Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa fursa hii. Naanza kwa kuwashukuru sana viongozi wa Wizara yetu hapa, Mheshimiwa Dkt. Mpango kama Waziri, Naibu Waziri wake Dkt. Kijaji, Katibu Mkuu pia Doto James, Naibu Katibu Mkuu, Wataalam wote wanaoongoza Tume ya Mipango na Watendaji wote katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili bajeti hii sisi ni wawakilishi kutoka maeneo mbalimbali. Mojawapo ya mambo yanayotuongoza kutafakari na hatimaye ama kuikubali ama kutoikubali bajeti hii ni pamoja na kuona mambo ambayo yamezingatiwa katika maeneo yetu ya kazi tunakotoka pamoja na mambo ya Kitaifa. Naanza kwa kusema naungana na wale wote ambao wanaiunga mkono bajeti hii asilimia mia moja kwa sababu, kule Jimbo la Sengerema ambako mimi nawakilisha, yako mambo ambayo yamejitokeza moja kwa moja kwenye bajeti hii na nitasema kwa ufupi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwa nini naiunga mkono bajeti kwa sababu, naona sekta ya maji. Nampongeza sana Mheshimiwa Injinia Lwenge na Msaidizi wake kule Sengerema ule mradi mkubwa kabisa ambao unaongoza kwa ngazi ya Halmashauri na Wilaya Tanzania umeshakamilika sasa uko hatua za mwisho mno. Baada ya hapa nina hakika kwamba Viongozi Wakuu wa Serikali watakwenda kuuzindua na mimi nawakaribisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule sasa unapokamilika tunaanza kuufungua kuwafikishia maji wananchi wanaozunguka Mji wa Sengerema na maeneo mengine. Sio hivyo tu, kuna miradi kadhaa imebuniwa inayotokana na chanzo cha Ziwa Victoria. Kwa hiyo, hivi tunavyozungumza bajeti hii naiona Sengerema imezingatiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kufika Sengerema unapotokea Mwanza lazima uvuke Ziwa. Tuna barabara ya Lami ya Kamanga – Sengerema pale, nimezungumza na TANROADS wametuahidi kwamba, mwaka huu wa bajeti unaokuja, mwaka mpya wa fedha, wataanza kushughulikia ujenzi wa lami. Pia, tuna vivuko, kutoka Mwanza kwenda Sengerema unavuka kwa kutumia njia mbili, kuna Kamanga pale kwenda Sengerema, lakini pia kuna njia ya Busisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale Busisi kuna mambo mawili yanafanyika kuanzia Kigongo, Jimbo la Misungwi; kwanza kuna ununuzi wa kivuko kipya, naipongeza sana Serikali, lakini pia kuna ferry tatu zinafanya kazi pale, zinafanyiwa matengenezo na bajeti imeonesha hivyo. Ndio maana nasema katika mazingira hayo hakuna namna nyingine, isipokuwa kuiunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maandalizi ya ujenzi wa daraja kubwa, kilometa 3.5 unafanyika pale kwenye kivuko kati ya Kigongo kwenda Busisi ambako ni Jimbo la Sengerema. Yote haya ni maandalizi yanayofanywa kupitia bajeti hii ya fedha. Kwa nini wananchi wa Sengerema tusiunge mkono? Tuiunge mkono kwa sababu tunaona tunafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ina mambo mengi, lakini lingine mojawapo ambalo ni baadhi ya mambo machache ambayo yamenifurahisha na mimi naungana na wenzangu ni kuwatambua rasmi wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama Machinga, lakini wanaofanya kazi za kujiendeleza wenyewe na kuchangia uchumi wa Taifa. Ni jambo muhimu na lazima tuliheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imepunguza ushuru wa mazao, kwa sisi tulioko kule vijijini tunafahamu. Inawezekana tukaongea katika lugha tofauti kwa sababu tunatoka maeneo tofauti, watu wa mjini watatuuliza mambo ya mjini, lakini sisi tunaotoka Majimbo ya vijijini tunafahamu kero ambazo zimekuwa zikiwagusa wananchi eneo hili. Kushusha ushuru wa mazao mpaka mzigo uzidi tani moja ni jambo kubwa sana. Tunasema mazao ya biashara ni asilimia tatu na mazao ya chakula asilimia mbili, hili ni jambo kubwa tunaishukuru sana Serikali kwa kuja na mapendekezo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Sh.40/= pale, tumesema kwenye utaratibu wa Road License sasa ziende kwenye