Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kusimama wakati huu nikiwa na afya njema. Napenda kumshukuru aliyewasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani na Waziri kwa kutambua umuhimu wa kilimo nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda kusema miongoni mwa wakulima tunaowazungumzia leo ni pamoja na wakulima wa Mkoa wa Rukwa. Kuna shamba ambalo Wabunge wangu wa Mkoa wa Rukwa wamelizungumza kwa miaka kadhaa humu ndani, tena ni wa Chama cha Mapinduzi, yawezekana hamkuwasikiliza kwa sababu ni Chama cha Mapinduzi leo nasimama kupitia CHADEMA kuzungumzia shamba hilo hilo ili mtambue kwamba ni suala ambalo linawagusa wananchi moja kwa moja, shamba la EFATHA, Manispaa ya Sumbawanga, Kijiji cha Isesa imekuwa ni sehemu ya watu kwenda kufanya kampeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili limetamkwa hapa ndani akiwa Waziri Mkuu Pinda kwamba anakwenda kulishughulia, lakini mpaka leo hakuna kilichofanyika. Sijajua speed mlionayo Chama cha Mapinduzi na kama mna nia njema na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga. Wananchi wale kwa sababu ni miongoni mwa watu waliowapa kura na sasa mnajiita ni kazi tu mmeacha porojo nendeni mkashughulikie suala lile, muache story mfanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitazungumzia suala moja ambalo ni kero kubwa kwa Watanzania hasa wakulima. Mimi ni miongoni mwa watoto waliotoka kwa wakulima tena wanaolima kilimo cha mkono. Nasikitika Waziri hayupo hapa alisema anataka jembe likae kwenye jengo la kumbukumbu, lakini angejua kwamba Manispaa ya Sumbawanga asilimia kubwa ya wakulima wanalima kwa mkono wanapata gunia mbili au tatu kwa mwaka lakini wanalipa kodi kwenye nchi hii wakati huo huo ni miongoni mwa wakulima ambao wanapata mateso mpaka wanajiona ni kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Analima kwa mkono, kutoa mazao yake shambani kuyapeleka sokoni anakamatwa njiani alipie kodi. Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Rais alipokuja hapa alipokuwa anazindua Bunge alizungumzia habari ya tozo zisizokuwa na tija, lakini mpaka leo kama mlikuwa serious mngekuwa mmeonyesha hatua. Hakuna kitu, zimekuwa ni story za miaka yote.
Mimi nawashauri, siku hizi Watanzania wanaelewa mnapotamka kitu mwende kwa vitendo, msitamke tu halafu mkanyamaza, mnapotamka tayari Watanzania wamesikia wanabaki kusubiri utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao haya tunayozungumzia ndugu zangu Wabunge tukiwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo kuna mkulima analipia mpaka mwenge, huu mwenge unakwenda kumsaidia nini mkulima, unammulikia nini shambani? Imefikia mahali hizi tozo hata wanaosimamia inaonekana kama kuna hali fulani ya upofu wa kutokutazama mbele. Wakulima hawa ni miongoni mwa watu ambao wanachangia pato kubwa la Taifa katika nchi hii, mmekuja na kauli mbiu nyingi sana lakini kauli mbiu hazijasaidia chochote imebaki story tu na mnaongoza kwa kupanga vitu kwenye karatasi, lakini utekelezaji mna zero positive. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la masoko, unapozungumzia viwanda, Waziri wangu naona ametoka, alisema Sumbawanga atajenga kiwanda, mimi nataka nimwambie Mkoa wa Rukwa tunalima mahindi, maharage, ngano na ulezi na pia kuna wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapozungumzia Serikali ya viwanda mpaka leo mmetoa elimu kiasi gani kuonesha kwamba mko serious na viwanda mnavyovizungumza? Kwa sababu hata wakulima wataona mnachokizungumza ni sawa na story za siku zote walizowahi kusikia. Kama elimu hamjatoa, halafu mnawaambia kwamba wao wanatakiwa kujenga viwanda wakati hawajaona utofauti wa wao walivyokuwa wanalima na leo unavyowaambia kwamba wapeleke kwenye viwanda, viwanda vinawasaidia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikaji wa pembejeo, sidhani kama huwa hamsikii siku zote tunavyokuwa tunawashauri. Kabla sijaingia kwenye hili Bunge mmeshauriwa mara nyingi sana. Kuna sehemu mpaka mnawaambia Wenyeviti wa Serikali washiriki kuandaa zile Kamati. Ukitazama Mkoa wa Rukwa hasa Manispaa ya Sumbawanga, huyo Mwenyekiti anayeshughulikia pembejeo, halafu mnapokuja mnakuwa mmeweka watu wenu mnaowajua, analipwa shilingi 5,000 baada ya miezi mitatu. Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa leo inamkopa hiyo shilingi 5,000 kwa miaka mitano..
