Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia niwapongeze wawasilishaji wote wawili. Nianze na dawa tu tunazotumia binadamu ambapo ni matumaini kwamba kiwango cha ubora wa dawa za binadamu zinafanyiwa utafiti wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masikitiko, baada ya dawa kutumia muda wa miaka mitano au miaka kumi tunaambiwa dawa hizo hasa hazifai zina madhara, hivi hamkufanya utafiti wa kutosha? Leo kuna baadhi ya dawa unaambiwa kabisa dawa hizi chroloquine usitumie tena, metakelfin zina madhara, hivi sisi ndio majaribio ya hizo dawa? Tumeshapata matatizo mengi, watu wameshaathirika na matatizo mbalimbali wanaambiwa sasa ninyi hizo dawa msitumie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wafanye majaribio ya kutosha kwa viumbe vingine sio binadamu, sio Watanzania. Nafikiri Mheshimiwa Waziri atuambie sasa kwa nini tunatumia dawa hizi, tunapata madhara ndio wanasema baadhi ya dawa hizi hazifai. Kwa nini wasifanye majaribio kwenye viumbe vingine ambavyo sio binadamu, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa dawa zenyewe, unapokwenda maduka ya dawa (pharmacy) unaambiwa unataka ya India, Ujerumani, Kenya au ya Tanzania, dawa hiyo hiyo ya aina moja, imesemwa kwenye semina, tatizo ni nini. Sasa kumbe ni kiwango cha ubora wa dawa zenyewe, nchi zinakotoka kuna ubora tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tunataka tujue Mheshimiwa Waziri atuambie sasa baadhi ya madhara wanayoyapata Watanzania baada ya kutumia dawa katika nchi fulani, nchi ambazo inaonekana dawa zake ni hafifu hazina standard inayotakiwa. Hilo pia Mheshimiwa Waziri atuambie ana mkakati gani wa ziada kuelimisha jamii juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya kulelea watoto yatima wanaoishi na VVU/UKIMWI na mazingira magumu. Mbona vitu hivi hamvipi umuhimu unaostahili? Ukienda katika maeneo mbalimbali unaona huruma, watoto hawa hawana lishe, masomo ni shida, nguo ni shida, ni tabu, lakini ukija hapa Serikali ukiwaambia wana mkakati gani wa ziada juu ya watoto hawa kujua maisha, masomo na lishe zao wanasema tuna mkakati wa ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote nikwambie, Serikali haitaki kukubali lile Azimio la Abuja la kutenga fedha inayostahili halafu wamewaachia wafadhili zaidi, umeona wapi wewe wa mwenye shamba unasema msaidizi mwenye shamba ndio atamaliza hiyo kazi. Hili ni jambo moja kubwa ambalo linatia wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti hasa wa takwimu za hali ya maambukizi ya VVU na UKIMWI. Ukiangalia TACAIDS, TACOSOA na mashirika mengine unaambiwa kwamba Dodoma ni 2.9, ukienda TACAIDS 2.9 na TACOSOA 2.9 na wewe ni mjumbe lakini ukikaa Dodoma yenyewe ukisoma mazingira ya Dodoma yenyewe, ukikaa na wataalam mbalimbali na ukifanya uchunguzi vizuri hospitali mbona mnadanganya watu Dodoma ni zaidi ya 2.9, tusidanganyane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ambazo mnazitoa sio halisia, ni kwa nini ukienda TACAIDS 2.9, TACOSOA 2.9 Mheshimiwa Waziri mnapofanya sherehe mbalimbali hapa Dodoma waambieni hali halisi ya ukweli ulivyo. Ukiangalia hali halisi hapa na pale mikusanyiko mikubwa ya watu, vyuo vya hapa zaidi ya wanafunzi 15,000. Ukiangalia hapa madereva wanaosafiri masafa marefu wanakaa hapa na mambo mengine mbalimbali yapo hapa. Sasa waambieni ukweli wananchi wa Dodoma kwamba hali sio shwari sana, lakini mnawapa moyo aah! Dodoma ipo vizuri sana ni 2.9 jamani mnataka muwamalize hata Dodoma, shauri yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka nizungumzie ni suala zima la swali langu la asubuhi, suala la posho ya kufundishia kwa Walimu (teaching allowance). Huu ni mwaka wa sita tangu Serikali ikubali kwamba Walimu watapatiwa posho ya kufundishia, tangu Oktoba mwaka 2012 mpaka leo Walimu hawajapatiwa teaching allowance, wamepewa Wakuu wa Shule na Waratibu, wamepewa peke yao hao tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika hapa, Serikali wanasema aaa tupo katika mkakati, Serikali ni sikivu, imepanga mikakati madhubuti, si muda mrefu Walimu watapata hizo fedha. Tunataka Mheshimiwa Waziri wa Elimu atuambie, simwoni sijui yuko wapo, yupo kule pembeni, atuambie sasa ni lini Walimu watapata teaching allowance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.