maji. Nasema tufanye uamuzi mgumu, lakini kwa sababu naiona neema inakuja labda tusifike huko, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa Shabiby juzi aliongea vizuri sana hapa, kwamba zile Sh.40/= tunazoziongeza zilikuwa kwenye utaratibu wa kawaida, lakini tumekuwa na kilio cha kuongeza Sh.50/= kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Maji kule. Sasa kwa sababu naiona neema inakuja saa nyingine tusifike huko, lakini ukiniuliza mimi ningesema ushauri wangu ni kwamba, hata ile Sh.50/= ambayo tulikuwa tumeikusudia, tuliyoichangia sana kabla ya bajeti hii tuiongeze kule ziende zote kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia na dunia nzima inafahamu, Bunge jana tumetoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kudhibiti na kuisimamia vilivyo bora zaidi sekta ya madini. Naungana na Watanzania wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi aliyofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita nilichangia hapa nikasema kwa hali tuliyofikia sasa hivi tunahitaji tu maamuzi ya usimamizi wa sheria na sera tulizonazo. Moja ya jambo nililozungumza kupitia kile Kifungu cha 11 cha Sheria ya Madini kinaruhusu kabisa kuipitia mikataba hii, lakini nikasema hata ushiriki wa Serikali kuwa na hisa katika makampuni haya kupitia Kifungu cha 10 tunaweza kabisa kuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo haya na nazungumza mimi nikiwa na Kiapo cha Bunge, lakini pia niko chini ya Kiapo cha Serikali, nilishawahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini kwa miaka mitano na nusu. Nazungumza nikifahamu michakato, tungefuata utaratibu wa kawaida wa kuanza mchakato wa kuwaalika wawekezaji tushauriane namna ya kuboresha mikataba hii, ingetuchukua miaka. Mheshimiwa Rais ameturahisishia, jana tumesikia wote na dunia imeelewa kwamba, ndani ya wiki mbili hizi mazungumzo yataanza na upo uelekeo wa kuelewana katika hali ya kuwa na win-win situation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tumepitisha Azimio la kumpongeza Mheshimiwa Rais JPM, lakini ilikuwa ni kabla ya Taarifa ya Mheshimiwa Rais. Kuna utamaduni umezoeleka duniani kwamba mambo makubwa yakifanywa na Viongozi Wakuu wa nchi kwa pamoja, kuna utaratibu na hasa kama hili Bunge, tunaweza sisi, sisi ndio wawakilishi wa wananchi Tanzania nzima. Wapo Wabunge hapa wana simu za kumpigia Mheshimiwa Rais moja kwa moja kumpa pongezi kwa kazi anayofanya, lakini wengine hata namba yake hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaowakilisha wawakilishi wa Watanzania, nilikuwa naliomba Bunge lako dakika moja, tumpe standing ovation Mheshimiwa Rais kwa wale tunaoguswa kuonesha sisi kuguswa kwetu kwa namna ambavyo tumeunga mkono na tumhakikishie kwamba, tuko pamoja. Tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya, tumuunge mkono kwa niaba ya Watanzania wote tunaoguswa na jambo hili, tumhakikishie kwamba vita hii sio ya kwake peke yake ni ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa hilo. Kwa kufanya hivyo, hatufanyi kwa sababu ya favour, lakini kwa sababu ya kutambua kazi kubwa anayoifanya. Kupambana katika sekta hii na mmeona katika mitandao inasemekana zipo familia mbili ambazo zimeamua kudhibiti madini yote duniani, lakini Mheshimiwa Rais anaungana na kundi la viongozi duniani ambao wana uthubutu na wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si jambo la kwanza, tunafahamu historia ya Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere alivyopigana katika mawimbi mazito sana akaifikisha nchi hii hapa, lakini ukienda Marekani kuna Rais yule mnafahamu, Rais Franklin Roosevelt aliikamata ile nchi akaongoza hata zaidi ya kile kipindi ambacho yeye kwa taratibu za Kimarekani kilikuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Franklin aliichukua nchi ikiwa katika hali ngumu sana na akaanzia pale ambapo Marais waliokuwa wamemtangulia, akaivusha Marekani mpaka kifo kilipomkumba. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amejitoa muhanga kwa niaba yetu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda China, Mao Tse Tung kuanzia mwaka 1949 walivyofanya mapinduzi China aliongoza lile Taifa mpaka mwaka 1978 akaja kiongozi, Mwanamapinduzi, akaanzia pale alipokuwa ameishia Mao Tse Tung akaichukua ile nchi, anaitwa Deng Xiao Ping, aliichukua ile nchi ni miaka ishirini na kitu tu, China ikabadilika sana kuanzia mwaka 1978 mpaka 1989 alipokuwa anaachia

