Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii iliyoko mbele yetu. Ni ukweli usiopingika kwamba haiwezekani mtu mwenye nia ya dhati na mzalendo kwenye Bunge hili ukasimama bila kuanza kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nilipokuwa natazama kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, niliona jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais hakukurupuka kwenda kuzuia madini yetu kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Ilikua ni sehemu ya vipaumbele ambavyo Mheshimiwa Rais alivizungumza alipokuwa hapa Bungeni akihutubia tarehe 20 Novemba, 2015 na habari ya madini ilikuwa kipaumbele chake Namba nne (4).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya. Hawa wanaosema jana amemkaribisha mwizi Ikulu, yaani tunasema hiyo ni danganya toto, maana Mheshimiwa Rais alisema anakaribisha wahusika kwenye meza ya majadiliano, wala hakuandika invitation letter ya kumleta yule Mwenyekiti hapa. Watu walijipima wenyewe, wakaona jinsi gani tumetiwa hasara na Makampuni yao hayo, wakaona wabebe mzigo huo wa kuja ku-negotiate mambo yaliyofanyika ya kutia nchi hii hasara na Rais wetu na mambo haya yamefanyika hadharani. Kwa hiyo, hawa ndugu zetu wakikosa la kusema, ni bora wakati mwingine wakanyamaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme, watu hawa mara nyingi wanawasumbua hawa Waheshimiwa Mawaziri kwa maswali na vitu vingine vya namna hiyo na michango Bungeni humu wakihitaji Serikali kupeleka mahitaji kwenye Majimbo yao; wanahitaji elimu, maji na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa, kama siyo Mheshimiwa Rais ameamua kuchukua jukumu hili zito la kujitoa muhanga akaamua kutetea rasilimali kwa ajili ya wananchi wa nchi hii, hivi hawa watu hayo mahitaji muhimu ya watu wao watayatoa wapi? Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na tunaendelea kumwombea Mungu aendelee kumpa maisha marefu, maana ana mpango wa kututoa mahali tulipo kwenda mahali pengine. Ni sawa na Musa alivyowatoa wana wa Israel kwenye nchi ya utumwa ya Misri na kuwapeleka Kanaani. Ndicho anachokifanya Mheshimiwa Rais kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa bajeti nzuri sana ambayo imekuja mbele yetu. Tunafahamu kwamba kazi kubwa inafanyika. Naipongeza na timu nzima ambayo iko chini ya Wizara hii ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza habari hii ya bajeti, naomba nianze na suala la makusanyo ya mapato. Naipongeza pia Serikali kwa sababu sasa imechukua hatua ya kuweza kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa fedha hasa katika Halmashauri na maeneo mengine mbalimbali nchini. Ninachokiomba na kuishauri Serikali yangu ni kwamba, katika mgawanyo huu sasa wa ile Keki ya Taifa baada ya makusanyo haya kufanyika, basi mgawanyo wa Keki ya Taifa uweze kwenda sawia kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikizungumza hili, naomba nizunguzie suala zima la elimu. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kukubali kupeleka katika shule zetu shilingi bilioni 18 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila malipo. Ni kweli na ni dhahiri kwamba watoto sasa wanasoma mashuleni na changamoto zilizokuwepo huko nyuma hazipo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nazungumza hivi, karatasi niliyoibeba mkononi mwangu inaeleza orodha ya shule ambazo zitakarabatiwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ile bajeti ya 2016/2017. Nitoe masikitiko yangu kwamba Mkoa wa Manyara shule inayokwenda kukarabatiwa ni moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama Mikoa mingi; Dar es salaam na Mikoa mingine, kila mtu aliiona hii karatasi. Kuna mikoa imepata bahati ya kukarabatiwa shule saba, sita, nane au nne lakini Mkoa wa Manyara tunakarabatiwa shule moja tu ya Nangwa iliyoko Wilayani Hanang. Naona kidogo hapa haijakaa sawa sawa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Ndalichako katika hili nalo atuangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shule kongwe, tuna shule inaitwa Endagikoti ambayo iko Wilayani Mbulu, ilianzishwa mwaka 1929, tuna shule iko Mbulu inaitwa Dawi, imeanzishwa mwaka 1917; hizi shule ni kongwe. Masikitiko mengine ni kwamba, hatuna high schools