kulikuwa na mashamba ya NAFCO. Kule Basutu yalikuwa yakipita pale inarahisisha kufika kwa walaji wengi ambao ni miji mikubwa lakini kwenye viwanda kule Dar es Salaam. Ni vizuri sasa mkaanza kufikiria reli hii ya Manyoni – Singida nayo iwe katika kiwango kizuri; lakini wameanza kung’oa hadi mataruma. Sasa sijui uwekezaji ule nchi inaenda namna gani? Naiomba Serikali iangalie kipande hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kidogo kuhusu suala zima la hifadhi ya chakula. NFRA wametengewa hela mwaka huu, lakini hapa nyuma tumeshuhudia maeneo mengi yanapata upungufu wa chakula lakini msaada na namna ya kuwahami wananchi wetu unachelewa sana. Leo hii tumeanza kutoa eti chakula cha bei nafuu wakati tayari watu wameshavuna. Naiomba Serikali kwa makusudi mazima, panapokuwa na upungufu wa chakula, basi zichukuliwe hatua za makusudi kusaidia watu wetu waweze kulima na kurudi tena mwaka mwingine usiwe na njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anapokutana na hali ya uhaba wa chakula, hawezi hata kufanya kazi zake za kila siku. Kwa hiyo, tunatengeneza mazingira ya janga kubwa zaidi kama hatutaweza kutumia akiba ya chakula ya Taifa kuwanusuru wananchi wanaokutana na tatizo hili. Hii imetokea sana miaka hii miwili ambapo nami nimeona nikiwa Mbunge kwamba hazichukuliwi hatua za haraka, wanaposaidia wananchi, wanapewa chakula kile wakati tayari wameshaumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nisemee kuhusu ujenzi wa Zahanati kila kijiji na ujenzi wa Kituo cha Afya kila Kata; ni ahadi yetu ya uchaguzi. Sasa sijui tukirudi tutakuja kusema nini? Naomba sasa juhudi za makusudi angalau tufikie nusu ya yale ambayo tuliahidi.

(Hapa kengele ilia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.