nafasi. Kwa hivyo, duniani kunawezekana. Nenda Singapore kuna yule Li Kuyan Yew ameichukua ile nchi akaibeba kutoka ilipokuwa ikafika hapa ilipokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, mambo haya yanawezekana. Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema kwa hii, hatua tulipofikia hapa ni nzuri sana. Pamoja na kwamba, hatujajua tutapata kiasi gani, lakini tunakoelekea ni kuzuri na Mheshimiwa Rais amethubutu na sote tunaungana kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye bajeti. Tunapozungumzia Tanzania ya Viwanda tunazungumzia yako mambo ambayo lazima yafanyike. Huwezi kuzungumzia nchi ya viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika. Nataka niseme ninachokifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu sasa linakwenda kufumuka kwa maendeleo. Unasikia sasa hivi Mheshimiwa Rais jana ametuambia akiwa na Mwekezaji ambaye ni Rais na Mwenyekiti wa Barrick amesema kwamba, pamoja na mambo mengine ambayo tutayajadili ni pamoja na ujenzi wa smelter, kunahitajika umeme mkubwa sana, lakini nimesikia reli itakayojengwa itatumia treni inayoendeshwa kwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Rais wa Rwanda kule amesema wanaisubiri reli hii inakwenda, unahitajika umeme mwingi sana. Unapozungumzia viwanda unazungumzia umeme mwingi, ushauri wangu kwa Serikali, lazima sasa kama ambavyo tumeji-commit kwenye bajeti hii, tuishirikishe sekta binafsi tusaidiane na Serikali kuwekeza katika vyanzo vya kuzalisha umeme, kwa sababu vinginevyo hatutaweza kuhimili hiyo kasi inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, hapa sasa hivi kuna miradi inatekelezwa pale Kinyerezi One mpaka Kinyerezi Six. Naomba, kama inawezekana kwa sababu, wapo Wakandarasi kwa mfano wanaomalizia ile Kinyerezi One, Serikali imeingia nao utaratibu wanajenga, naishauri Serikali wakati tunaishirikisha sekta binafsi pia, inaweza kuwa-engage hawa Wakandarasi kwa utaratibu kwa sababu, ndani ya miaka mitatu tunaweza kufanikiwa kumaliza mradi mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bomba la gesi ambalo limejengwa miaka michache iliyopita na mimi ambaye nilisimamia katika eneo hilo nafahamu, sasa hivi wamesema limetumika asilimia sita tu asilimia 90 haijatumika, inahitaji vyanzo vingi vya kuzalisha huo umeme ili uwafikie wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hii tuna vyanzo vingi vya nishati, tusitegemee gesi peke yake kwa sababu, kwanza gesi ina bei juu kidogo kuliko vyanzo vya maji. Leo hapa tuna Bonde la Rufiji inafahamika, kuna mradi mkubwa wa Stiegler’s Gorge. Nakumbuka mpaka mwaka 2012 tulikuwa tumeshaanzisha mazungumzo na Wabrazil walikuwa tayari kuja kuungana na sisi, una uwezo wa kuzalisha megawatt 2,100. Nchi hii kwa potential tuliyonayo kwenye sekta ya umeme unaoweza kuzalishwa kutokana na maporomoko ya maji ni zaidi ya megawatt 4,600. Naomba Serikali ifunguke kote kule twende tukatumie vyanzo vyote kuhakikisha kwamba, nchi hii inafikia lengo lililokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nirudie tena kusema umuhimu wa sekta binafsi ulivyojionesha, Mheshimiwa Waziri ameonesha utayari huo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante. Mheshimiwa Mbene, ajiandae Mheshimiwa Musukuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono na ahsante sana.