kwenye Mkoa wa Manyara. Tuna high schools chache mno, mfano Wilaya ya Simanjiro haina high school hata moja; Hanang haina high school hata moja; Wilaya ya Mbulu ina high school mbili. Kwa hiyo, naomba, kwa sababu kipaumbele cha kwanza cha Mtanzania ni elimu na tukimkamata huyu elimu tukaacha kumwacha aende zake, watoto wetu watakombolewa. Naomba sana kwa hili tukumbukwe katika Mkoa wa Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru na kuipongeza bajeti hii kwa kuwa inatambua akinamama; Mama Lishe, akinamama wanaofanya biashara zao ndogo ndogo na vijana hawa Wamachinga, hili ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu kutambua hili. Wakati haya ya kurasimisha biashara zao yanafanyika, naiomba Serikali iangalie namna gani itakusanya kodi kwenye Makampuni makubwa ambayo hayakusanyi kodi inavyotakiwa ili ikiwezekana hawa watu wapewe baada ya kutambuliwa na kupewa maeneo ya kufanyia biashara zao, waweze kupatiwa muda wa kutosha ili kwamba sasa ifikie mahali nao waweze kuchangia kodi. Siyo kwamba wanapewa maeneo na wakati huo huo basi wanaanza tena kutozwa kodi wakati wanakuwa hawajajijenga vile inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema bado tuna vyanzo vingi vya kodi vinavyoendelea kupotea; kuna Makampuni makubwa ambayo yanakwepa kodi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, juzi hapa alizindua data center kwa ajili ya collection ya mapato yote yanayotakiwa kukusanywa katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya Makampuni makubwa kama ya simu, Makampuni ya uchimbaji ambayo yamehodhi vitalu vikubwa kwa ajili ya uchimbaji lakini hawachimbi, vitalu hivyo vimekaa tu. Naomba Serikali ifanye tathmini ya kutosha waone kwamba Serikali inakwenda kufaidika na nini. Najua Mheshimiwa Rais ameshaanza hili na nina hakika tunakwenda kufanikiwa siku zijazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusisahau pia kwamba tatizo kubwa la maji bado lipo pale pale. Hatukuona ile Sh.50/= ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameipigia kelele humu ndani ya kuongezwa kwenye mafuta ili kwamba tuweze kumtua mama wa Kitanzania ndoo kichwani. Bado naendelea kuililia na kuiomba Serikali yangu itazame hili kwa jicho la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wengi ambao ni wazalishaji na wachangiaji wa uchumi wa mapato ya nchi hii, wanapoteza muda mwingi kwenye kutafuta maji. Tunaomba ile Sh.50/= iongezwe kwenye mafuta ili kwamba tuweze kumtua mama ndoo kichwani. Wakati huo huo, Mkoa wa Manyara ni Mkoa wa wafugaji; tuna Kata kama za Ndedo kule Kiteto; kata nyingi tu za pale Kiteto, Simanjiro, Kata za Dongo, Kijungu, Lolera, Olboloti; Kata hizi hazina maji kabisa ya bomba wala mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ikiwezekana watu hawa wapate kuchimbiwa mabwawa. Juzi tulikuwa na mafuriko ya kutosha hapa nchini. Naiomba Serikali yangu kupitia hizi Halmashauri zetu, wahakikishe hawa watu wanachimbiwa mabwawa wakati ambapo mvua imesimama kama hivi, ili nyakati za mvua tuweze ku-track yale maji yaende kwenye hayo mabwawa kupunguza hii changamoto ya maji. Mbona ni rahisi! Kwa hiyo, naomba hasa maeneo ya Kiteto na Simanjiro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya ya Hanang’ tunahitaji mabwawa pia, maana nako katika zile Kata tuna wafugaji wengi tu. Tukiweza kuwawekea wafugaji hawa maji kupitia mabwawa, wataacha kuhamahama, watakaa kwenye maeneo yao, maana rasilimali za kutosha zitakuwepo pale, maji pamoja na mambo mengine wanayoyahitaji. Naomba sana Mkoa wa Manyara ukumbukwe katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna matatizo ya mawasiliano baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kiteto, tuna shida katika Kata za Ndedo pamoja na Makame. Bado watu hawa wanaishi ile karne ya kupanda juu ya miti ili uweze kuzungumza na ndugu yako aliyeko upande mwingine. Kwa hiyo, namwomba sana Waziri husika ama Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii aikumbuke Wilaya ya Kiteto na maeneo mengine mengi tu ya Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia masuala mazima ya mazingira ya ulipaji kodi. Naishauri sana TRA; naishauri Wizara ya Fedha waweze…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.