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niwaambie Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama mko serious na mnatambua umuhimu wa kilimo katika nchi hii nendeni mkafanye utafiti kwanza. Unapozungumzia viwanda lazima ujue kabla ya viwanda wananchi walikuwa na changamoto zipi. Kama soko mlishindwa kutafuta mlipokujana na kauli mbiu ya kilimo kwanza ikawa kilimo mwisho, viwanda leo vitakwenda kumkomboa Mtanzania kwa style ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la hawa Maafisa Kilimo kuna wengine wako mjini na Mkoa wa Rukwa utakuta wale wakulima hawamfahamu. Yeye faida yake kuwepo kule ni nini, hakuna faida ambayo mkulima anaiona. Inabidi tusiwalaumu wataalam hawa, yawezekana hamjawawezesha wanawafikiaje wakulima hawa. Kwa hiyo, nawashauri Chama cha Mapinduzi kama mna nia njema na wakulima wa nchi hii hasa wa Mkoa wa Rukwa wawezesheni hawa Maafisa Kilimo wakatimize wajibu wao wa kutoa elimu kwa wakulima hawa ili kilimo hiki kilete tija ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la utabiri wa hali ya hewa, yawezekana ni Nyanda za Juu Kusini peke yake, Mkoa wa Rukwa kipindi cha nyuma walikuwa wanalima kutumia utabiri wao wa kawaida, wa Kifipa ule, wakitazama ndege wanajua kwamba safari hii kuna mvua nyingi au chache lakini walikuwa wanapata vizuri kuliko leo wakiambiwa kuna mvua nyingi wanapolima mvua haiji. Naomba hawa watabiri wa hali ya hewa utabiri wao uwe ni wenye tija, usiwe na hasara kwa Watanzania na wanapofanya utabiri wasifanye utabiri wa Dar es Salaam kwani huko hakuna wakulima, wafanye utabiri kwa kuangalia wakulima wa vijijini hasa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la uvuvi kwa sababu wavuvi pia wako Mkoa wa Rukwa. Wavuvi katika Taifa hili hususani Mkoa wa Rukwa imekuwa ni Mkoa ambao wamenyang‟anywa sana vifaa vyao kwamba ni haramu, hivi viwanda vinavyozalisha hivi vitu hamjui viko wapi? Yawezekana hata kodi mnachukua lakini mkifika mnawaambia vifaa vyao ni haramu, kwa nini msiende kwenye viwanda vinavyozalisha?
Mimi naomba kuwaambia hawa Watanzania wapo kama ninyi ambao leo ni Mawaziri lakini mlikuwa kama wao na mlitazame hili kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia kwamba na wao wanastahili kuishi kwa amani katika nchi yao wasijione kama wakimbizi ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Ziwa Rukwa amelizungumza jana Mama Maufi, yule ni Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, hili suala limesemwa sana humu ndani na Mbunge wa Kwela, sasa tunaomba tunapowaambia mchukue hatua. Inafikia mahali mnapokuwa mnajiita ninyi ni Serikali sikivu hata mtu ambaye alikuwa haelewi anajitokeza kuja kusikiliza kwamba huyu anayesema anasema kitu gani kwa sababu kama mmeambiwa mara moja, mmeambiwa mara ya pili kitu gani kinazuia msiende kutekeleza, shida ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bajeti ya kilimo mnayokuwa mnatenga kama mna nia ya kuboresha kilimo, hizi fedha ni za wapi, mkitegemea fedha za nje mnakwenda kufanya nini au mnakuja kucheza comedy hapa ndani ya Bunge na kutudanganya? Huwezi kupanga kwenda kufanya kitu unategemea mhisani akupe fedha wakati wewe hujajipanga una kiasi gani? Kama mko serious kweli basi Taifa litazame kwamba kilimo ni uti wa mgongo kama mlivyokuwa mmesema mara ya kwanza. Mambo mnayofanya hayafanani na hiki mnachokizungumza. Niombe kauli mbiu zenu ziendane na kile mnachokifanya. Hatutachoka kuwashauri lakini msiposikia tutatumia kauli nyingine ya kuwaambia maana kauli ya kawaida naona ni ngumu sana kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu, hivi mnaweza mkaboresha kilimo bila kuwa na miundombinu ya uhakika? Kwa mfano, Wilaya yangu ya Nkasi pale Namanyere toka Mheshimiwa Rais wa leo akiwa Waziri alitamka hapa akasema Wafipa hawajawahi kuona hata lami, nilijua anatania maana alisema watani wangu mpaka leo hakuna lami, kwa hiyo, alikuwa serious kwamba kweli Wafipa watabaki kuwa hivyo. Kwa hiyo, nawashauri hawawezi kulima halafu hawana barabara ambayo itawafanya wafike sokoni kupeleka mazao yao. Muwe serious kutazama kwamba kilimo kinakwenda sambamba na miundombinu na mfanye hayo mkiwa mnamaanisha kwamba kweli mpo serious kuboresha kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.